Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa filamu za Afrika Kusini, ni ngumu kutotaja jina la Sdumo Mtshali staa anayeng’ara kwa zaidi ya miaka 15 katika upande huo wa Burudani.
Sdumo Mtshali ambaye anatikisa kwenye series ya ‘The Polygamist’ akitumia jina la Jonasi, alizaliwa Machi 3, 1983 katika Hospitali ya King Edward, Durban, Afrika Kusini. Tangu akiwa mtoto alikuwa na ndoto ya kuwa mwigizaji.
Alisomea masomo ya sanaa ya uigizaji katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Durban (Durban University of Technology), ambapo alianza kujenga msingi wa taaluma yake ya baadaye.
Kabla ya kupata umaarufu, Sdumo alifanya kazi mbalimbali za kawaida ili kujikimu. Hata hivyo, moyo wake uliendelea kuvutwa kwenye sanaa ya uigizaji na maigizo ya jukwaani.
Mwaka 2010 ulikuwa wa kihistoria kwa Sdumo baada ya kushiriki na kushinda shindano maarufu la vipaji vya uigizaji la ‘Class Act’ lililoonyeshwa na SABC1. Ushindi huo ulimfungulia milango mingi katika tasnia ya burudani.
Kama sehemu ya zawadi yake, alipata mafunzo ya uigizaji katika New York Film Academy. Muda mfupi baada ya ushindi huo, alipata nafasi yake ya kwanza kubwa katika tamthilia ya Intersexions, ambayo ilimfanya aanze kutambulika kwa watazamaji wengi wa Afrika Kusini.
Baada ya mafanikio ya Intersexions, Sdumo aliendelea kuonekana katika tamthilia na filamu mbalimbali zilizomjengea jina kubwa miongoni mwa hizo ni Intersexions, Rhythm City, Tempy Pushas, Isibaya, iNumber Number, Avenged na nyinginezo.
Kutokana na vipaji vyake, Sdumo amepokea uteuzi na tuzo mbalimbali katika uigizaji. Mwaka 2019 alishinda tuzo ya SAFTA Golden Horn Award ya Mwigizaji Bora Msaidizi katika tamthilia ya Is’Thunzi. Pia amepata uteuzi kadhaa katika tuzo za SAFTA kwa kazi zake katika Isibaya, Saints & Sinners na iNumber Number: Jozi Gold.
Aidha, mwaka 2015 alipata uteuzi wa African Movie Academy Awards (AMAA) katika kipengele cha Muigizaji Bora kwa filamu ya Avenged. Mafanikio haya yamemfanya kuwa mmoja wa waigizaji wanaoheshimika zaidi katika kizazi chake nchini Afrika Kusini.
Licha ya umaarufu wake mkubwa, Sdumo Mtshali ni mtu anayependa kuweka maisha yake ya familia mbali mitandao. Katika mahojiano mbalimbali amewahi kueleza kuwa familia yake na imani yake kwa Mungu vimekuwa nguzo muhimu katika mafanikio yake ya muda mrefu.
Aidha mwaka huu 2026, Sdumo alipata nafasi nyingine kubwa kupitia tamthilia ya Netflix inayoitwa ‘The Polygamist’. Katika tamthilia hiyo anaigiza kama Jonasi Gomora, mfanyabiashara tajiri na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni kubwa ambaye maisha yake ya kifamilia yanaanza kuyumba kutokana na maamuzi yake ya kuoa wake wengi.
Tamthilia hii imetokana na riwaya maarufu ya mwandishi wa Zimbabwe, Sue Nyathi. Hadithi hiyo inaangazia mapenzi, usaliti, madaraka na changamoto zinazotokana na mfumo wa ndoa za wake wengi.