DAR ES SALAAM: TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) inatarajia kuanzisha benki ya mifupa ambayo itakidhi mahitaji na kuwasaidia watu ambao wamepoteza mifupa kutokana na ajali au sababu zingine.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya utoaji huduma za kibingwa na ubingwa bobezi, Mkurugenzi wa MOI, Balozi Dk Mpoki Ulisubisya amesema wanajiandaa kuanza kutumia roboti katika utoaji wa huduma za matibabu za kubadilishaji wa nyonga na magoti hatua inayolenga kuongeza usahihi ,ubora na ufanisi wa huduma za kibobezi .

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka 30 taasisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika utoaji wa huduma za afya, utafiti na mafunzo, huku ikiweka mikakati ya kuendelea kuimarisha huduma zake katika miaka ijayo.

“MOI imeendelea kubuni na kutekeleza huduma mbalimbali za kibunifu, ikiwemo huduma za mkoba na programu ya ‘Back Stopping’, inayolenga kuanzisha na kuimarisha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi katika hospitali za mikoa mbalimbali nchini. Mikoa inayonufaika na mpango huo ni pamoja na Arusha, Mara, Kagera, Njombe na Ruvuma, hatua inayolenga kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu,”amefafanua .

Mgeni rasmi Katika uzinduzi wa maadhimisho hayo ambapo pia taasisi imeendesha Ibada Maalumu ya Shukrani ya miaka 30 ya MOI, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe, amewapongeza watumishi wa MOI kwa mchango wao mkubwa katika kuokoa maisha ya wananchi na kuendelea kuiwezesha taasisi hiyo kuwa kinara wa huduma za kibingwa ndani na nje ya Tanzania.

Dk Shekalaghe amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa watumishi wa kada zote, kuanzia ngazi za juu hadi za chini, ili kuhakikisha huduma bora na endelevu zinaendelea kutolewa kwa wagonjwa na wananchi kwa ujumla.

Aidha, ameitaka MOI kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii kuhusu kinga dhidi ya ajali, ambazo zimeendelea kuwa chanzo kikubwa cha majeraha yanayohitaji huduma za mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.

“Nipo tayari kuendelea kutoa ushirikiano wangu kwa MOI katika juhudi mbalimbali za kuboresha afya za wananchi na kuhamasisha elimu ya kinga dhidi ya ajali,” amesema Dk Shekalaghe.

Mkurugenzi mstaafu MOI ,Prof. Lawrence Mseru ameeleza kwa kina safari ya miaka 30 ya MOI, akibainisha hatua mbalimbali za ukuaji, mafanikio na mchango wa taasisi hiyo katika sekt a ya afya nchini.

“Miaka 30 ya MOI ni ushuhuda wa dhamira, ubunifu na kujitolea kwa watumishi wake. Tulianzia hatua ndogo lakini leo taasisi imekuwa kitovu cha ubingwa katika tiba ya mifupa, ubongo na mgongo kwa kiwango cha kimataifa,” amesema Prof. Mseru.

Taasisi imezindua rasmi tovuti ya MOI pamoja na MO Dewji Foundation Marathon, mbio zinazolenga kuhamasisha jamii na kuchangia matibabu ya zaidi ya watoto 600 wenye tatizo la vichwa vikubwa nchini.

Aidha katika kutambua mchango wa waasisi wa MOI , jengo la OPD Phase II limepewa jina la Dk Uma Grob, huku jengo la OPD Phase III likipewa jina la Prof Philemon Sarungi, kwa heshima ya mchango wao mkubwa katika maendeleo na historia ya taasisi hiyo.

Uzinduzi wa madhimisho ya miaka 30 ya MOI umekuwa fursa muhimu ya kutafakari safari ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuhakikisha taasisi inaendelea kuwa kituo kinachoongoza Afrika katika utoaji wa huduma za mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *