Arusha. Aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo ameibuka hadharani baada ya kipindi kirefu cha ukimya wa kisiasa, akiwashukuru wananchi wa Arusha kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake cha miaka mitano ya ubunge.

Jana Jumapili, Juni 21, 2026, Gambo alikuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Makao Makuu ya Kanisa la Pentecostal Revival Church (PRC) Kanda ya Kaskazini iliyofanyika jijini Arusha.

Gambo alikuwa mbunge wa Arusha Mjini mwaka 2020-2025. Kabla ya hapo, alikuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha. Katika mchakato wa ndani wa CCM kumpata mgombea ubunge, Gambo aliwekwa kando na tangu wakati huo alikaa kimya takribani miezi tisa.

Katika hotuba yake, Gambo amesema anawashukuru wananchi wa Arusha Mjini kwa nafasi waliompa ya kuwatumikia na kwamba ataendelea kuthamini mchango wao katika maisha yake ya kisiasa na kijamii.

“Nitumie pia fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Arusha kwa ushirikiano na sapoti waliyonipa katika kipindi chote nilichopata nafasi ya kuwatumikia wananchi wa Arusha katika nafasi zote,” amesema.

Amesema kusimama hapo kwa mara ya kwanza na kuzungumza ni wito wa kutoa mchango kama sadaka yake kwa Mungu kwa mapito yote ya maisha na kisiasa aliyopitia.

“Tangu nihitimishe uongozi wangu wa ukuu wa wilaya, mkuu wa Mkoa (wa Arusha) na ubunge sijawahi kusimama popote, nimeamua kunyamaza kimya kwa kila jambo maana naamini kimya nayo ni jibu zuri kwa nyakati zote,” amesema.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanasiasa huyo kuonekana hadharani katika shughuli kubwa ya kijamii tangu alipoachwa nje ya mchakato wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa Arusha Mjini mwaka jana.

CCM ilimpitisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuwania ubunge na katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambaye aliibuka mshindi.

Katika hotuba yake, Gambo pia amezungumzia umuhimu wa haki katika kujenga amani ya kudumu nchini akisema haiwezi kutenganishwa na haki.

“Nchi yoyote inayotafuta amani lazima ihakikishe haki inatendeka, amani ya kweli hujengwa juu ya misingi ya haki,” amesema.

Amewataka viongozi wa dini kuendelea kuhubiri amani, maridhiano na mshikamano wa kitaifa huku akisisitiza maridhiano ya kweli lazima yawe na msingi wa haki na ukweli.

“Amani lazima iende sambamba na haki na ndivyo ilivyo kuwa maridhiano ya kweli yanapaswa kuwa na ukweli na nia ya dhati ya kulijenga Taifa,” amesema.

Akizungumzia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea jijini Arusha amesema ana furaha kuona matunda ya alichopigania kwa miaka mitano yanaonekana.

“Miradi ikiwamo ya uwanja wa mpira wa Afcon, masoko ya Mrombo na Kilombero na pia ujenzi wa barabara za nje nne zinazoendelea ni matunda ya bajeti yetu tuliyopitisha Bunge lililoisha ambalo linaishia Juni 30,2026,” amesema.

“Hivyo baada ya miaka hii mitano mtaona thamani ya mlichokuwa nacho na kitakachokuwa nacho miaka ijayo,” amesema.

Akizungumzia maisha yake binafsi, Gambo amesema anaamini changamoto zote zinazotokea katika maisha hutokea kwa mapenzi ya Mungu na kwamba amejifunza kukubaliana na mipango ya Mungu.

“Sisi wanadamu tunaweza kujiuliza kwa nini jambo limetokea au halikutokea, lakini Mungu huona mbali zaidi kuliko mwanadamu. Mimi nimekubaliana na mpango wa Mungu,” amesema.

Katika mchango wa harambee Gambo ametoa Sh10 milioni ambayo amesema hiyo ni sehemu ya sadaka yake ya shukrani kwa Mungu.

Awali, Askofu wa PRC Kanda ya Kaskazini, Kredo Adam amesema lengo la harambee hiyo ni kukusanya Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kanisa la makao makuu ya Kanda ya Kaskazini.

Amesema katika kanisa lao lenye makanisa saba Kanda ya Kaskazini wanatarajia kuanza mradi mwezi ujao katika kiwanja walichonunua eneo la kwa Mrombo lenye ukubwa wa ekari 1.5.

Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh250 milioni zimeahidiwa kati ya hizo Sh150 milioni zimekusanywa.

Gambo aliwahi kuwa mkuu wa Wilaya ya Korogwe kabla ya kuhamishiwa Wilaya ya Arusha na baadaye kuteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Arusha. Mwaka 2020 alichaguliwa kuwa mbunge wa Arusha Mjini na kulitumikia jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *