Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto katika Maeneo ya Migogoro ya Silaha Vanessa Frazier, amezungumzia ripoti hiyo, uso wake ukiwa umejaa huzuni alipokuwa akizungumza mbele ya waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Bi. Vanessa anasema ripoti hiyo imebaini kuwa mwaka 2025 ulikuwa miongoni mwa miaka mibaya zaidi kwa watoto wanaoishi katika maeneo ya vita na migogoro.

“Matokeo ya ripoti ya leo ni ya kutisha sana. Yanaonesha uhalisia wa kusikitisha unaowakabili watoto katika maeneo ya machafuko duniani kote, hali inayopaswa kutugusa sisi sote. Mwaka 2025, Umoja wa Mataifa ulithibitisha ukiukwaji mkubwa, matukio yaliyoripotiwa ni 38,558 na ambayo yamewaathiri watoto 24,174.”

© UNICEF/Mohammed Jamal Watoto waliokimbia ghasia huko El Fasher wanapokea vifaa vya shule huko Tawila.

Katika kipindi cha miaka 30 ya ufuatiliaji wa Umoja wa Mataifa, mwaka 2025 umeandika rekodi ya kusikitisha ya ukiukwaji mkubwa zaidi dhidi ya watoto.

“Watoto 14,224 walithibitishwa kuuawa au kujeruhiwa na huu ndio ulikuwa ukiukwaji ulioenea zaidi. Idadi ya watoto waliouawa iliongezeka kwa asilimia 35 ikilinganishwa na 2024.”

Pengine ukubwa wa idadi hii unaweza kueleweka zaidi kwa mfano wa Kombe la Dunia.

Kombe la Dunia 2026 linashirikisha timu 48 pekee, zenye jumla ya wachezaji 1,248. Sasa fikiria timu zote za Kombe la Dunia, halafu zidisha mara 11. Huo ndio ukubwa wa idadi ya watoto 14,224 waliouawa au kujeruhiwa mwaka jana.

Au fikiria mashabiki waliokaa kwenye uwanja wa fainali wa Kombe la Dunia wa MetLife. Ukiondoa karibu sehemu moja kati ya sita ya uwanja mzima, hiyo ndiyo idadi ya watoto waliouawa au kujeruhiwa mwaka jana.

Ripoti hiyo pia imeonesha jambo lingine la kusikitisha: katika baadhi ya maeneo ya migogoro, si makundi ya silaha pekee yanayotuhumiwa, bali pia vikosi vya serikali.

Ukipata wasaaa tembelea wavuti wetu au mtandao wa X kusoma habari hii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *