
Azimio namba 2823 (2026) linazitaka pande zote husika kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kuwezesha utambuzi, uchunguzi na kufikishwa mahakamani kwa wahusika wa mashambulizi hayo bila kuchelewa.
Rasimu ya azimio hilo imewasilishwa na Denmark na Pakistan, wanachama wawili wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama, na kuungwa mkono na zaidi ya nchi 150.
Kupambana na kutokuwajibika
Balozi Asim Iftikhar Ahmad wa Pakistan amewasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya wadhamini hao wawili.
Amekumbusha kuwa karibu walinda amani 4,500 wa Umoja wa Mataifa wamepoteza maisha wakiwa kazini, wakiwemo 183 kutoka Pakistan.
Amebainisha kuwa azimio hilo linaendeleza misingi ya maazimio mawili yaliyopita ambayo yaliimarisha ushiriki wa Baraza la Usalama katika kulinda usalama wa walinda amani.
Amesema kuwa katika operesheni mbalimbali za kulinda amani, mashambulizi dhidi ya walinda amani yameongezeka kwa idadi na kwa kiwango cha utata wa mbinu zinazotumika. Aidha, walinda amani wamekuwa wakilengwa moja kwa moja huku mara nyingi wahusika wakikosa kuwajibishwa.
“Walinda amani wanapouawa au kujeruhiwa kutokana na mashambulizi wakati wakitekeleza majukumu yaliyoidhinishwa na Baraza hili, basi Baraza lazima lifuatilie kinachotokea baadaye: kama ukweli umebainishwa, kama uchunguzi unaendelea, kama wahusika wametambuliwa na kama haki imetendeka,” alisema.
“Kutowajibika kwa uhalifu wa aina hii hakupaswi kuruhusiwa kuendelea. Lazima kuwe na uwajibikaji.”
Kusaidia uchunguzi
Azimio hilo linamwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa, endapo kutatokea mashambulizi mengine dhidi ya walinda amani siku zijazo, operesheni za kulinda amani zinakusanya kwa haraka taarifa sahihi za matukio hayo na kuzifanya zipatikane kwa ajili ya uchunguzi unaofanywa na nchi mwenyeji.
Pia linazitaka nchi zote husika na wahusika wengine kushirikiana kikamilifu katika uchunguzi huo.
Katibu Mkuu ametakiwa kumteua afisa mwandamizi wa kuratibu masuala ya uwajibikaji kwa uhalifu dhidi ya walinda amani, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uratibu na uwezo wa kushughulikia changamoto hizo.
Vilevile, Katibu Mkuu ameombwa kuwasilisha ripoti ya kila mwaka kwa Baraza la Usalama kuhusu hali ya kesi zinazohusiana na mauaji au vitendo vya ukatili dhidi ya walinda amani, ambapo ripoti ya kwanza inapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 120.
“Ujumbe muhimu na wenye nguvu”
Baada ya kura ya kupitisha azimio hilo, Balozi Christina Markus Lassen wa Denmark a amesema kuwa uungwaji mkono wa kauli moja “unatuma ujumbe muhimu na wenye nguvu”.
Kwa zaidi ya watumishi 50,000 wanaohudumu katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa duniani kote kwa sasa, amesema kuwa azimio hilo linaonesha kwamba Baraza la Usalama “limesimama imara nyuma yao”.
Kwa nchi zinazochangia wanajeshi na polisi katika operesheni hizo, amesema azimio hilo linatoa uhakikisho kwamba endapo kutatokea uhalifu dhidi ya walinda amani, Baraza la Usalama na mfumo wa Umoja wa Mataifa “uko tayari, una nia na una uwezo wa kuchukua hatua”.
Na kwa wahusika wa uhalifu huo, amesema azimio hilo linatuma ujumbe thabiti kwamba jumuiya ya kimataifa inafuatilia kwa karibu, kwamba uhalifu huo hautabaki bila adhabu, na kwamba uwajibikaji pamoja na haki vitasimamiwa na kutekelezwa.