Mbunge wa Pangawe, Haji Amour Haji, ameipongeza Serikali kwa kuwasilisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, akisema imepangwa vizuri na ina maono ya kuleta maendeleo iwapo itatekelezwa kwa ufanisi.

Akichangia bungeni, Mbunge huyo amesema bajeti hiyo imejikita katika mikakati ya kukuza uchumi wa taifa na kuboresha maisha ya wananchi kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji na miundombinu.

Amesema miongoni mwa malengo makuu ni kukuza uchumi kufikia asilimia 6.3, kuongeza mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa misaada hadi asilimia 17.1 ya pato la taifa, pamoja na kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli.

Aidha, amebainisha kuwa bajeti hiyo inalenga kukuza viwanda, kuongeza thamani ya malighafi, kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na mafunzo ya ujuzi, pamoja na kuongeza ajira hususan kwa vijana na wanawake kupitia sekta binafsi.

Pia amesema Serikali inatarajia kudhibiti mfumuko wa bei kati ya asilimia 3 hadi 5, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, na kuongeza matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika uchumi na ukusanyaji wa mapato.

Haji ameongeza kuwa mafanikio ya malengo hayo yatategemea usimamizi madhubuti wa mapato na matumizi ya serikali, pamoja na kuimarisha miundombinu, rasilimali watu na kukuza ujasiriamali nchini.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *