
Katika ujumbe wake kuelekea siku hiyo muhimu, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Barham Ahmed Salih, ametoa pongezi kwa ujasiri na azma ya wakimbizi duniani kote, akisisitiza kwamba ingawa mtu anaweza kuwa mkimbizi kwa kipindi fulani, hali hiyo haipaswi kufafanua maisha yake yote. Amebainisha kuwa wakimbizi huchangia kwa kiasi kikubwa katika jamii zinazowapokea, wakifanya kazi kama wafanyakazi, wanafunzi, wafanyabiashara, wasanii na viongozi.
Kutoka ukimbizini hadi kuwa Rais
“Wakimbizi wamelazimika kuyaacha makazi yao, lakini hawapaswi kamwe kulazimishwa kuacha matumaini yao,” anasema Salih ambaye yeye mwenyewe aliwahi kuishi ukimbizi na baadaye akaja kuwa Rais wa Iraq mwaka 2018–2022. Amesisitiza kuwa msaada wa kibinadamu unaendelea kuwa muhimu katika kuokoa maisha, lakini akaonya kwamba msaada huo pekee hauwezi kuwa suluhisho la muda mrefu kwa mamilioni ya watu wanaotumia miaka, na wakati mwingine miongo kadhaa, wakisubiri fursa za kujenga upya mustakabali wao.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Salih kupitia ujumbe wake huo ametangaza lengo la kupunguza kwa nusu ndani ya miaka kumi ijayo idadi ya wakimbizi wanaoishi katika ukimbizi wa muda mrefu na wanaotegemea misaada ya kibinadamu. Amesema kufikiwa kwa lengo hilo, hasa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati ambazo zinahifadhi idadi kubwa ya wakimbizi duniani, kutasaidia kuhamisha juhudi za kimataifa kutoka katika kusimamia ukimbizi hadi kutafuta suluhisho la kudumu.
Katibu Mkuu
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres kupitia ujumbe wake kwa ajili ya kesho anatoa wito kama huo wa kuongezwa kwa msaada kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, ikiwa ni pamoja na kuheshimu sheria za kimataifa za wakimbizi, kulinda haki ya kuomba hifadhi, kuunda fursa za kujitegemea na kuongeza juhudi za kuleta amani. Katibu Mkuu pia anapongeza ukarimu wa nchi zinazoendelea ambazo zinahifadhi karibu robo tatu ya wakimbizi wote duniani, akihimiza dunia kushirikiana kulinda haki za watu waliolazimika kukimbia makazi yao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Mchezaji wa kombe la dunia mwenye ‘asili ya ukimbizi’
Hayo yanayosemwa na viongozi hao ni dhahiri kabisa kwamba wakimbizi hawapaswi kamwe kuwekwa katika mazingira ya kulazimishwa kuacha matumaini yao, Mfano mmoja wa wazi kuwa wakimbizi wakipewa nafasi wanaweza kuwa na mchango chanya kwa jamii za wenyeji na ulimwengu ni huu wa Toni Rüdiger, anaeleza wazazi wake walikimbia vita Sierra Leone wakapokelewa Ujerumani. Hivi sasa sio tu yuko na kikosi cha Ujerumani katika kombe la Dunia, bali pia ni msaidizi wa Kapteni wa timu na hajaisahau asili yake kwani ameanzisha Wakfu kusaidia watoto wa Sierra Leone kupata elimu, michezo na huduma za afya.