Mary Chigumira raia wa Zimbabwe, ambaye Kiswahili si lugha mama yake bali anaipenda na anajifunza hivyo ikabidi kuendelea mazungungumzo yetu kwa lugha ya Kiingereza, ni mwanzilishi wa shirika hilo la Unlimited Hope Alliance, linalotoa tumaini kwa waliopoteza matumaini, likiwasaidia wanawake na wasichana waliokumbwa na ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na umasikini.

“Shirika letu linajikita na wanawake na wasichana. Tuna miradi ya elimu, ajira endelevu, maji, usafi na afya. Tunawawezesha manusura wa ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia GBV na hata wale waliokuwa kwenye biashara ya ngono.”

UN News Mary Chigumira raia wa Zimbabwe akizungumza na Flora Nducha wa UN News Kiswahili.

Mary amesema kupitia mkutano aloihudhuria amejifunza umuhimu wa miradi endelevu inayowaachia wanawake ujuzi wa kuendelea kujitegemea hata baada ya wafadhili kuondoka.

Amesisitiza pia kuwa mapinduzi ya kidijitali hayawezi kufanikiwa ikiwa wanawake wa maeneo ya vijijini wasiokuwa na umeme wala intaneti wataachwa nyuma.

“Tukizungumzia masuala ya kidijitali lazima tuwakumbuke wanawake wa vijijini. Kama hakuna umeme au intaneti na bado tunasema tusimuache mtu nyuma, basi hatutafikia malengo yetu.”

Kwa mujibu wa Mary shirika lake linashirikiana na wafadhili wa ndani pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo UN Women  shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake na hasa katika mafunzo na kujenga uwezo kwa wanawake na wasichana.

Kwa sasa amesema wamewasilisha pendekezo kwa UN Women la kuendesha mkutano wa wilaya kuhusu ndoa za utotoni na maambukizi ya VVU nchini Zimbabwe.

Na wakati viongozi wa dunia wakijiandaa kwa mjadala wa Baraza Kuu baadaye mwaka huu Mary ana ujumbe mmoja ulio wazi kwao lakini pia kwa wasichana wanaopitia changamoto.

“Kwa viongozi wa dunia, tunawaomba wafanye kazi pamoja nasi. Hatuwezi kutembea peke yetu. Na kwa wasichana, haujachelewa. Hata kama ulipata mtoto ukiwa na miaka 14, huo sio mwisho wa maisha. Inawezekana kusimama tena na kujenga maisha yakom inawezekana.”

Kwa mujibu wa Mary, uwekezaji katika elimu, teknolojia na uwezeshaji wa wanawake wa vijijini ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo jumuishi duniani kote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *