Dar es Salaam. Kisukari na shinikizo la damu ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yenye uhusiano mkubwa, na mara nyingi huweza kumpata mtu mmoja kwa wakati mmoja.

Hali hiyo huongeza hatari ya kupata matatizo makubwa ya kiafya kama magonjwa ya moyo, figo, macho pamoja na kiharusi.

Shinikizo la damu hutokea pale damu inapopita kwenye mishipa kwa nguvu kubwa kuliko kawaida. Kwa upande mwingine, kisukari hutokea pale mwili unaposhindwa kuzalisha au kutumia insulin vizuri, hivyo kusababisha kiwango cha sukari kwenye damu kupanda. Ingawa magonjwa haya ni tofauti, yanaweza kuathiriana kwa kiasi kikubwa ndani ya mwili.

Wataalamu wanaeleza kuwa watu wenye kisukari wako kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata shinikizo la damu.

Sukari ikiwa juu kwa muda mrefu inaweza kuharibu mishipa ya damu na kufanya mishipa hiyo kuwa migumu au myembamba. Hali hii hufanya moyo kufanya kazi kwa nguvu zaidi ili kusukuma damu mwilini, na matokeo yake ni kuongezeka kwa shinikizo la damu.

Wagojwa wa kisukari aina ya pili pia huwa na uzito mkubwa au mafuta mengi mwilini, jambo linaloongeza hatari ya kupata shinikizo la damu. Kutofanya mazoezi, ulaji wa chumvi nyingi, mafuta mengi pamoja na msongo wa mawazo,  ni baadhi ya mambo yanayochangia magonjwa haya mawili.

Dalili za shinikizo la damu wakati mwingine zinaweza kutoonekana mapema, baadhi ya watu wanaweza kupata maumivu ya kichwa, uchovu, mapigo ya moyo kwenda kasi au kizunguzungu. Kwa wagonjwa wa kisukari, dalili hizi zinahitaji uangalizi wa haraka kwa sababu huongeza hatari ya matatizo ya moyo na mishipa ya damu.

Wataalamu wanasisitiza kuwa kudhibiti sukari na shinikizo la damu kwa pamoja ni muhimu. Mgonjwa mwenye kisukari anashauriwa kupima shinikizo la damu mara kwa mara ili kugundua tatizo mapema. Kufuata matibabu kwa usahihi kunaweza kusaidia kupunguza madhara ya magonjwa hayo.

Ulaji unaofaa na ufanyaji wa mazoezi ya mwili vina nafasi kubwa katika kudhibiti kisukari na shinikizo la damu. Wataalamu wanashauri kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na mafuta mengi. Badala yake, watu wanapaswa kula mboga za majani, matunda kwa kiasi, nafaka zisizokobolewa na vyakula vyenye nyuzinyuzi. Vyakula hivi husaidia kudhibiti kiwango cha sukari pamoja na afya ya moyo.

Pia wataalamu wanashauri watu kuacha kuvuta sigara na kupunguza matumizi ya pombe kwa sababu vinaongeza hatari ya kuharibika kwa mishipa ya damu.  

Wataalamu wanaamini kuwa kwa elimu sahihi, lishe bora, mazoezi pamoja na matumizi sahihi ya dawa, wagonjwa wanaweza kudhibiti hali zao na kuendelea kuishi maisha yenye afya na matumaini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *