
Maboresho hayo yanajumuisha ujenzi wa vyumba binafsi vya kutenga wagonjwa vinavyokidhi viwango vya kudhibiti maambukizi na kuongeza tanki la maji lenye uwezo wa lita 10,000 ili kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika kwa ajili ya huduma za wagonjwa na shughuli za kituo hicho.
WHO imesema uwekezaji huo unalenga kutoa huduma salama zaidi kwa wagonjwa huku ukipunguza hatari ya maambukizi ndani ya vituo vya afya.
Dalili za mafanikio huku changamoto zikiendelea
Akizungumza katika mkutano wa ngazi ya juu kwa njia ya mtandao wa Wakuu wa Nchi za Afrika na washirika kuhusu mlipuko wa Ebola aina ya Bundibugyo jana Juni 16 Juni, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kuna dalili za maendeleo licha ya changamoto zinazoendelea kufuatia ziara yake ya hivi karibuni katika jimbo la Ituri.
“Nilishuhudia mnepo, niliona kujitolea na niliona matumaini,” alisema. “Uwezo wa matibabu unaongezeka, na tunaona wagonjwa wakipona.”
Hata hivyo, Dkt. Tedros ameonya kuwa uwezo wa upimaji na maabara bado haujafikia kiwango kinachohitajika ili kukatiza maambukizi ya ugonjwa huo. Amesema pia hali ya ukosefu wa usalama, watu kuhama makazi yao na harakati za mara kwa mara za wananchi vinaendelea kuathiri juhudi za kudhibiti mlipuko huo. Aidha, ameeleza kuwa ukosefu wa imani kwa jamii kwa wahudumu wa afya na mashirika ya kimataifa ni kikwazo kikubwa katika mapambano dhidi ya Ebola.
WHO yapinga vikwazo vya usafiri vya jumla
Dkt. Tedros amesema alijionea mwenyewe changamoto zinazowakabili wahudumu wa afya na wananchi wa Bunia, ambako mashaka dhidi ya timu za hatua za kupambana na Ebola bado ni makubwa.
“Kutokuwa na imani kwa jamii ni kikwazo kikubwa katika mlipuko huu kwa sababu jamii hizi zinahisi na huenda ziko sahihi kwamba dunia ya nje inataka kujilinda yenyewe dhidi ya Ebola na haijali kwa dhati maisha yao,” alisema. Kwa mujibu wa WHO, kujenga imani kupitia huduma bora za afya na ushirikishwaji wa jamii ni jambo muhimu katika kudhibiti mlipuko huu.
Mkuu huyo wa WHO pia amekosoa vikwazo vya usafiri vilivyowekwa na baadhi ya nchi kutokana na mlipuko huo, akisema vina madhara zaidi kuliko manufaa. “Vikwazo vya jumla vya usafiri vinavuruga minyororo ya usambazaji wa vifaa na kuathiri operesheni za hatua bila kushughulikia chanzo halisi cha maambukizi,” alisema.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 50 tangu Ebola ilipogunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika, ni wagonjwa wanne pekee waliowahi kurekodiwa kwa wasafiri kutoka Afrika, bila kujumuisha wagonjwa waliohamishwa kwa matibabu.
WHO inapendekeza hatua mahsusi za afya ya umma kama vile uchunguzi wa wasafiri katika maeneo ya kuondokea badala ya kufunga mipaka au kuweka vikwazo vya jumla.
Zaidi ya hatua za dharura
Changamoto nyingine kubwa ni kwamba kwa sasa hakuna chanjo wala tiba zilizoidhinishwa dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo. Hata hivyo, Dkt. Tedros alitangaza kuwa majaribio ya kitabibu ya dawa zinazotia matumaini kwa ajili ya matibabu na kinga yanatarajiwa kuanza katika wiki zijazo, huku majaribio ya chanjo yakihitaji muda zaidi.
Licha ya hali hiyo, amesisitiza kuwa mlipuko huo unaweza kudhibitiwa kwa uongozi thabiti wa serikali na ushirikiano wa karibu wa wadau wote. “Chini ya uongozi wa serikali, tunaweza kuushinda mlipuko huu hata bila chanjo au tiba maalum, kama tulivyofanikiwa kudhibiti milipuko 16 ya Ebola iliyopita nchini DRC,” amesema.
Akizungumzia mustakabali wa muda mrefu, Dkt. Tedros ametoa wito kwa serikali na washirika kushughulikia sababu za msingi zinazochangia milipuko ya Ebola, ikiwemo usalama wa chakula na maambukizi ya magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma muhimu za afya, kuweka njia salama za misaada ya kibinadamu katika maeneo yenye migogoro na kuongeza uwezo wa Afrika kuzalisha chanjo na bidhaa nyingine za matibabu.
“Iwapo tutawalinda watu hawa dhidi ya Ebola lakini si dhidi ya malaria, uzazi usio salama, surua, utapiamlo au migogoro isiyosababishwa na wao, basi hatujawasaidia kikamilifu,” amesema.
Akihitimisha taarifa yake, amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda na kimataifa akisema, “Hili si jukumu la DRC pekee. Sote tuko pamoja katika mapambano haya. Kwa pamoja tunaweza kuumaliza mlipuko huu.”