Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Iran, Amir Ghalenoei, amesema kuwa ‘Team Melli’ ndiyo “timu inayodhulumiwa zaidi katika historia ya Kombe la Dunia la FIFA.”

Ghalenoei ameikosoa vikali Marekani kwa kuibagua timu hii ya taifa ya soka ya Iran kwa kuilazimisha kuondoka nchini humo mara moja baada ya mchezo wao wa ufunguzi uliochabangwa mjini Los Angeles. Akizungumza baada ya sare ya 2-2 dhidi ya New Zealand katika Uwanja wa Los Angeles siku ya Jumanne, Ghalenoei aliwasifu mashabiki wa Iran waliofurika uwanjani hapo.

Amesema: “Anga ya leo ilikuwa hatua muhimu katika historia ya mpira wetu wa miguu. Takriban Wairani 70,000, licha ya tofauti zao, waliishangilia Team Melli kwa sauti moja, na huo ndio ulikuwa ushindi wetu mkubwa zaidi.”Hata hivyo, kocha huyo alielezea mazingira yasiyokubalika yanayoikabili timu hiyo akisema: “Team Melli iko katika hali ngumu sana. Hatukupewa muda wa kutosha wa maandalizi na mapumziko, na hata baada ya mechi hii, tunalazimika kurejea mara moja Tijuana. Hali hii inatupa shinikizo kubwa sana.”

Amesema kuwa awali timu ilipanga kuweka kambi yake ya mazoezi mjini Tucson, Arizona, lakini matatizo ya viza na uratibu yaliwalazimisha kuhamia Tijuana, Mexico, katika dakika za mwisho.

Ghalenoei ameongeza: “Walichelewesha kuwasili kwetu, na sasa wanatulazimisha kuondoka mapema bila muda wa kupumzika. Wanazidi kufanya hali kuwa ngumu na kutuwekea vikwazo zaidi. Lakini hatutaruhusu hilo lituzuie kufanya juhudi zetu zote. Ndiyo maana naamini sisi ndio timu inayodhulumiwa zaidi katika Kombe la Dunia.”

Ghalenoei amehitimisha kwa kupongeza ari ya wachezaji wake licha ya changamoto hizo: “Wachezaji wamejitolea kwa kila hali na kupigana kwa ajili ya wananchi licha ya matatizo yote.”

Nahodha wa timu hiyo, Mehdi Taremi, naye amekosoa vikwazo hivyo vilivyowekwa na Marekani akisema kuwa hali ya kutokuwa na uhakika inaathiri kikosi kiakili na kimwili.

“Bado tuna matatizo mengi,” mshambuliaji huyo wa klabu ya Olympiacos aliwaambia waandishi wa habari baada ya mchezo.

Aliendelea kusema kuwa timu imekuwa ikikabiliana na changamoto kwa miezi kadhaa na kuyataja mazingira yanayozunguka ushiriki wa Iran kuwa ni “janga la kweli.”

Amesema: “Kuna shinikizo kubwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na kila mmoja, hatuna uungaji mkono tunaouhitaji.”

Ameongeza kuwa: “Nadhani FIFA inapaswa kutusaidia zaidi. Walituambia kuwa watatusaidia, na tutaona nini kitatokea siku zijazo.”

Hali hii inakuja huku kukiwa na ukosoaji unaoongezeka dhidi ya namna Marekani inavyoshughulikia ushiriki wa Iran katika Kombe la Dunia, linaloandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada, na Mexico.

Ingawa wachezaji wa Iran hatimaye walipata visa ya kusafiria, maafisa kadhaa muhimu wa benchi la ufundi na shirikisho la mpira wa miguu walinyimwa viza na mamlaka za Marekani kabla ya mashindano kuanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *