
Mchakato huo uliongozwa na Tume ya Kitaifa ya Sudan Kusini ya usalimishaji silaha na ujumuishaji kwenye jamii, DDR cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), pamoja na mamlaka za serikali za jimbo la Equatoria Magharibi. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukomesha matumizi ya watoto katika vikosi vya ulinzi na makundi yenye silaha.
Video ya UNMISS inaonesha watoto waliokuwa wamehusishwa na vikosi vya ulinzi wakipokelewa katika kituo cha mpito mjini Yambio. Baadhi yao wamevalia mavazi ya kiraia huku wakisikiliza maelekezo kutoka kwa maafisa wa ustawi wa jamii, hatua inayoweka msingi wa kurejea kwao katika maisha ya kawaida.
Oluku Andrew Holt, Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa DDR kwa Watoto Wanaohusishwa na Vikosi vya Ulinzi na Makundi Yenye Silaha (CAAFAG), anaeleza umuhimu wa kuwalinda watoto dhidi ya kuingizwa katika shughuli za kijeshi.
“Hizi ni sare za kijeshi tulizozikuta kwa watoto waliotaka kuwa wanajeshi, lakini kutokana na umri wao hawastahili kupewa mafunzo kama sehemu ya jeshi la taifa la Sudan Kusini. Sera ya jeshi iko wazi, Katiba iko wazi, pamoja na Sheria ya Mtoto, kwamba hakuna mtu mwenye umri chini ya miaka 18 anayepaswa kusajil iwa au kutumiwa katika shughuli za kijeshi.”
Video ya UNMISS inaonesha watoto waliokuwa wakihusishwa na vikosi vya kijeshi wakikabidhiwa mabegi na mavazi yenye nembo ya UNICEF, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kurejea katika maisha ya kiraia. Baada ya kuachiliwa, watoto hao wanapatiwa msaada wa kina unaolenga kuwasaidia kujenga upya maisha yao, ikiwemo kupata elimu, mafunzo ya ufundi stadi na huduma za ushauri nasaha. Msaada huo unalenga kuwawezesha kujitegemea, kurejesha matumaini yao na kuwapa fursa ya kufikia malengo na ndoto zao za baadaye.
Clement Gbatanawo, Mkuu wa Ofisi ya UNICEF Yambio, anasema uwekezaji katika elimu na mafunzo ya ufundi ni muhimu kwa mustakabali wa watoto hao.
“Baadhi ya watoto hawa ambao sasa wana umri wa karibu miaka 17 waliondoka nyumbani au waliingizwa katika vikosi vya ulinzi walipokuwa na umri wa miaka saba au kumi tu. Katika Shule ya Ufundi ya Tindoka hapa Yambio, tunatoa mafunzo ya umeme, ushonaji, uashi na uchomeleaji vyuma. Kupitia ujuzi huu wanaweza kujijengea maisha bora ya baadaye. Kwa watoto wadogo zaidi, tutawasaidia kurejea shuleni.”
Kuachiliwa kwa watoto hao ni hatua muhimu katika utekelezaji wa juhudi za kitaifa na kimataifa za kuwalinda watoto dhidi ya madhara ya migogoro ya silaha na kuhakikisha haki zao zinaheshimiwa.
Rita Bampo, Afisa wa Ulinzi wa Mtoto wa UNMISS katika Ofisi ya Yambio, anasema Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha watoto wanalindwa.
“Katika zoezi hili la uhakiki, tulibaini wavulana watano wenye umri kati ya miaka 16 na 17 ambao wameachiliwa na kukabidhiwa kwa UNICEF kwa ajili ya kurejeshwa katika jamii. UNMISS itaendelea kuisaidia Serikali ya Sudan Kusini kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kina wa kuzuia na kukomesha ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.”
Watoto hao sasa wana nafasi ya kurejea kwa familia zao, kuendelea na masomo, kujifunza stadi za maisha na kujenga mustakabali wenye matumaini. Simulizi hii inaonesha jinsi ushirikiano kati ya serikali, Umoja wa Mataifa na wadau wengine unavyoweza kubadilisha maisha ya watoto walioathiriwa na migogoro na kuwapa nafasi ya kuanza upya.