
UFARANSA: Rais wa Marekani na Rais wa Iran wameripotiwa kusaini makubaliano ya awali ya amani yanayolenga kumaliza vita, makubaliano yanayoanza mara moja.
Makubaliano hayo yanajumuisha kufunguliwa tena kwa Mkondo wa Bahari wa Hormuz, mpango wa takribani Dola bilioni 300 kwa ajili ya ujenzi upya wa Iran na Marekani kuondoa aina zote za vikwazo dhidi ya Iran.
Hata hivyo, suala la mpango wa nyuklia wa Iran, ambalo ndilo lililotajwa kama sababu kuu ya Marekani kuingia kwenye mzozo huo, bado linajadiliwa katika kipindi cha siku 60.
Rais wa Marekani Donald Trump, aliyesaini makubaliano hayo nchini Ufaransa wakati wa mkutano wa G7, ametetea mpango huo akisema utazuia “janga la kiuchumi.” Hata hivyo ameonya kuwa Marekani “itailipua Iran” iwapo makubaliano ya mwisho hayatofanyiwa kazi.
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian pia alisaini hati hiyo Jumatano, Serikali ya Tehran imethibitisha.
Spika wa Bunge la Iran na mmoja wa washauri wakuu wa mazungumzo, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema kupitia vyombo vya habari vya serikali kuwa bado ana mashaka na Marekani.
Amesema: “Adui asipoelewa lugha ya mazungumzo ya busara, tutarejea tena kwenye lugha ya nguvu.”
Marekani na Israel wameripotiwa kuanzisha vita dhidi ya Iran Februari 28 wakimuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei na viongozi wakuu wa kijeshi siku ya kwanza.
Tangu wakati huo, mzozo huo umeendelea na kusababisha kupanda kwa bei ya nishati na kuongeza shinikizo la mfumuko wa bei, huku Iran ikifunga kwa kiasi kikubwa mkondo wa Hormuz, njia muhimu ya biashara inayopita takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia ya dunia.
Trump aliliambia vyombo vya habari mjini Ufaransa katika eneo la Evian-les-Bains, ambako mkutano wa G7 ulifanyika, kuwa mpango huo utaepusha “mdororo wa kiuchumi duniani.”
“Sikutaka kuona janga la kiuchumi,” alisema Trump. “Ukiendelea na hali hii, hilo lingeweza kutokea.”
“Kila mara tulipozungumzia amani, soko la hisa lilipanda kama roketi,” aliongeza.
“Kila tuliposema jambo hasi, kama kwamba hatuwezi kufikia makubaliano, lilishuka sana.”