
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ametangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uwaziri Mkuu pamoja na uongozi wa Chama cha Labour, katika hatua inayotajwa kuashiria mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini humo.
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatatu Juni 22, 2026, imeelezwa kuwa Starmer ameamua kuachia madaraka kutokana shinikizo la kisiasa lililokuwa likiongezeka ndani ya chama chake pamoja na mijadala ya ndani kuhusu mustakabali wa uongozi wa serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo umefungua rasmi ukurasa mpya ndani ya Chama cha Labour, huku mchakato wa kumpata mrithi wake ukitarajiwa kuanza mara moja.
Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa taratibu za mpito wa madaraka zitaendelea kwa utaratibu ili kuhakikisha hakuna pengo la uongozi katika kipindi hiki cha mabadiliko.
Kujiuzulu kwake kumefanya Uingereza kujikuta katika wakati mgumu wa kisiasa, ambapo sasa inaelekea kuwa na kiongozi wa saba ndani ya kipindi cha miaka 10 pekee, hali inayoashiria mzunguko wa kasi wa mabadiliko ya uongozi usio wa kawaida kwa taifa hilo kubwa barani Ulaya.
Taarifa hizo zimezidi kuleta mjadala mpana ndani ya Chama cha Labour pamoja na vyama vingine vya siasa, huku wachambuzi wakieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza presha ya mchakato wa kumpata mrithi atakayekabiliana na changamoto za kiuchumi, kijamii na kisiasa zinazoikabili nchi hiyo.
Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Uingereza imekuwa ikishuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ya viongozi wakuu, hali inayoleta taswira ya kutokuwepo kwa utulivu wa muda mrefu katika uongozi wa taifa hilo.
Endelea kufuatilia Mwananchi…