DAR ES SALAAM: Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umeitangazia fursa za uwekezaji katika miradi sita mikubwa ya kimkakati ya barabara kuu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Hatua hiyo inakuja kama matokeo ya mageuzi makubwa ya kisheria na kisera yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan, yenye lengo la kuvutia mitaji ya sekta binafsi ili kupunguza mzigo wa matumizi kwenye bajeti kuu ya Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-Centre), David Kafulila ameeleza hayo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter) amepongeza hatua hiyo ya uwazi.
Kafulila amebainisha kuwa uamuzi wa TANROADS kutangaza fursa hizo duniani na ndani ya nchi ni wa kimkakati, kwani unazifanya fursa hizo zijulikane kwa uwazi na usawa kwa wawekezaji wote wakubwa, huku ukiwapa fursa Watanzania kufuatilia maendeleo ya nchi yao.

Tangazo la TANROADS linatafuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kubuni, kujenga, kugharamia, kuendesha, kutunza na hatimaye kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali. Miradi hiyo ya kihistoria ni pamoja na: Upanuzi wa Barabara ya Morogoro–Dodoma (Km 260), Barabara ya Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida (Km 384), Upanuzi wa Barabara ya Chalinze–Segera–Tanga (Km 246), Mteremko wa Kitonga (Km 27), Barabara ya Mwendokasi (Expressway) Dar es Salaam–Kibaha (Km 42), Expressway ya Katikati ya Jiji hadi Uwanja wa Ndege wa JNIA (Km 10).