Matamshi ya balozi wa Marekani huko Israel, Mike Huckabee, yamezua wimbi la hasira na ukosoaji mkubwa katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani, baada ya kusema kwamba Marekani “haingekuwepo bila Israel,” katika taarifa iliyozusha mjadala mkubwa kuhusu ushawishi wa Israel ndani ya duru za kufanya maamuzi za Marekani na mipaka ya majukumu ya balozi wa Marekani huko Tel Aviv.

Matamshi ya Huckabee yametolewa katika ufunguzi wa “Mkutano wa Kimataifa kuhusu Urithi wa Israel” uliofanyika katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu huko Palestina, ambapo alisema jukumu lake “sio tu kuiwakilisha Marekani Israel, lakini pia linajumuisha kuwakilisha umuhimu wa Israel kwa Wamarekani.”

Aliongeza akimwambia Waziri wa Urithi wa Israel Amichai Eliyahu: “Bila shaka huu ni urithi wako, lakini mheshimiwa, huu pia ni urithi wa Marekani. Bila Israel, na bila msingi wa Kiyahudi, Marekani isingekuwepo.”

Matamshi hayo ya balozi wa Marekani huko Israel yanapata umuhimu wa pekee kwa sababu yametolewa saa chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kusema kuwa Israel “isingekuwepo bila Marekani,” jambo ambalo limewafanya wengi kuyatambua matamshi ya balozi huyo wa Marekani kuwa ni jibu kwa rais wake, na kuibua wimbi la mijadala na ukosoaji ndani ya Marekani.

Matamshi hayo ya balozi Mike Huckabee yameibua wimbi kubwa la ukosoaji katika duru za kisiasa na vyombo vya habari vya Marekani na kwenye mitandao ya kijamii, ambapo wakosoaji wameyataja kuwa ni ushahidi wa upendeleo wa balozi wa Marekani kwa Israel kwa gharama ya maslahi ya Marekani, huku wengine wakitaka afukuzwe au ajiuzulu wadhifa wake.

Mbunge wa chama cha Republican, Marjorie Taylor Greene alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa kwanza kukosoa matamshi ya Huckabee kupitia jukwaa la X, akisema: “Uwepo wetu unahusishwa na Mungu, si Israel,” na ameyataja matamshi yake kuwa ni “machafu.”

Mchambuzi wa kisiasa wa Marekani, Anna Kasparian amedhihaki matamshi ya Huckabee, akisema kwamba Marekani haikuundwa kwa sababu ya fadhila za Israel kama anavyodai, na ametoa wito wa kusitishwa misaada ya kifedha na kijeshi ya Marekani ili kuona kama Israel inaweza kuishi bila msaada wa Washington.

Afisa mstaafu wa jeshi la Marekani na mchambuzi wa masuala ya kijeshi Daniel Davis amemtaka balozi wa Marekani huko Israel, Mike Huckabee ajiuzulu wadhifa wake, akisema kwamba balozi huyo “haweki mbele maslahi ya Marekani,” akisisitiza kwamba kazi yake kuu ni kuiwakilisha Marekani katika nchi nyingine, si kuitangaza Israel au kuipendelea kuliko nchi yake mwenyewe.

Katika muktadha huo huo, mwanaharakati wa kisiasa wa Marekani na mjumbe wa zamani wa kitaifa wa Chama cha Republican huko Texas, Trisha Hope, ametoa wito wa Huckabee kutimuliwa katika nafasi yake mara moja, akisema kwamba kauli zake zinaibua shaka kuhusu ustahiki wake wa kuendelea kuiwakilisha Marekani huko Israel.

Baadhi ya wakosoaji wameenda mbali zaidi, huku mchambuzi wa kisiasa Jackson Henkle akimtaja Huckabee kuwa ni “kibaraka wa Israel,” huku mwanaharakati Carolina akisema balozi huyo wa Marekani anamkosoa rasmi Rais Trump kwa niaba ya Israel.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *