Hatari tatu zinazotishia makubaliano ya Iran na Marekani

Tayari umakini umeelekezwa kwenye maeneo makuu ya mvutano katika makubaliano kati ya Iran na Marekani.

Chanzo cha picha, Getty Images/BBC

Baada ya wiki kadhaa za mazungumzo, Marekani na Iran zimefikia makubaliano ya awali, lakini tayari umakini umeelekezwa kwenye changamoto kubwa zinazoweza kuzuia kumalizika kwa vita.

Ingawa makubaliano hayo yalitarajiwa kusainiwa rasmi nchini Uswisi siku ya Ijumaa, yalitiwa saini mapema bila viongozi kuwepo ana kwa ana na Rais wa Marekani, Donald Trump, pamoja na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian.

Makubaliano hayo yanafungua njia ya kufikiwa kwa “makubaliano ya mwisho” ndani ya siku 60, huku kukiwa na uwezekano wa kuongeza muda iwapo pande zote mbili zitakubaliana.

Yanajumuisha ahadi ya kuanza mchakato wa kuondoa mzingiro wa majini wa Marekani, kurejesha usafirishaji wa meli kupitia Mlango bahari wa Hormuz, na kujadili kuondolewa kwa “aina zote za vikwazo” dhidi ya Iran.

Hati hiyo pia inapendekeza kuundwa kwa mfuko wa angalau dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi upya na maendeleo ya uchumi wa Iran. Aidha, Tehran imeahidi tena kutofuatilia utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Rais Trump ameonya kuwa makubaliano hayo ya awali “siyo ya mwisho” na amesema kwamba yakishindikana, Marekani inaweza “kuanza tena mashambulizi ya mabomu.”

Nchini Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, Spika wa Bunge la Ushauri la Kiislamu na mmoja wa wakuu wa majadiliano wa Jamhuri ya Kiislamu, aliiambia vyombo vya habari vya serikali kwamba kutokuwa na imani kwake kwa Marekani bado hakujabadilika.

Aliongeza kusema: “Adui ameelewa kwamba tunapozungumza kuhusu mazungumzo, upanga wetu pia uko tayari.”

Kwa mujibu wa wataalamu, mambo matatu yafuatayo ni miongoni mwa vitisho vikubwa zaidi vinavyoweza kuhatarisha mazungumzo hayo:

Mashambulizi ya Israel huko Lebanon

Inakadiriwa kuwa nyumba 50,000 nchini Lebanon ziliharibiwa au kubomolewa kabisa wakati wa vita.

Chanzo cha picha, Reuters

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 7

Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye alikuwa mmoja wa wapatanishi wakuu katika mazungumzo hayo, alisema alipokuwa akitangaza makubaliano ya awali kwamba pande hizo mbili zimetangaza “kusitishwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwa ni pamoja na Lebanon.”

Maandishi yaliyochapishwa ya makubaliano hayo pia yanaitaja waziwazi Lebanon na yanatoa dhamana ya “kulinda uadilifu wa eneo lake na mamlaka yake ya kujitawala.

Hii ina maana kwamba pande zilizohusika zinakubali kuheshimu mipaka ya Lebanon, kutokiuka ardhi yake, na kutambua haki yake ya kujitawala bila kuingiliwa na mataifa mengine.

Hata hivyo, Israel imeendelea na mashambulizi yake nchini Lebanon, hata baada ya Donald Trump kusema katika mkutano wa viongozi wa G7 nchini Ufaransa kwamba Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anapaswa kuonesha “uwajibikaji zaidi kuhusu Lebanon.”

Siku ya Jumatano, shirika rasmi la habari la Lebanon liliripoti kuwa ndege za kivita za Israel zililenga eneo la Nabatieh Foqa na kitongoji cha karibu cha Kafr Tibnit.

Aidha, maafisa wa Marekani wanasema kwamba ingawa Lebanon imejumuishwa katika mfumo wa usitishaji mapigano, kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka ardhi ya Lebanon si sharti la makubaliano hayo. Wanasema kuwa Israel itaendelea kuwa na haki ya kujilinda.

Lakini Iran imesisitiza kwamba kumalizika kwa vita nchini Lebanon ni “sehemu muhimu na isiyotenganishwa ya makubaliano ya kumaliza vita.”

Hezbollah, kundi la wanamgambo nchini Lebanon linaloungwa mkono na Iran, linaunga mkono msimamo huo. Ofisi ya mahusiano ya vyombo vya habari ya Hezbollah iliiambia Reuters kwamba Iran imeihakikishia kuwa katika awamu inayofuata ya mazungumzo itasisitiza kuondolewa kabisa kwa majeshi ya Israel kutoka Lebanon.

Israel nayo imeweka wazi kwamba haijioni kuwa imefungwa na makubaliano yoyote yatakayofikiwa kati ya Iran na Marekani. Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, amesema kuwa majeshi ya Israel yataendelea kubaki katika maeneo ya usalama nchini Lebanon “kwa muda usiojulikana,” na ameonya kwamba iwapo Iran itaishambulia Israel kwa sababu ya Lebanon, Israel itajibu “kwa nguvu.”

Netanyahu

Chanzo cha picha, Getty Images

H. A. Hellyer, mwanasayansi wa siasa katika taasisi ya Royal United Services (RUSI), anasema kuwa mji wa Tel Aviv umekuwa “kikwazo kikuu” kwa juhudi za kuleta amani.

“Ujasiri wa kijeshi wa Israel, iwe dhidi ya Iran au kupitia kuendelea kwa uharibifu nchini Lebanon, ndio tishio kubwa zaidi kwa maendeleo ya kidiplomasia,” amesema.

Bw. Hellyer anaongeza kuwa ikiwa Iran itajikuta katika mapambano ya moja kwa moja, mchakato huo unaweza kusambaratika kabla hata ya “mazungumzo ya kina kuhusu suala la nyuklia kuanza.”

Rais wa Lebanon, Joseph Aoun, amekaribisha makubaliano ya awali na kusema ana matumaini kwamba yatapelekea “hatua za vitendo zitakazomaliza mzunguko wa vurugu mara moja na kwa wote.”

Kwa Lebanon yenyewe, athari za vita zimekuwa mbaya sana. Zaidi ya watu 3,700 wameuawa, karibu watu milioni moja wamelazimika kuyahama makazi yao, na maeneo makubwa ya kusini mwa nchi yamekumbwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu na mali.

Hali hiyo imeacha changamoto kubwa za kibinadamu na kiuchumi, huku juhudi za ujenzi upya, kurejesha huduma za msingi, na kuwasaidia wakimbizi wa ndani zikihitaji rasilimali nyingi na msaada wa kimataifa.

Mpango wa Nuclear wa Iran

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Suala jingine linalozua mvutano katika mazungumzo hayo ni akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran, ingawa Donald Trump amesema kuwa hakuna haraka ya kuichukua.

Kwa mujibu wa International Atomic Energy Agency (IAEA), hadi mwaka jana Iran ilikuwa imekusanya takribani kilo 400 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 60. Kiwango kinachohitajika kutengeneza silaha ya nyuklia ni karibu asilimia 90.

Tehran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa matumizi ya amani pekee, na katika makubaliano haya ya awali imeahidi tena kwamba haitatafuta kutengeneza silaha za nyuklia.

Hata hivyo, masuala muhimu, yakiwemo hatima ya urani iliyokwisha kurutubishwa, yameahirishwa hadi makubaliano ya mwisho yatakayojadiliwa baadaye.

Pande zote mbili zimekubaliana kimsingi kuamua hatima ya akiba hiyo ya urani. Chaguo la chini kabisa linalotarajiwa ni “kupunguzwa kwa kiwango cha urutubishaji wa nyenzo hiyo ndani ya Iran chini ya usimamizi wa IAEA.”

Katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 yaliyotiwa saini wakati wa utawala wa Barack Obama, Tehran ilikubali kupunguza urutubishaji wa urani hadi asilimia 3.67. Baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano hayo mwaka 2018 wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, Iran ilipanua kwa kiasi kikubwa shughuli zake za nyuklia.

Darin Selnick, aliyekuwa naibu mkuu wa wafanyakazi wa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, aliiambia BBC kwamba ikiwa rais ataona Iran inarutubisha tena urani hadi viwango vya kutengeneza silaha za nyuklia, “huenda akaanzisha tena operesheni za kijeshi.”

Kwa mujibu wa mfumo wa awali wa makubaliano hayo, pande zote zinatarajiwa kudumisha hali ilivyo katika kipindi cha siku 60 za mazungumzo. Hii ina maana kwamba Iran haitapanua shughuli zake za nyuklia, na Marekani itajizuia kuweka vikwazo vipya au kuongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.

Mlango bahari wa Hormuz

Makubaliano hayo pia yanalenga kufungua tena mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafiri wa baharini ambayo imekuwa imefungwa kwa kiasi kikubwa tangu mwishoni mwa Februari. Kabla ya vita, takribani asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta na gesi duniani ulipitia katika njia hii muhimu.

Kwa mujibu wa makubaliano ya awali, njia hiyo ya maji itafunguliwa tena baada ya kutiwa saini rasmi kwa hati ya makubaliano, na inatarajiwa kurejea katika uwezo wake kamili wa kufanya kazi ndani ya siku 30 baada ya vikwazo vya kiufundi na kiusalama kuondolewa, ikiwemo kusafishwa kwa mabomu ya baharini na Iran.

Makubaliano hayo yanaeleza kwamba kwa kipindi cha awali cha siku 60, meli zitapita bila kulipa ushuru wowote katika njia hiyo “kwa pande zote mbili kati ya Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.”

Pia yanabainisha kuwa Iran itajadili na Oman pamoja na mataifa mengine ya Ghuba kuhusu namna ya kusimamia njia hiyo ya maji siku zijazo na kutoa huduma za baharini kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Kifungu hicho kinaacha wazi uwezekano wa kutozwa ada kwa meli zitakazopita katika mlango huo wa bahari hapo baadaye.

Tehran imewahi kuashiria kwamba inataka kuwa na nafasi kubwa zaidi katika usimamizi wa njia hiyo. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, amesema kuwa meli zinazopita katika mlango huo zitatozwa ada za huduma, ingawa bado haijawekwa wazi ada hizo zitakuwa za huduma gani hasa.

Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kutoza ushuru kwa meli kwa ajili ya kuvuka mlango huo pekee hakuruhusiwi, ingawa kutoza ada kwa huduma maalum kunaruhusiwa.

Hata hivyo, Marekani imeeleza kuwa ina imani kwamba njia hiyo ya maji itaendelea kuwa wazi na bila matatizo hata baada ya mazungumzo kukamilika.

Afisa mmoja wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran inaweza kujaribu kuimarisha ushawishi wake katika njia hiyo ya maji, lakini akaongeza kuwa mataifa ya Ghuba hayatakubali mfumo wowote utakaozuia upatikanaji wao wa njia hiyo bila ushuru.

Donald Trump amesema kuwa Iran itatumia “busara” na haitatoza ushuru, kwa kuwa hatua kama hiyo inaweza kusababisha kurejea kwa mvutano wa kijeshi. Marekani pia inaamini kwamba mataifa ya Ghuba “hayatakubali kamwe” mfumo utakaohusisha ushuru hapo baadaye.

Hata hivyo, bado kuna maswali ya kiutendaji yanayohitaji majibu.

Mark Montgomery, admirali mstaafu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, aliiambia BBC kwamba kusafisha mabomu ya baharini kunaweza kuchukua “wiki kadhaa hadi miezi kadhaa.”

Makampuni ya usafirishaji wa meli huenda yakachukua tahadhari kubwa hadi yatakapokuwa na uhakika kwamba usitishaji mapigano unatekelezwa kikamilifu.

Martin Kelly wa kampuni ya usimamizi wa migogoro ya AOS Risk Group aliiambia BBC kwamba:

“Kwa kuzingatia hali ya sasa, kupita katika Mlango wa Hormuz kunahitaji ujasiri wa hali ya juu kutoka kwa nahodha wa meli.”

Hata hivyo, H. A. Hellyer anaonya kwamba makubaliano ya kumaliza vita bado ni “hati ya makubaliano ya awali mfumo wa mazungumzo, si suluhisho lenyewe.”

“Kazi ngumu bado haijaanza hata kidogo.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *