Baada ya kushindwa kikamilifu mbinu zake zote za vikwazo, vitisho vya kijeshi na mashinikizo ya kisiasa, vitisho vipya vya Trump dhidi ya Iran vinaashiria wazi kushindwa kwake kimkakati, kabla ya kuwa ni dhihirisho la nguvu za Marekani.

Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, Donald Trump ametumia karibu kila mbinu kwa ajili ya kuishinikiza Iran: Kuanzia vitisho vya mara kwa mara vya kijeshi na kuimarisha majigambo ya kijeshi ya Marekani katika eneo, hadi kuanzisha vita vya siku arubaini, kuongeza mashinikizo ya kisiasa, na majaribio ya kuweka mzingiro wa majini dhidi ya Iran. Lengo la pamoja la hatua zote hizi lilikuwa kuilazimisha Iran iachane na misimamo yake ya kimkakati, lakini mwenendo wa matukio umeonyesha kuwa hakuna hata mbinu moja kati ya hizo iliyoweza kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na Washington. Sasa, rais wa Marekani ameanzisha tena mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran, chaguo ambalo si tu kwamba karibuni hivi lilishindwa kumletea matokeo yaliyokusudiwa, bali pia tangu mwanzo lilitabiriwa kufeli na wachambuzi wengi wa Magharibi.

Katika muktadha huu, John Mearsheimer, msomi mashuhuri wa taaluma ya mahusiano ya kimataifa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chicago, ana shaka kubwa kuhusu kufanikiwa chaguo la kijeshi la Marekani dhidi ya Iran. Anaamini kuwa serikali ya Marekani imeshindwa kufafanua namna mashambulizi ya kijeshi ya sasa yatakuwa na matokeo tofauti na ya huko nyuma. Kwa mtazamo wa Mearsheimer, matumizi ya nguvu yana mantiki pale tu yanapokuwa na malengo ya kisiasa yaliyo wazi, yanayoweza kufikiwa, na yanayolingana na gharama zinazokubalika, hali ambayo haijathibiti kabisa kuhusiana na Iran. Hivyo, kurudia chaguo la kijeshi badala ya kutekeleza mkakati mpya, kunaashiria kushindwa Washington kubuni suluhisho madhubuti la kukabiliana na Iran.

Uzoefu wa miezi ya karibuni unathibitisha wazi ukweli huu. Licha ya kukabiliwa na mashinikizo makubwa ya kijeshi, kiusalama na kisiasa, Iran si tu imeendelea kudumisha mfumo wake wa kuzuia uchokozi (deterrence), bali pia imefanikiwa kuongeza gharama za adui mchokozi. Hali hii haihusu tu uwezo wa kijeshi wa Iran bali inajumuisha pia uwezo wake wa kimkakati, kijiopolitiki, uwezo wa kulipiza kisasi, na ushawishi wa kikanda, vipengele ambavyo vimefanya tathmini yoyote kuhusu hatua za kijeshi dhidi ya Iran kukumbwa na shaka na wasiwasi mkubwa. Kwa maelezo haya, dhana kwamba Iran inaweza kulazimishwa kubadili msimamo wake wa kimkakati kupitia mashambulizi machache yenye malengo maalum au hata operesheni kubwa ya kijeshi, haiendani na uhalisia wa mambo katika eneo. Katika miaka ya karibuni, imethibitika wazi kupitia uzeofu kuwa mlinganyo wa kiusalama katika eneo la Asia Magharibi hauwezi kubadilishwa kwa kutumia mbinu ya nguvu za kijeshi. Hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran inaweza kuwa na taathira zinazovuka mipaka ya Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormuz, na hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa maslahi ya Marekani na washirika wake katika eneo.

Katika mazingira hayo, vitisho vya mara kwa mara vya Trump dhidi ya Iran vinapaswa kuchambuliwa katika muktadha wa msuguano wa kimkakati unaoikabili Washington. Kwa upande mmoja, utawala wa Marekani hautaki kukubali ukweli kwamba umepoteza nyenzo zake za mashinikizo, na kwa upande mwingine, uzoefu unaonyesha kuwa kutekeleza vitisho hivyo kunaweza kuisababishia Washington gharama kubwa kuliko faida. Hivyo, lugha ya vitisho imebadilika kuwa chombo cha kudumisha mashinikizo ya kisaikolojia na kisiasa, kuliko kuwa utangulizi wa hatua madhubuti.

Katika mtazamo wa kimkakati, tatizo kuu la Marekani ni kutokuwa na lengo la kisiasa linaloweza kufikiwa. Katika nadharia za kitamaduni za mahusiano ya kimataifa, nguvu za kijeshi zinaweza kufanikiwa tu pale zinapoambatana na malengo ya wazi ya kisiasa. Hilo lisipotimia, matumizi ya nguvu sio tu hushindwa kutatua matatizo yaliyopo bali pia yanaweza kuzidisha mgogoro.

Katika miaka iliyopita Iran imejenga mfumo wake wa kuzuia hujuma ya adui kwa kuongeza gharama za uchokozi wa adui. Uzuiaji huu hautimii kwa vifaa vya kijeshi pekee, bali ni mchanganyiko wa uwezo wa kujilinda, yakiwemo makombora, ndege zisizo na rubani, udhibiti wa mgogoro na uwezo wa kuathira hali ya mambo katika maeneo ya karibu. Ni sifa hizi ndizo zimefanya chaguo la kijeshi dhidi ya Iran kuwa chaguo lenye gharama kubwa na lisilotabirika kwa Marekani.

Ukweli wa mambo ni kwamba mzozo wowote mpya na Iran hautaishia ndani ya mipaka yake bali utaathiri moja kwa moja usalama wa nishati, njia za usafiri wa baharini, masoko ya kimataifa na usalama wa nchi nyingine za eneo. Hali kama hii imewafanya hata baadhi ya washirika wa Marekani kuelezea wasiwasi wao mkubwa kuhusu ongezeko la mivutano katika eneo, kwani gharama za kiuchumi na kiusalama hazibebwi na Iran pekee, bali na nchi zote za eneo na kimataifa.

Sambamba na mambo haya, uzoefu wa vita vya Marekani katika eneo katika miongo miwili iliyopita pia ni muhimu kuzingatiwa. Migogoro ya Afghanistan, Iraq, na maeneo mengine ya Asia Magharibi imethibitisha kuwa nguvu za kijeshi hazina maana ya moja kwa moja ya mafanikio ya kisiasa. Katika migogoro mingi kati ya hiyo, na licha ya kuwa na nguvu kubwa za kijeshi, lakini Washington imeshindwa kufikia malengo yake ya muda mrefu na hatimaye kukabiliwa na gharama kubwa za kifedha, kiuchumi, kibinadamu na kisiasa. Uzoefu huo wa kihistoria umewafanya wataalamu wengi wa Marekani kutoa tahadhari dhidi ya kurudiwa makosa yaliyofanyika huko nyuma.

Hata kama vitisho vya maneno vinaweza kuathiri mazingira ya kisiasa na ya vyombo vya habari kwa muda mfupi, lakini haviwezi kubadilisha hali halisi ya mambo ikiwa havitaambatana na mkakati halisi na malengo yanayoweza kufikiwa. Ukweli ni kwamba uhusiano wa Iran na Marekani haufafanuliwi tena kwa nguvu za kijeshi pekee; bali kuna mambo kadhaa ya kisiasa, kiusalama, kiuchumi, na ya kikanda yanayochangia mafanikio, mambo ambayo yamefanya uamuzi wowote wa kutumia nguvu dhidi ya Iran kuwa suala tata sana.

Madamu Marekani haitabuni mkakati unaoendana na uhalisia mpya wa mambo katika eneo pamoja na kuzingatia uwezo mkubwa wa Iran wa kuzuia uchokozi, uwezekano wa kupata matokeo tofauti na ya huko nyuma utabakia kuwa ndoto. Katika mazingira haya, lugha ya vitisho, kabla ya kuwa inaashiria nguvu, inaakisi msuguano wa kimkakati unaoikabili Marekani katika kukabiliana na Iran; hali ambayo imeiacha Washington ikiendelea kuyumbayumba kati ya kuonyesha nguvu bandia na mwishowe kushindwa kufikia malengo yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *