
Ripoti hiyo mpya ya mashirika hayo inayobainisha maeneo hatari ya njaa iitwayo kwa lugha ya kiingereza “Hunger Hotspots” iliyotolewa leo mjini Roma nchini Italia, imebainisha kuwa nchi za Sudan, Sudan Kusini, Yemen, na Palestina ndizo zinazoongoza kwa kuwa na hali mbaya zaidi duniani, huku Nigeria na Somalia zikitajwa kuingia kwenye hatua ya hatari kubwa ambapo hatari ya njaa inakaribia viwango vya maafa. Vita, machafuko, matatizo ya kiuchumi, na mabadiliko ya tabianchi kama vile kimbunga cha El Niño vinatajwa kuwa vyanzo vikuu vinavyosukuma mamilioni ya watu kwenye janga hili.
Takwimu zadhihirisha hali mbaya ya njaa
Nchini Sudan, watu wapatao milioni 19.5 tayari wanakabiliwa na njaa kali, huku hatari ya ukame na njaa ikitarajiwa kuendelea hadi mwezi Januari mwaka 2027 katika maeneo 13. Kwa upande wa Sudan Kusini, takriban watu milioni 7.8 wanatarajiwa kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku kaunti nne zikiwa kwenye hatari ya kukumbwa na njaa ifikapo mwezi Julai mwaka 2026.
Hali kadhalika nchini Yemen, zaidi ya nusu ya idadi ya watu (watu milioni 18.3) wamekadiriwa kuwa katika hatari kubwa ya njaa, wakati nchini Nigeria, karibu watu milioni 34.8 wanatarajiwa kuathirika vibaya kati ya mwezi Juni na Agosti mwaka 2026, hasa katika jimbo la Borno.
Huko Palestina, ingawa hali imetulia kidogo tangu kusitishwa kwa mapigano mwezi Oktoba mwaka 2025, takriban watu milioni 1.6 katika Ukanda wa Gaza bado wapo hatarini na wanahitaji misaada ya dharura.
Uhaba mkubwa wa fedha za misaada na hatua zinazotakiwa kuchukuliwa
Ripoti hii imetolewa katika kipindi ambacho kuna upungufu mkubwa wa fedha za msaada wa kibinadamu usio na kifani, kwani rasilimali za kusaidia chakula na kilimo cha dharura zimeshuka kwa asilimia 59 kati ya mwaka 2022 na 2025. Wakati huohuo, idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa kali imeongezeka hadi kufikia karibu watu milioni 266 katika nchi hizo.
Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, ameeleza kuwa, “uwekezaji wa mapema katika kilimo cha dharura ndiyo njia bora na ya gharama nafuu ya kulinda maisha ya watu na kupunguza mahitaji ya kibinadamu ya baadaye kabla ya masoko na mifugo kuharibika.”
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau, amesisitiza kuwa onyo hili halipaswi kupuuzwa kwani migogoro na majanga vinalazimisha familia kufanya maamuzi magumu ya nani ale na nani alale njaa.
“Timu zetu ziko tayari kutoa misaada kwa haraka, lakini tunahitaji rasilimali fedha na njia salama za kuwafikia watu kabla njaa haijageuka kuwa maafa makubwa,” ameongeza Carl Skau.
Mbali na maeneo hayo yenye hatari kubwa, nchi kama Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambayo inakabiliwa pia na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola pamoja na Haiti, zimetajwa kuwa katika maeneo yenye wasiwasi mkubwa, huku nchi za Lebanon na Madagascar zikiwa zimeongezwa hivi karibuni kwenye orodha hiyo kutokana na vita na hali mbaya ya hewa.