Kati ya timu za taifa 48 zinazoshiriki fainali za Kombe la Dunia 2026, ni Curaçao pekee ambayo dawati lake la matibabu liko chini ya mwanamama Dk Suzanne Huurman.
Dk Huurman amekuwa habari ya mjini kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026 kwa kuwa daktari mkuu mwanamke pekee anayeongoza benchi la matibabu.
Katika michuano hii inayotimua vumbi katika nchi za Marekani, Canada, na Mexico, Dk Huurman ndiye mwanamke wa kipekee aliyeaminiwa kati ya timu zote 48 zinazochuana, huku timu nyingine 47 zilizosalia zikitawaliwa na madaktari wakuu wa kiume.
Hatua hii inamfanya kuingia rasmi kwenye vitabu vya historia vya FIFA kama mwanamke wa tatu pekee kuwahi kushika wadhifa huo wa juu tangu kuanzishwa kwa Kombe la Dunia mwaka 1930.
Dk Suzanne Huurman (wa pili kutoka kulia), akiwa pamoja na madaktari wengine wa timu y a taifa ya Curacao. Picha na Mtandao
Dk Huurman ndiye Mkuu wa Kitengo cha Tiba na Afya cha timu ya taifa ya Curaçao.
Nchi hii ni kisiwa kidogo kilichopo chini ya himaya ya Uholanzi na ndilo taifa dogo zaidi kijiografia na kiidadi ya watu (ikiwa na takriban wakazi 150,000 pekee) kuwahi kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia katika historia ya soka.
Kazi yake kubwa ni kuhakikisha miili ya wachezaji wa timu hiyo inakuwa na utimamu, lishe bora, na nguvu ya kuhimili mikanyago na kukabiliana na miamba yenye mamilioni ya watu na miundombinu mikubwa.
Dk Huurman amethibitisha kuwa sayansi haina jinsia. Akiwa na shahada na uzoefu mkubwa katika tiba ya michezo (Sports Medicine), amejizolea heshima kubwa kutokana na uwezo wake wa kusoma na kugundua haraka ukubwa wa majeraha ya misuli ya wachezaji uwanjani.
Sifa nyingine ni kuandaa programu za kisasa za kurejesha utimamu wa mwili kwa haraka baada ya mechi ngumu (recovery programs).
Dk Suzanne Huurman akiwa katika majukumu yake katika kikosi cha timu ya taifa ya Curacao. Picha na Mtandao
Wanawake wengine
Katika historia ya miaka 96 ya Fainali za Kombe la Dunia za Wanaume za FIFA, ni wanawake watatu pekee waliobahatika kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama madaktari wa timu za taifa zilizoshiriki.
Wanawake wengine wawili waliotangulia kabla ya ujio wa Dk Suzanne Huurman ni Dk Celeste Geertsema (New Zealand – 2010).
Huyu ndiye mwanamke wa kwanza kabisa katika historia ya soka duniani kuhudumu kama daktari mkuu wa timu ya wanaume kwenye Fainali za Kombe la Dunia.
Alishika wadhifa huo wakati akiongoza benchi la matibabu la timu ya taifa ya New Zealand (‘All Whites’) kwenye michuano iliyofanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2010.
Mwingine ni Dk Silja Schwarz (Ujerumani – tangu 2023): Dk Schwarz amekuwa mwanamke wa pili wa kihistoria baada ya kuteuliwa na kuanza kufanya kazi na timu ya taifa ya wanaume ya Ujerumani tangu mwaka 2023.
Ameendelea kuwepo kwenye benchi lao la ufundi hadi sasa.
Imeandikwa na Noor Shija kwa msaada wa mtandao.