IRINGA: KATIBU wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Maoinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewataka wazazi kushirikiana na walimu katika malezi na makuzi ya watoto ili kujenga kizazi chenye maadili mema na uwezo wa kuliletea taifa maendeleo.

Kihongozi ametoa mwito huo leo Juni 20,2026 alipokagua Shule ya Msingi Nduli mkoani Iringa, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi katika mkoa huo.

Awali Kihongosi amewapongeza walimu kwa kazi wanayoifanya ya kuwafundisha na kuwalea wanafunzi, huku akisisitiza kuwa mafanikio ya watoto yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu.

“Walimu tunawatia moyo kama chama, tuendelee kuchapa kazi. Kazi ya walimu ni wito, kufundisha watoto wetu maarifa mazuri, elimu na kesho kutwa wawe wakombozi katika kata hii, wilaya yetu, mkoa pamoja na taifa kwa ujumla,”amesema Kihongosi.

Aliwataka wazazi kutowadekeza watoto na badala yake kuwajengea misingi bora ya maadili kwa kushirikiana na walimu wanaowafundisha shuleni.

“Wazazi na walimu, leeni watoto wenu, msiwadekeze watoto, wafundisheni katika misingi mema kwa sababu baadhi ya wazazi mwanafunzi anapohadhibiwa mnakasirika,”amesema Kihongosi.

Kihongosi amesisitiza kuwa nidhamu ni sehemu muhimu ya malezi ya mtoto na kwamba wazazi wanapaswa kuwaunga mkono walimu katika juhudi za kuwajenga watoto kuwa raia wema.

“Kwa hiyo wazazi tushirikiane na walimu kuhakikisha watoto wanakuwa na maadili mazuri ili tuwe na kizazi bora,” amesisitiza.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi, Isaya Lalika amesema mradi huo ulianza kutekelezwa Septemba 9,2026 na kukamilika Juni 9,2026 ukigharimu jumla ya Sh milioni 529.5 kwa ujenzi wa miundombinu yote iliyokusudiwa.

Lalika alisema lengo la mradi huo ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kupunguza msongamano wa wanafunzi, akibainisha kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wanafunzi wapatao 820.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *