Video iliyoandaliwa na UN Women inaanza kwa kumwonesha Rahma Ali Salum, mtendaji wa dawati la jinsia katika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, akieleza hatua za kwanza ambazo manusura wa ukatili wanapaswa kuchukua mara wanapopata madhara.

“Mtu yeyote aliyefanyiwa kitendo cha ukatili, hatua ya kwanza ni kuripoti mapema kabla hajapata mawazo mengine tofauti. Aidha afike kwa sheha au kituo cha polisi moja kwa moja kwenye kitengo cha dawati la jinsia.”

Rahma anasema kuripoti mapema huwasaidia manusura kupata huduma muhimu kwa wakati, ikiwemo matibabu ya haraka na kinga dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza baada ya tukio.

“Atapatiwa matibabu stahiki kwa wakati. Ikiwa amefanyiwa ukatili wa kingono au kubakwa, akiwahi kufika kwenye kituo cha huduma za afya atapokea huduma za dharura, ikiwemo kinga dhidi ya ujauzito usiokusudiwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama virusi vya ukimwi. Aidha, atapatiwa ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia ili kumwezesha kurejea katika hali yake ya kawaida na kuendelea na maisha yake kwa matumaini na nguvu mpya.”

Mbali na huduma za afya na ushauri nasaha, mradi huu pia unaimarisha uwezo wa watoa msaada wa kisheria ili kuhakikisha kesi za ukatili wa kijinsia zinashughulikiwa kwa ufanisi zaidi.

“Anapowahi kutoa taarifa, ushahidi muhimu hukusanywa kwa wakati na hatua za haraka huchukuliwa kumkamata mtuhumiwa. Hali hii huimarisha msingi wa kesi mahakamani na kuongeza uwezekano wa haki kutendeka. Kwa njia hiyo, manusura hupata faraja na kuridhika kwamba hatua stahiki zimechukuliwa dhidi ya aliyemdhuru na kwamba haki yake imetendeka.”

Mradi huu unaonesha kuwa taarifa sahihi, huduma za haraka na mifumo imara ya haki vinaweza kuwasaidia manusura kupata ulinzi, haki na matumaini mapya, huku jamii ikisogea karibu zaidi na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *