
Huku utawala katili wa Israel ukiendeleza jinai Lebanon, mashirika ya misaada ya kibinadamu yametoa tahadhari mpya kuhusu Gaza, ambapo watoto 265 wa Kipalestina wameuawa katika mashambulizi ya Israel tangu usitishaji wa mapigano ulipotangazwa mwezi Oktoba 2025.
Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), James Elder, amesema katika kipindi ambacho kilipaswa kuongozwa na kujizuia na kulinda maisha, kwa wastani mtoto mmoja amekuwa akiuawa kila siku kwa zaidi ya miezi minane.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi Ijumaa kwa njia ya video kutoka Amman, Jordan nguli huyo wa masuala ya misaada wa UNICEF amebainisha kuwa watoto hao “hawakuuawa katika eneo la vita,” bali wameuawa wakiwa majumbani mwao, shuleni, wakicheza mpira wa miguu au wakivua samaki. “Walipigwa risasi, walishambuliwa kwa mabomu, walilengwa na ndege zisizo na rubani aina ya quadcopter,” ameendelea kusema Bwana Elder, akiashiria operesheni za jeshi la Israel.
Kwa mujibu wake vifo hivyo vya watoto ni sehemu ya karibu Wapalestina 1,000 waliouawa Gaza na zaidi ya 3,100 waliojeruhiwa tangu usitishaji wa mapigano ulipoanza, kulingana na mamlaka za afya za eneo hilo. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka 2023 kabla ya usitishwaji vita Oktoba mwaka jana. Katika kipindi hicho cha mauaji ya kimbari, Israel iliwaua Wapalestina wasipungua 73,000, wengi wakiwa ni wanawake na Watoto. Waziri Mkuu wa utawala katili wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa vita Yoav Gallan wanasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kutokana na jinai walizotenda huko Gaza. Nchi kadhaa zimetangaza kuwa tayari kumakamat Netanyahu na kumkabidhi kwa mahakama hiyo ya kimataifa iwapo atakanyaga ardhi zao.
Majaji wa ICC walitoa kibali cha kukamatwa Netanyahu na Gallant Novemba mwaka 2024. Aidha Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) imeitaka Israel isitishe sera za mauaji ya kimbari huko Gaza. Watawala wa Israel wamepuuza taasisi hizo za kimataifa na wanaendeleza jinai zao dhidi ya Wapalestina.