Texas, Marekani. Mabao mawili ya nahodha wa Argentina, Lionel Messi aliyofunga katika dakika za 39 na 90 dhidi ya Austria yameifanya timu hiyo kufuzu hatua ya 32 ya Kombe la Dunia.
Mbali na hilo, yamemfanya Messi afikishe mabao 18 na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa mashindano hayo.
Kabla ya mechi ya leo, Messi alikuwa akishikilia rekodi hiyo sambamba na Miroslav Klose wa Ujerumani kila mmoja akiwa na mabao 16.
Argentina imefuzu hatua ya 32 bora kwa vile imefikisha pointi sita ambazo zitaifanya imalize katika nafasi mbili za juu kwenye kundi lake.
Nahodha wa Argentina, Lionel Messi akishangilia bao la pili katika mechi ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Austria. Picha na Mtandao
Hata hivyo huo unakuwa muendelezo wa mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona kufunga mabao baada ya kufanya hivyo katika mechi ya kwanza dhidi ya Algeria ambapo alifunga mabao matatu (hat trick).
Vilevile nyota huyo amekuwa na muendelezo katika michuano hiyo akifunga katika mechi sita mfululizo za Kombe la Dunia.
Anakua mchezaji wa tatu katika historia ya mashindano hayo kufunga kwenye michezo sita mfululizo, baada ya Just Fontaine (Ufaransa) na Jairzinho (Brazil).
Ikiwa nyota huyo atafunga mechi ya mwisho ya kundi dhidi ya Jordan atakuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao kwenye mechi saba mfululizo za Kombe la Dunia.
Baadhi ya wachezaji wa Argentina wakishangilia moja ya bao katika mechi ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Austria. Picha na Mtandao
Katika mechi hiyo iliyopigwa Dallas, Austria iliingia ikiwa na matumaini makubwa baada ya kuifunga Jordan mabao 3-1 katika mchezo wake wa kwanza, huku Argentina ikitoka kuichapa Algeria mabao 3-0.
Hivyo, pambano hilo lilikuwa kama fainali kutokana na ubora waliouonyesha kwenye mechi zao za kwanza za kundi hilo.
Messi alianza kwa kukosa penalti jambo lililowapa Austria nguvu ya kuamini wanaweza kufanya kitu mbele ya mabingwa hao watetezi wa dunia.