Dar/Dom. Mawaziri wamejibu maswali ya wabunge na kuchangia hoja zao katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27 ya Sh62.3 trilioni, wakitoa tahadhari ya ongezeko la idadi ya watu, afya kuwa mtaji wa uchumi na kuboreshwa kwa sekta ya kilimo.
Katika hoja zao, mawaziri hao wa wizara mbalimbali wamehitimisha baadhi ya mijadala ukiwamo wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Serengeti na mapinduzi ya sekta ya bandari.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akizungumza wakati akichangia mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni jijini Dodoma.
Wengine, wamegusia mjadala kuhusu wingi wa wanyama, majibu kuhusu fedha zinazokopwa na Serikali zinavyotumika kuboresha miundombinu.
Hoja ya mikopo
Akizungumza leo Jumatatu Juni 22, 2026 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema mikopo ya maendeleo imechangia kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya barabara na viwanja vya ndege nchini huku akisema si kweli madai ya baadhi ya viongozi wa upinzani kuwa, fedha zinazokopwa hazionekani katika miradi ya maendeleo.
Amesema hakuna mkopo uliopatikana ambao haujaelekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosimamiwa na sekta ya ujenzi na uchukuzi.
Kauli hiyo imekuja wakati kukiwa na mjadala kuhusu ongezeko la mikopo ya Serikali na matumizi yake katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Ulega amesema ushahidi wa matumizi ya mikopo hiyo unaonekana katika maboresho ya viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Sumbawanga, pamoja na miradi inayoendelea katika viwanja vya ndege vya Kigoma, Tanga na Manyara.
“Hakuna kilichokopwa kikakosa kufanya jambo la maendeleo katika barabara na viwanja vya ndege vinavyosimamiwa na Wizara ya Ujenzi,” amesema.
Amesema mikopo hiyo pia imewezesha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato mkoani Dodoma, unaotarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vikubwa vya ndege nchini.
Mbali na sekta ya usafiri wa anga, Ulega amesema Serikali imeelekeza sehemu ya mikopo hiyo katika ujenzi na uboreshaji wa barabara za kimkakati zinazobeba shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni barabara za Kigoma, Kasulu na maeneo ya kusini mwa Tanzania, pamoja na ujenzi wa madaraja yaliyoboreshwa kwa lengo la kuimarisha mawasiliano na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
Mbali na mikopo, Serikali pia imeeleza kuwa inapanua matumizi ya Mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.
Ulega amesema tayari mamlaka husika zimetangaza baadhi ya barabara za kimkakati zinazotarajiwa kujengwa au kuendelezwa kupitia mfumo huo.
Amesema matumizi ya PPP yatasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi, huku yakipunguza mzigo kwa Serikali katika kugharamia miradi yote kwa wakati mmoja.
Waziri huyo amesisitiza kuwa, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha miradi yote inayoendelea na ile iliyosainiwa mikataba inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na matokeo yake.
Pia, ametaja pia miradi ya barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali ya nchi, ikiwamo Kigoma na kusini mwa Tanzania, kuwa sehemu ya mafanikio yaliyowezeshwa na mikopo ya maendeleo.
Ulega amesema Serikali pia imejipanga kufanya ukarabati na upanuzi wa barabara kuu zinazochangia ukuaji wa uchumi, huku baadhi zikitarajiwa kubadilishwa kutoka njia moja kwenda mfumo wa njia mbili.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza usalama wa watumiaji wa barabara, kupunguza msongamano wa magari na kuendana na mahitaji yanayoongezeka ya usafiri nchini.
Waziri huyo amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kukamilisha miradi yote inayoendelea na ile ambayo tayari mikataba yake imesainiwa ili kuepuka kuchelewa kwa utekelezaji wake.
Aidha, amewataka Watanzania kupuuza madai yanayohoji matumizi ya mikopo ya maendeleo na badala yake kutazama matokeo ya miradi iliyotekelezwa katika sekta mbalimbali za miundombinu.
“Mikopo hii ndiyo imewezesha utekelezaji wa miradi mingi ambayo wananchi wanaiona na kuitumia kila siku,” amesema.
Alichokisema Mchengerwa
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema sekta ya afya inapaswa kuondokana na mtazamo wa kuwa mlaji wa fedha za Serikali pekee badala yake kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, uzalishaji wa viwanda na ajira kwa Watanzania.
Amesema ujenzi wa uchumi wa Tanzania si jukumu la Serikali au wizara moja pekee, bali ni wajibu wa kila Mtanzania.
“Kazi ya kujenga uchumi wa Tanzania ni ya mkulima, mfugaji, mvuvi, mama lishe, bodaboda, mfanyabiashara, mwanasayansi, mwekezaji na kila mwananchi mwenye mchango katika uzalishaji,” amesema.
Amesisitiza kuwa, Taifa haliwezi kujengwa kwa maneno matupu, lawama au vurugu, bali kwa jasho, nidhamu, uzalishaji, ulipaji kodi na uzalendo.
Katika mchango wake, Mchengerwa amesema Wizara ya Afya imeanza kusukuma ajenda ya kuifanya sekta hiyo kuwa mshiriki mkubwa wa maendeleo ya uchumi kwa kuimarisha uzalishaji wa dawa, vifaatiba, vitendanishi na chanjo ndani ya nchi.
Amesema kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza bidhaa za afya kutoka nje, jambo linalosababisha ajira, teknolojia na mapato ya kodi kunufaisha mataifa mengine.
“Tunataka fedha za afya zisizunguke hospitalini pekee. Zizalishe viwanda, zijenge ajira, zilinde fedha za kigeni na kuongeza pato la Taifa,” amesema Mchengerwa.
Pia, amesema uzalishaji wa dawa nchini utaleta manufaa manne ikiwamo kuimarisha usalama wa afya kwa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa dawa, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni na kuzalisha ajira kwa vijana.
Amesema kila kiwanda cha dawa au cha vifaatiba kinachojengwa nchini kinamaanisha fursa za kazi kwa wataalamu wa afya, wahandisi, wafamasia na vijana wengine pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.
Akizungumzia hali ya uchumi, Mchengerwa amesema licha ya changamoto mbalimbali za kimataifa, ikiwamo migogoro na vita vinavyoendelea duniani, uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika.
Mchengerwa amewataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu na kuwapa viongozi nafasi ya kutekeleza majukumu yao huku akisisitiza umuhimu wa kufanya uamuzi mgumu kwa masilahi ya Taifa.
“Nchi huru itajengwa na watu wake. Tuwape viongozi wetu nafasi ya kufanya kazi na kuwatumikia Watanzania,” amesema.
Tahadharisha idadi ya watu bila ujuzi
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda ametahadharisha kuhusu ongezeko la idadi ya watu, akisema linaweza kuwa bomu kwa upande mmoja au mtaji kwa upande mwingine.
Profesa Mkenda amesema ili idadi ya watu iwe mtaji, ni muhimu kufanya mageuzi ya elimu kwa kuwajengea vijana ujuzi, wawe na uwezo unaoendana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia na utandawazi, mambo ambayo tayari Serikali imeanza kuyafanya.
Pia, amesema idadi hiyo ya watu inaweza kugeuka kuwa bomu, iwapo ujuzi kwa vijana utapuuzwa na kusababisha kukwamisha hata utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika hoja yake hiyo, Profesa Mkenda amesema Dira ya 2050 inaonesha wapi idadi ya watu inaweza kugeuzwa kuwa mtaji wa maendeleo ya nchi, badala ya kuwa bomu kama watafiti mbalimbali walivyowahi kueleza.
Ameeleza kuwa, dira hiyo na nyenzo zinazotumika ni ajenda ya vijana ambayo lazima wote waitekeleze na muhimu kuangalia idadi ya watu kama mtaji na sio tatizo.
“Lakini ili iwe mtaji, kuna vitu tunapaswa tuyafanye, kuanzia sasa na kila mwaka hadi 2050,” amesema Profesa Mkenda.
Amesema wakati wa uzinduzi wa sera ya elimu, Rais Samia Suluhu Hassan alitaja sababu tatu za mageuzi ya elimu, ambazo ni demografia, utandawazi na mabadiliko ya kasi ya teknolojia.
Profesa Mkenda amesema maswali mengi yanayoulizwa bungeni yanahusu ujuzi na uwezo wa watu, kwamba kwa kiasi gani Serikali inawekeza.
“Hatuwezi kupuuza ujuzi, hatuwezi kupuuza vijana, tukatarajia tutatekeleza dira hii. Tutaita wawekezaji bila ujuzi tutaita na wataalamu kutoka nje,” amesema.
Amesema suala la ujuzi halipaswi kuepukwa na utekelezwaji wake unapaswa kuwa wa kufa au kupona.
Profesa Mkenda ameeleza kuwa, kadiri uchumi unavyodhibitiwa kwa demografia iliyopo, mahitaji ya ajira yatakua kwa sababu wengi watamaliza shule na wengine watazaliwa.
“Kama tusipozalisha ajira za kutosha, kuwa na watu wenye ujuzi wa kuajiriwa, demografia hii tutaiona kama laana, tukijipanga na kuwekeza vema hii ni baraka kubwa,” amesema Profesa Mkenda.
Kuhusu utandawazi, amesema ikiwa kuna idadi kubwa ya watu ambao uchumi wao unakua, lakini kwa kiasi kikubwa wananunua kutoka nje, hilo linaweza kuwa balaa.
“Lakini tukiandaa vijana wetu vizuri, wakawa na ushindani duniani, na ujuzi wa kawaida tu, hata wa kutengeneza suti, wakawa nao wanakwenda kufanya nchi nyingine, sisi kwetu utandawazi utakuwa baraka kubwa utakaotusaidia kusonga mbele,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe, akichangia mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.
Ameeleza utandawazi ni mzuri, lakini nchi imejipanga vipi kuhakikisha unakuwa na tija kwa Taifa.
Profesa Mkenda amesema Serikali imejipanga vema hasa kwenye kuwaandaa vijana kuwa na ujuzi na hilo linaanza kwa kuhakikisha watoto wanamaliza elimu wakiwa na umri wa kuweza kuajiriwa.
Pia, amesema mtiririko wa elimu hasa ya sekondari unakuwa na amali ili watoto wajifunze ujuzi wakiwa shuleni na kuwawezesha kuwa na uwezo wa kuajirika.
Bandari ya Uvuvi Kilwa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally amesema ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa umefikia asilimia 99.9 na majaribio ya mitambo yataanza wiki ijayo kabla ya uzinduzi wake unaotarajiwa kufanyika kati ya Agosti na Septemba mwaka huu.
Dk Bashiru amesema Agosti au Septemba mwaka huu, Rais Samia anatarajia kuizundua bandari hiyo.
Amesema bandari hiyo itakuwa ya kwanza ya uvuvi katika ukanda wa Afrika Mashariki na inatarajiwa kubadilisha sekta ya uvuvi wa bahari nchini.
“Tunapozungumza sasa, wataalamu wa Serikali wameweka kambi kwa ajili ya mchakato wa makabidhiano ya mradi huo. Wiki ijayo tunaanza majaribio ya mitambo na kati ya mwezi wa nane na wa tisa mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan atazindua bandari hii,” amesema Dk Bashiru.
Amesema Sh280 bilioni za Watanzania zimewekezwa katika mradi huo utakaokuwa kichocheo cha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata samaki, huduma za usafirishaji na sekta ya utalii wa bahari.
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema uamuzi wa Serikali kujenga Uwanja wa Ndege wa Serengeti, unalenga kutoa fursa zaidi kwa ukuzaji wa sekta ya utalii.
Profesa Mbarawa ameeleza hayo ikiwa ni takriban wiki moja tangu kuibuke mjadala miongoni mwa wabunge kuhusu umuhimu wa ujenzi wa uwanja huo, huku baadhi wakipendekeza ujengwe wa Mwanza.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Geita (CCM), Joseph Musukuma alisema hapingi kujengwa uwanja wa ndege Serengeti, isipokuwa haupaswi kujengwa wa kimataifa na juhudi zipelekwe kwenye uboreshwaji wa Uwanja wa Mwanza kuwa wa kimataifa.
Mbunge wa Bunda, Boniface Getere, alisema kujengwa kwa uwanja huo sio kwa ajili ya mapato ya Serikali pekee, bali kutahifadhi ikolojia ya eneo hilo na kuvutia watalii zaidi.
Profesa Mbarawa amesema hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatatu, Juni 22, 2026 alipochangia hoja katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema anafahamu jambo hilo liliibua mjadala bungeni, lakini Serikali inajenga uwanja huo kwa lengo maalumu na inaamini itatoa fursa zaidi kwa sekta ya utalii.
“Utarahisisha watalii kushuka pale na hii sio kwa Tanzania tu nchi nyingi duniani zinafanya hivyo,” amesema.
Ujenzi wa Minara
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki amesema Serikali imeweka mkakati wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia Teknolojia na Habari na Mawasiliani (Tehama) ili kudhibiti uvujaji wa fedha.
Amesema wabunge walishauri Serikali kuboresha mfumo wa Tehama na kuunganisha mifumo ya malipo iliyotolewa na mbunge wa Tarime Mjini (CCM), Esther Matiko.
Kuhusu mawasiliano, amesema jumla Sh229 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kujenga minara 287 maeneo ya mipakani na inakopita Reli ya Kisasa (SGR) huku mingine 304 ikifanyiwa maboresho ya kuongeza uwezo wa usikivu.
Kingine ni ujenzi wa kilomita 186 za Mkongo wa Taifa ili kuunganisha na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) lakini na kwenye wilaya 17 ambazo hazijapitiwa na mkongo.
Mjadala wa Simba na tembo
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji amesema kufuatia ongezeko la wanyama wakiwamo tembo na simba, Serikali imepanga kuja na mjadala wa kitaifa juu ya nini kifanyike kuhusu ongezeko hilo.
“Wakati tulipopata uhuru 1961, nchi yetu ilikuwa na tembo 134,000, mwaka 2014 tembo walikuwa 34,000 lakini kwa sensa ya mwaka 2025 inaonesha tembo wamefikia 66,714,” amesema Dk Kijaji.
Waziri amesema kwa sasa wizara hiyo inafanya maandalizi ya filamu nyingine baada ya iliyofanyika miaka michache ikimhusisha Rais Samia kuonesha mafanikio makubwa.