ZAPOPAN, MEXICO: Wenyeji wa Kombe la Dunia Mexico imekuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo baada ya kuifunga Korea Kusini bao 1-0, katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa kwenye Uwanja Akron karibu na Jiji la Guadalajara, Mexico.
Katika mechi hiyo ilianza kwa timu zote kushambuliana kwa zamu na kwa nidhamu ya hali ya juu ya kujilinda licha ya Korea Kusini kutopiga shuti lolote lililolenga lango kipindi cha kwanza dhidi ya wenyeji wao, Mexico.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu zote japo dakika ya 50, Mexico ilipata bao la kwanza lililofungwa na nyota wa timu hiyo, Luis Romo baada ya makosa yaliyofanywa na kipa wa Korea Kusini, Kim Seung-Gyu na kuwatanguliza wenyeji kifua mbele.
Bao hilo la Romo linamfanya nyota huyo kuandika rekodi mbili, ambapo ya kwanza ni ya kuanza mechi ya kwanza ya Kombe la Dunia, huku ya pili ni ya kufunga pia bao lake la kwanza katika michuano hiyo ambayo Mexico ndio wenyeji kwa kushirikiana na Marekani na Canada.
Licha ya jitihada za Korea Kusini za kutaka kusawazisha bao hilo, ila Mexico ilionyesha uimara mzuri wa kuzuia mashambulizi ya wapinzani wao na kuondoka na ushindi muhimu ikiwa ni wa pili pia kwa kikosi hicho.
Mechi ya kwanza timu hizo zilianza Michuano ya Kombe la Dunia kwa ushindi, baada ya wenyeji, Mexico kuichapa Afrika ya Kusini mabao 2-0, huku kwa upande wa kikosi cha Korea Kusini kikianza pia vizuri kwa kuifunga Jamhuri ya Czech mabao 2-1.
Ushindi huo unaifanya Mexico kufuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo ya Kombe la Dunia, baada ya kuongoza kundi A na pointi sita, nyuma ya Korea Kusini yenye pointi tatu, huku Jamhuri ya Czech na Afrika ya Kusini zikiwa na pointi moja kufuatia kila timu kucheza mechi mbili.
Mexico ilishiriki Kombe la Dunia la mara ya kwanza la FIFA mwaka 1930, lililofanyika Uruguay na wenyeji kutwaa ubingwa, huku ikiandaa michuano hiyo kwa mara ya tatu katika historia yake, baada ya kufanya hivyo kuanzia mwaka 1970, 1986 na 2026.
Katika miaka yote iliyoandaa michuano hiyo ya Kombe la Dunia, Mexico ilifika hadi hatua ya robo fainali, ikianza mwaka 1970 na 1986, huku mafanikio mengine ni kuishia 16, bora mara saba kuanzia 1994, 1998, 2002, 2006, 2010, 2014 na 2018.
Kwa upande wa Korea Kusini, ilianza kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1954, ikiwa na timu za Hungary na Ujerumani Magharibi, ambapo ilipoteza mechi zote mbili kwa kufungwa jumla ya mabao 16, huku ikishindwa kufunga pia bao.
Mafanikio makubwa kwa timu hiyo ni kufika hatua ya nusu fainali ya mwaka 2002, ilipoandaa michuano ya Kombe la Dunia kwa kushirikiana na Japan, ikishangaza vigogo wa soka duniani baada ya kuzifunga Italia na Hispania na kuandika rekodi mpya.