
“Katika kipindi ambacho kilipaswa kuongozwa na kujizuia na kulinda maisha, kwa wastani mtoto mmoja amekuwa akiuawa kila siku kwa zaidi ya miezi minane,” amesema msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), James Elder. “Hiyo ni takwimu ya kusikitisha na isiyoelezeka.”
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo kwa njia ya video kutoka Amman, nguli huyo wa masuala ya misaada wa UNICEF amebainisha kuwa watoto hao “hawakuuawa katika eneo la vita,” bali wameuawa wakiwa majumbani mwao, shuleni, wakicheza mpira wa miguu au wakivua samaki. “Walipigwa risasi, walishambuliwa kwa mabomu, walilengwa na ndege zisizo na rubani aina ya quadcopter,” ameendelea kusema Bwana. Elder, akirejelea operesheni za jeshi la Israel.
Watoto ni waathirika wakubwa
Kwa mujibu wake vifo hivyo vya watoto ni sehemu ya karibu Wapalestina 1,000 waliouawa Gaza na zaidi ya 3,100 waliojeruhiwa tangu usitishaji wa mapigano ulipoanza, kulingana na mamlaka za afya za eneo hilo.
“Ukipiga chafya karibu na Mstari wa rangi ya Machungwa (Orange Line), unaweza kabisa kupigwa risasi,” amesisitiza Bwana. Elder, akirejelea kusogezwa mbele mara kwa mara kwa kile Israel inachokiita “Mstari wa Njano” (Yellow Line) na “Mstari wa rangi ya Machungwa” (Orange Line). Amesema kutokuwa na uhakika kuhusu mipaka hiyo inayobadilika na “ukosefu kamili wa uwajibikaji ndizo sababu za idadi kubwa ya mauaji, huku vikosi vya Israel vikihusika na idadi kubwa sana ya visa hivyo zaidi ya asilimia 90”.
Umoja wa Mataifa na washirika wake wamekuwa wakionya mara kwa mara kwamba mzozo huo umeleta athari kubwa za kibinadamu tangu vita vilipoanza mwezi Oktoba 2023, kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyoongozwa na Hamas dhidi ya Israel.
Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), hakuna hospitali hata moja inayofanya kazi kikamilifu Gaza, huku UNICEF ikionya kwamba upatikanaji wa maji bado ni jambo lisilo na uhakika kwa watoto milioni 1.1 kila siku.
“Ninazungumza na akina mama ambao watoto wao wanalia kwa maumivu kwa sababu hawana maji safi ya kuosha miili yao. Hebu fikiria mzazi asiyeweza kutatua hali hiyo usiku baada ya usiku,” amesema Bwana. Elder. “Kiwango cha mateso ya kibinadamu kinachowapata watoto wa Kipalestina huko Gaza, na kinachoruhusiwa kuendelea na wengine, ni vigumu sana kukilinganisha na chochote tulichoshuhudia katika maisha yetu.”
Zaidi ya watu milioni 1.9 wamefurushwa makwao
Kwa sasa, karibu watu milioni 1.9 wamefurushwa kutoka makazi yao Gaza, wengi wao mara kadhaa, huku zaidi ya watu milioni 1.2 wakipoteza nyumba zao.
Katika taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya jana Alhamisi, mkuu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, aliripoti kwamba kiwango cha kukataliwa kwa misafara ya misaada kuingia Gaza na Israel kimeshuka kutoka asilimia 31 kabla ya usitishaji wa mapigano hadi asilimia 11 kwa sasa.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Wapalestina wa Gaza bado “wananyimwa mahitaji ya msingi ambayo kila mmoja wenu angehitaji kwa familia yake mwenyewe, usalama, makazi, maji safi, huduma za afya na elimu.”
Bwana. Elder ameunga mkono tathmini hiyo ya kusikitisha, akieleza kwamba ingawa kiasi fulani cha mafuta kinafika kwa jenereta ambazo bado zinafanya kazi, mamlaka za Israel haziruhusu vipuri kuingia Gaza ili kutengeneza mashine zilizoharibika, wala mafuta ya kulainisha injini ili ziendelee kufanya kazi vizuri. “Hii ndiyo mazingira ambayo wenzangu wanafanyia kazi, wakijitahidi kuwaweka watoto hai bila hata chembe ya hadhi ya kibinadamu,” amesema.
Matatizo mengine makubwa pia yanaendelea bila kutatuliwa kutokana na ucheleweshaji na kukataliwa kwa misaada kuingia Gaza, hususan kiasi kikubwa cha taka ngumu zinazozidi kuongezeka, amesema Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
“Sote tumesikia kuhusu panya, wadudu na matatizo mengine yanayotokana na hali hiyo. Kuna fursa na uwezekano wa kuondoa taka hizo zote, lakini hatupati ruhusa ya kufikia maeneo hayo,” amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.
Mauaji zaidi nchini Lebanon
Msemaji huyo wa OCHA pia amelaani kuendelea kwa mashambulizi nchini Lebanon usiku kucha, huku taarifa zikionesha kwamba takriban watu 18 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel kusini mwa nchi hiyo yaliyolenga wapiganaji wa Hezbollah.
“Tunashuhudia taarufa hizo za usiku kucha kwa wasiwasi mkubwa sana… mapigano zaidi hayatamsaidia yeyote,” amesema Bwana. Laerke, akibainisha kiwango kikubwa cha mahitaji ya kibinadamu nchini Lebanon, hasa katika maeneo ya kusini.
“Ni rahisi sana na haraka kuumiza watu na kusababisha uharibifu kuliko kurejesha maisha yao, kuwasaidia kurudi nyumbani, kuwapatia chakula na mahitaji mengine. Siku moja au mbili tu za vita vya aina hii zinaweza kuhitaji miezi, au hata miaka, ya shughuli za kibinadamu kurekebisha madhara yake.”
Kulingana na UNICEF, zaidi ya watoto 770,000 wanakabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo kutokana na kuendelea kushuhudia vurugu, kupoteza wapendwa wao na kulazimika kuhama makazi mara kwa mara.