
Leo ni Ijumaa 04 Mfunguo Nne Muharram 1448 Hijria mwafaka na 19 Juni 2026.
Siku kama ya leo, miaka 1387 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa utawala wa Yazid bin Muawiya katika mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo.
Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba, atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo.
Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad alifunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa na akawahonga kwa fedha wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala; tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (saw). ***
Katika siku kama ya leo miaka 964 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq.
Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi.
Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua Aya 226 za Qur’ani Tukufu. ***
Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1867, Maximilian mwana wa mfalme wa Austria ambaye aliikalia kwa mabavu Mexico, alinyongwa na wapigania uhuru wa nchi hiyo.
Baada ya Benito Juarez kupata urais wa Mexico mwaka 1855, aliwang’anyya mamlaka wazungu na kupunguza nguvu za Kanisa nchini humo. Hatua hiyo iliwakasirisha mno wazungu na wakoloni wa Ulaya waliokuwa wakiongozwa na Ufaransa ambao walituma jeshi nchini Mexico kwa shabaha ya kulihami Kanisa pamoja na wawekezaji wazungu. Hata hivyo, Juarez aliendeleza mapambano dhidi ya majeshi ya Ufaransa na washirika wake, na baada ya kuwashinda na kumnonga mfalme wa kutwishwa, akashika tena urais wa Mexico. ***
Katika siku kama ya leo miaka 149 iliyopita inayosadifiana na tarehe 19 Juni 1877, Enrico Forlanini mhandisi wa Kiitalia alifanikiwa kufanya majaribio ya kwanza ya kurusha angani helikopta katika mji wa bandari wa Alexandria nchini Misri.
Helikopta hiyo iliboreshwa zaidi na mtaalamu wa Kipolandi, na ubunifu huo ukaandikwa kwa jina lake. ***
Siku kama ya leo miaka 65 iliyopita nchi ya Kuwait iliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi ilijipatia uhuru baada ya kufutwa makubaliano ya ukoloni ya mwaka 1899 kati ya Uingereza na Kuwait.
Katikati ya karne 18, iliasisiwa silsila ya al Swabah nchini humo na ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19, Kuwait iliomba uungaji mkono wa Uingereza kwa shabaha ya kukabiliana na dola la Othmaniya. Mwaka 1899, Uingereza na Kuwait zilifanya makubaliano ambayo yaliiweka Kuwait chini ya ukoloni wa Uingereza. ***
Katika sku kama ya leo miaka 49 iliyopita, sawa na tarehe 29 Khordad 1356 Hijria Shamsia, alifariki dunia Dakta Ali Shariati mwandishi na msomi wa zama hizi wa Kiirani mjini London, Uingereza.
Dakta Shariati alipata elimu yake ya juu katika taaluma ya fasihi sambamba na kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya utawala wa mfalme hapa nchini. Dakta Shariati alikuwa bega kwa bega na Shahidi Mutahhari na Shahidi Bahonar, katika kuanzisha Husseiniya ya Ershad mjini Tehran kwa shabaha ya kukomaza fikra za tabaka la vijana.
Msomi huyo wa Kiirani ameandika zaidi ya vitabu 200 na miongoni mwao ni ‘Uislamu na Mwanadamu’, ‘Historia ya Ustaarabu’ na ‘Fatima ni Fatima’. ***