
Tangu Tanzania iingie katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa miaka 34 iliyopita, Watanzania wengi wamekuwa wakililia kuandikwa kwa Katiba ambayo itatujengea taasisi imara na kutoa hakikisho la utawala wa sheria.
Kuwa na Katiba ni jambo moja lakini kuwa na ukuu wa Katiba ni jambo muhimu zaidi kwa sababu baadhi ya nchi za Kiafrika zina maneno matamu ya haki, lakini kiuhalisia, mambo ni tofauti kabisa.
Ukitizama Katiba ya Ghana ya 1992, Ibara za 1 hadi 5 zinaeleza wazi wazi kuwa mtu yeyote atakayekiuka Katiba anatenda kosa kubwa (high crime) na mwananchi yeyote anaweza kufungua mashitaka Mahakama ya juu au Supreme court.
Mahakama ikiridhika kuwa anayelalamikiwa amevunja Katiba, basi itatoa maelekezo kwa mtu au kikundi cha watu (viongozi) waliovunja Katiba kurekebisha makosa na kuifuata na wanapokaidi wanakuwa wametenda kosa “high crime.”
Endapo ni Rais au makamu wake ametenda kosa hilo, basi inatosha kuwa sababu ya kumuondoa madarakani lakini kama ni mtu mwingine basi anahukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na akimaliza, haruhusiwa kuteuliwa ofisi ya umma.
Hiyo ndio Katiba ambayo pia Watanzania wanaililia tofauti na Katiba ya sasa ya mwaka 1977 na marekebisho yake ya mwaka 2000, ambayo iliandikwa katika mazingira ya chama (CCM) kushika hatamu na haihimili mfumo wa kidemokrasia.
Watanzania wanalilia Katiba mpya na bora inayoweza kuishi katika mazingira ya sasa ya demokrasia ya vyama vingi na itakayotoa hakikisho la utawala bora unaoheshimu kwa dhati utawala wa sheria na sio utawala wa kisiasa.
Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa, maana ya utawala wa sheria ni kwamba hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia Rais wa nchi mpaka mimi mnyonge niliye hapa Mtaa wa Relini, Kata ya Bomambuzi.
Kwa maneno mengine, kuanzia Dola ya nchi mpaka kaya iliyopo kwenye kijiji kidogo kabisa ambacho jina lake halijulikani isipokuwa wenyeji wake. Kwa ufupi ni kwamba kila chombo cha Dola, kila taasisi, kila mtu anawajibika kwa sheria.
Aristotle, aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, alitamka:”Utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi.”
Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizali ambayo hutokea pale utawala wa sheria haupo.
Ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi na utawala wa sheria ni lazima uanze na watawala wenyewe.
Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, basi kama Tangazo la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.
Tunasema hakuna mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria au nje ya sheria. Tunasema kila mmoja wetu anawajibika kwa sheria. Mbona sasa utawala wa siasa ndio unaonekana kuchukua nafasi ya utawala wa sheria?.
Katika utawala wa kisiasa, uamuzi unaofanyika kwa kuwapendeza watu fulani ambao bila kufanya hivyo itakuwa hasara ya kisiasa. Hapo sheria inawekwa pembeni na siasa inachukua mkondo wa sheria ambao haupindi.
Kwa vingine, uamuzi unafanywa kwa woga kukidhi mahitaji ya kisiasa ya wakati husika, na sio kwa kuheshimu sheria ambayo haipindi haki wala wajibu.
Tukiacha siasa itawale badala ya sheria, utekelezaji wa sheria bila woga wala upendeleo unasahauliwa na ni vigumu kuelezea kwa ukamilifu hasara ambayo utawala wa siasa utailetea nchi yetu ambayo ni ya mfumo wa vyama vingi.
Uimarishwaji wa utawala wa sheria utatokana pia na sheria zenyewe. Kwa maneno rahisi, sheria nazo lazima zifuate “sheria”. Sheria kandamizi hazina uhalali wa kisheria. Sheria zinazokiuka Katiba ya nchi hazina uhalali wa kisheria.
Ili sheria zilandane na dhana ya utawala wa sheria, lazima ziwe na sifa kama saba.
Moja, ziwe zinafahamika vizuri na zisizitungwe kwa ajili ya madhumuni finyu, na ziwe hazibadiliki badiliki, mbili, zitumike kwenda mbele, zisisiathiri mambo ambayo yameshapita na tatu, utungwaji wa sheria zenyewe uwe na sheria zake.
Nne, sheria hizo zisimamiwe na Mahakama huru, tano, zinapotumika, basi haki za msingi za kupata fursa ya kujitetea kabla ya kuadhibiwa izingatiwe, sita, Mahakama ziwe na uwezo wa kudhibiti vitendo vya serikali na kuangalia uhalali wa sheria zinazotungwa naB na saba, haki ipatikane bila kucheleweshwa.
Tunapotafakari makala haya, tujiulize Katiba na sheria zetu zinavyozuia kuhojiwa matokeo ya kiti cha urais ni utawala bora? Au ni utawala bora kwa Rais kuteua mwenyekiti na makamishina wa Tume ya Uchaguzi wakati naye ni mgombea?
Tujiulize pia, ni utawala wa sheria kwa polisi wetu kukamata washukiwa wa uhalifu bila kufuata Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) wala Kanuni za Uendeshaji wa Jeshi la Polisi (PGO) na kuwashikilia mahabusu kwa muda mrefu.
Utawala wa sheria unasema hakuna aliye juu ya sheria, sasa tujiulize ni utawala bora kwa Bunge letu kutunga sheria ya kinga ya kutoshitakiwa kwa baadhi ya viongozi wetu na watendaji wa Serikali? Orodha ya wenye kinga inajulikana.
Je, ni utawala wa sheria kwa polisi kubagua kwa kukamata kundi fulani tu la viongozi wa kisiasa wanapotoa kauli zenye mwelekeo wa uchochezi lakini halithubutu kuwagusa wanaotoa kauli kama hizo hizo kwa chama tawala.
Katiba yetu Ibara ya 107A inasema chombo chenye kauli ya mwisho katika utoaji haki ni Mahakama, sasa hao wanaoteka na kupoteza watu wanatumia sheria gani? Kama Bunge letu ni taasisi huru, kwanini haitaki mijadala ya utekaji watu.
Je ni sahihi viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa amri na maagizo kwa watumishi wa umma ambao hawawajibiki kwao? Kwa sheria ya utumishi, wao hawana chama, sasa ni sheria ipi inawapa nguvu CCM kuwaamrisha?.
Hivi ni utawala bora kwa Katiba yetu na Sheria zetu kulazimisha kila anayetaka kugombea nafasi katika vyombo vya Dola (Urais, ubunge, udiwani) ni lazima adhaminiwe na chama cha siasa wakati sio Watanzania wote wana Itikadi.
Mifano ni mingi lakini itoshe kusema utawala wa sheria ni bora kuliko wa siasa na njia pekee ya kuwa na hakikisho hilo ni kuandikwa kwa Katiba mpya.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 0656600900