Wakili mashuhuri na mwanasiasa kutoka nchini Kenya Martha Karua amezuiwa kuingia nchini Uganda na kufukuzwa nchini, alikokuwa amekwenda kuhudhuria kesi ya wakili Erias Lukwago aliyefunguliwa mashtaka ya uhaini.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Martha Karua na Erias Lukwago ni Mawakili wa mwanasiasa mkongwe Kizza Besigye ambaye amekuwa akizuiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Lukwago alikamatwa Jumatatu wiki iliyopita kwa amri ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda na mtoto wa rais Yoweri Museveni Jenerali Muhoozi Kainerugaba na kushtakiwa mahakamani baada ya siku mbili kwa kosa la kuficha uhaini.

Martha Karua alikuwa amesafiri akiwa na mkuu wa wanasheria nchini Kenya Charles Kanjama ambaye anaeleza kilichotokea.

“Tulipofika kwenye uwanja wa ndege, tukapita sehemu ya uhamiaji na tukaruhusiwa kuingia nchini lakini baada ya Martha Karua kupita akaitwa tena na akaambiwa wamepata onyo asiruhisiwe kuingia Uganda.” Amesema Wakili Kanjama.

Hakuna maelezo rasmi ambayo yametolewa na mamlaka ya uhamiaji kuhusu swala hili. Mwanasheria Karua ana kibali kilichotolewa na Baraza la Sheria la Uganda kinachomruhusu kufanya kazi nchini Uganda na amekuwa pamoja na Erias Lukwago akimwakilisha Dkt Besigye katika kesi ya uhaini bila kipingamizi chochote.

Uamuzi wa kumzuia kuingia Uganda umelaaniwa na chama cha Wanasheria wa Uganda na viongozi wa upinzani.

Medard Ssegonna ni wakili wa Erias Lukwago.

“Mheshima Martha Karua amezuiliwa na kufukuzwa nchini. Hii ni mbaya na sio roho ya jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni suala ambalo linashugulikiwa na chama cha Wanasheria wa Uganda na chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki.” Ameeleza Medard Ssegonna wakili wa Erias Lukwago

Wakati huo huo, hakimu katika kesi ya Erias Lukwago Sarah Basemera ameamua kutoa uamuzi wake wa ombi la dhamana kupitia barua pepe ndani ya saa 24. Lukwago anataka achiliwe akisema afya yake inazidi kuzorota jambo ambalo upande wa mashtaka umepinga.

Kenneth Lukwago, Kampala, RFI Kiswahili

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *