VANCOUVER, CANADA. Wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia Canada imepata ushindi wa kwanza mnono baada ya kuichapa Qatar mabao 6-0, huku nyota wa timu hiyo, Jonathan David akifunga Hat Trick ya pili ya Kombe la Dunia, baada ya Lionel Messi kuanza kuifungia Argentina.
Katika mechi hiyo ya kundi B iliyopigwa kwenye Uwanja wa BC Place, Vancouver, wenyeji Canada ilitumia vyema makosa ya Qatar iliyoshuhudiwa wachezaji wawili wa kikosi hicho, Homam Al Amin na Assim Omer Madibo kuonyeshwa kadi nyekundu ya dakika ya 33 na 53.
Mbali na Jonathan David kufunga mabao matatu (Hat-Trick) kuanzia dakika ya 29, 45+3 na 90+2, mabao mengine ya Canada yamefungwa na Cyle Larin dakika ya 16, Nathan Saliba dakika ya 64 na Mohammad Al Mannai dakika ya 75.
Hat trick hiyo ya Jonathan David ni ya pili katika Kombe la Dunia la mwaka 2026, baada ya Lionel Messi wa Argentina kufunga katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0, dhidi ya Algeria Juni 17, 2026.
Canada ambayo ni wenyeji wa Kombe la Dunia kwa kushirikiana na Marekani na Mexico, ilianza mechi ya kwanza ya hatua ya kundi B kwa kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Bosnia and Herzegovina.
Matokeo hayo yanaifanya Canada kuongoza kundi B na pointi nne ambazo ni sawa na za Uswisi, huku Bosnia na Qatar zikiwa na pointi moja kila mmoja.
Canada ambao ni wenyeji wa Kombe la Dunia la 2026, kwa kushirikiana na Marekani na Mexico, ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1986, ikiwa kundi moja na Ufaransa, Hungary na Soviet Union na kuchapwa mechi zote kisha kuishia hatua ya makundi.
Baada ya kutolewa hatua ya makundi mwaka 1986, huku ikiwa haijafunga bao lolote, timu hiyo ilichukua miaka 36, kufuzu tena Kombe la Dunia la 2022 lililofanyika Qatar na kuburuza mkiani kundi F, lililokuwa na Morocco, Croatia na Ubelgiji.
Alphonso Davies ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga bao la kwanza la Canada katika historia ya Kombe la Dunia, ambapo alifunga kwenye fainali za Qatar hatua ya makundi, wakati timu hiyo ilipochapwa na Croatia mabao 4-1, Novemba 27, 2022.
Kiujumla hii ni mara ya tatu kwa Canada kushiriki Kombe la Dunia ikianza kwa mara ya kwanza mwaka 1986, kisha ikarudia tena 2022 baada ya miaka 36 na 2026, ikiwa mwenyeji na mara zote ilizoshiriki haijawahi kufika hatua yoyote ya mtoano.
Kwa upande wa Qatar haina historia ya kuvutia katika Kombe la Dunia ikilinganishwa na mataifa mengine, ambapo timu hiyo ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2022, ikiwa wenyeji wa fainali hizo zilizofanyika kuanzia Novemba hadi Desemba 2022.
Katika fainali hizo za mwaka 2022, zilizofanyika eneo la Mashariki ya Kati na nchi ya Qatar ikiandaa mashindano hayo, kikosi hicho kilipangwa kundi A lenye timu za Ecuador, Senegal na Uholanzi ambapo ilipoteza zote na kuburuza mkiani.
Licha ya kuchapwa mechi zote tatu, ila mchezaji wa Qatar, Mohammed Muntari aliandika historia ya kufunga bao la kwanza kwa kikosi hicho katika Michuano ya Kombe la Dunia, wakati timu hiyo ilipochapwa na Senegal mabao 3-1, Novemba 25, 2022.
Qatar ilifuzu Kombe la Dunia la 2026 kupitia Kundi A la raundi ya nne ya mchujo wa Asia (AFC Fourth Round), lililokuwa na timu za Falme za Kiarabu (UAE) na Oman na kumaliza kileleni ikiwa na pointi zake nne na kufuzu rasmi Oktoba 14, 2025.
Timu hiyo ilitoka suluhu ya (0-0), dhidi ya Oman na kuifunga Falme za Kiarabu (UAE) mabao 2-1 na kukata rasmi tiketi ya kucheza Kombe la Dunia la 2026 kwa mara ya kwanza kupitia mchujo, baada ya mwaka 2022 kushiriki pia japo ikiwa mwenyeji.