
Leo ni Jumapili tarehe 6 Muharram 1448 Hijria inayosadifiana na tarehe 21 Juni 2026.
Tarehe sita Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1387 iliyopita katika siku kama hii ya leo mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) aliyekuwa Karbala alimwandikia barua fupi lakini muhimu sana ndugu yake, Muhammad bin Hanafiyya na wafuasi wake kadhaa waliokuwa Madina.
Barua hiyo ilisema: “Kwa jina la Allah, Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu. Hakika anayejiunga nami atapata daraja ya kuuawa shahidi, na ambaye hatajiunga nami hatapata ushindi.”
Barua hii ilikuwa na ujumbe kadhaa, miongoni mwa ujumbe hizo ni kwamba, Imam Hussein alikuwa akijua kuwa, atauawa shahidi yeye na masahaba wake katika mapambano yake na mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya. Pili ni kwamba aliweka wazi hatima ya wale wote watakaofuatana naye katika mapambano ya Karbala na kwamba wote watauawa, na hivyo mtu yeyote mwenye malengo tofauti bora arejee Madina. ****
Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, Habib Bin Madhahir, mmoja wa masahaba wa Mtume Muhammad (saw) na mfuasi wa kweli wa Imam Hussein (as), aliwalingania watu wa kabila la Bani Asad kwa ajili ya kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah.
Katika siku hiyo, sahaba huyo wa Mtume aliomba idhini kwa Imam Hussein (as) kwa kusema: “Ewe mjukuu wa Mtume, katika maeneo haya jirani wanaishi watu wa kabila la Bani Asad, ikiwa utaniruhusu nitaenda kwao nikawalinganie, huenda Mwenyezi Mungu akakuokoa kutokana na shari ya watu hawa makatili kupitia uwepo wa watu wa kabila la Bani Asad.”
Imam Hussein alimruhusu Habib Bin Madhahir ambaye alitoka majira ya usiku kwenda kwa watu wa kabila hilo akiwataka wamsaidie mjukuu huyo wa Mtume. Akiwa katika linganio hilo, sahaba huyo wa Mtume alisema: “Kwa kuwa nyinyi ni watu wa ukoo na kabila langu, ninakulinganieni kufuata njia hii, leo ninakuombeni msikie usia wangu na mfanye haraka kwenda kumsaidia Imam Hussein (as) ili mpate utukufu wa dunia na Akhera.”
Kutokana na wito huo, watu wachache kutoka kabila hilo wanaokadiriwa kufikia 90 walisimama na kwenda kumsaidia mjukuu huyo wa Nabii wa Allah. Hata hivyo baadaye walitoroka na kurejea makwao baada ya kuelewa kwamba jeshi la Omar Bin Sa’ad liliing’amua nia yao, hivyo walihofia kuuawa na jeshi hilo. Baada ya Imam Hussein kusikia habari hiyo, alisema: “Laa haula walaa quwwata illa Billah.”
Siku kama ya leo miaka 1039 iliyopita inayosadifiana na tarehe 6 Muharram mwaka 406 Hijria, alifariki dunia Sayyid Muhammad Hussein Musawi Baghdadi, msomi mashuhuri, mwanafikra na mshairi wa Kiislamu.
Aalim huyo pia alijulikana kwa jina la Sayyid Radhi. Alipata elimu za wakati huo katika kipindi cha ujana wake akiwa pamoja na ndugu yake, Sayyid Murtadha, ambaye pia alikuwa msomi mtajika. Sayyid Radhi aliinukia kuwa msomi mkubwa katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur’ani Tukufu na elimu nyingine za Kiislamu. Msomi huyo alikuwa wa kwanza kuasisi chuo kikuu kwa mtindo wa kisasa na ameandika zaidi ya vitabu 20 katika taaluma za fiqhi, tafsiri ya Qur’ani, historia na fasihi ya Kiarabu.
Kitabu mashuhuri zaidi cha mwanazuoni huyo ni Nahjul Balagha ambacho kinakusanya semi, hotuba, amri, barua na mawaidha ya Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as). ****
Siku kama ya leo miaka 499 iliyopita aliaga dunia Niccolò Machiavelli, mwanahistoria na mwanasiasa wa Italia katika mji wa Florence.
Sambamba na shughuli zake za kisiasa, Machiavelli aliandika pia historia ya Florence. Katika mtazamo wa kisiasa, Machiavelli alikuwa akiamini kwamba yawezekana kutumia wenzo wowote ule kwa ajili ya kupata madaraka na kwa ajili ya kuyalinda, na kwamba hakuna udharura wowote wa kuheshimu misingi ya maadili katika masuala kama hayo.
Miongoni mwa kazi za mwanahistoria na mwanasiasa huyo wa Italia ni “The Art of War” na “The Prince.” ***
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia.
Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa.
Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto. ***
Siku kama ya leo miaka 45 iliyopita inayosadifiana na tarehe 31 Khordad 1360 Hijria Shamsia, sawa na tarehe 21 Juni mwaka 1981, aliuawa shahidi Dakta Mustafa Chamran, msomi na kamanda shujaa wa vikosi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran.
Dakta Chamran alifanikiwa kupata shahada katika fani ya elektroniki na kisha alielekea Marekani ambako alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu.
Kwa miaka kadhaa Dakta Chamran alikuwa nchini Lebanon kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo waliokuwa wakipambana na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Dakta Chamran alichaguliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na kisha akawa mbunge wa Tehran. ****
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, inayosadifiana na 31 Khordad 1369 Hijria Shamsia, mikoa ya Gilan na Zanjan iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa Iran ilikumbwa na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na 7.3 kwa kipimo cha Rishta, na kusababisha maafa makubwa.
Zaidi ya watu elfu hamsini walifariki dunia na wengine zaidi ya elfu sitini kujeruhiwa, na laki tano kukosa makaazi. Mtetemeko huo licha ya maafa yake makubwa kwa binadamu, ulisababisha hasara kubwa ya kiuchumi kwa wananchi na serikali, hasa kwenye miundombinu.