Morogoro. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wajane, baadhi ya wajane katika Mkoa wa Morogoro wameeleza machungu wanayoyapitia baada ya kufiwa na waume zao.
Wamesema changamoto hizo zimekuwa zikiathiri maisha yao ya kila siku, ikiwemo unyanyapaa, migogoro ya kifamilia na ukosefu wa haki za msingi, huku wakiiomba jamii na Serikali kuendelea kuwasaidia kupata haki zao na kuishi kwa amani.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wajane hufanyika kila Juni 23. Siku hii ilianzishwa rasmi na Umoja wa Mataifa mwaka 2010.
Kwa upande wake mjane Asha Ally ametoa ushuhuda akieleza namna maisha yake yalivyobadilika ghafla baada ya kufiwa na mume wake, yakimwingiza katika kipindi kigumu kilichojaa migogoro ya kifamilia, mashinikizo na madai ya kutaka kuondolewa kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.
Asha anasema wakati mume wake akiwa mgonjwa, alibaki akimuguza peke yake huku ndugu wa marehemu wakijitenga bila msaada wowote.
Baadhi ya wajane wa manispaa ya Morogoro wakiwa kwenye kongamano la siku ya wajane ambayo kitaifa inafanyika Kibaha mkoani Pwani. Picha Hamida Shariff
Hata hivyo, baada ya kifo hicho, hali ilibadilika ambapo ndugu wa marehemu walijitokeza na kumtaka aonyeshe hati ya nyumba waliyokuwa wakiishi, kisha wakamwamuru aondoke kwa madai kuwa hakuzaa na marehemu.
“Ni kweli sikuzaa naye na nyumba niliikuta, lakini mimi ni mke wa ndoa. Baada ya msiba walinitaka niondoke. Niliishi humo kwa siku 40 kisha nikaondoka na kwenda kuishi kwa ndugu yangu Kilosa,” anasema Asha.
Baadaye alirejea Morogoro mjini na kuanza biashara ndogo ndogo za matunda na mboga ili kujikimu kimaisha.
Mjane mwingine, Mariam Shabani, anasema alipofiwa na mume wake ambaye alikuwa akisumbuliwa na kisukari, alituhumiwa kuwa amemtelekeza kwa sababu siku ya kifo chake alikuwa Morogoro akimuguza baba yake.
Anasema tuhuma hizo zilimfanya akataliwe hata kushiriki ipasavyo katika mazishi.
Amesema licha ya changamoto hizo, faraja yake kubwa ni kwamba mume wake aliacha wosia uliompa jukumu la kulea watoto na mgawanyo wa mali.
Kwa upande wake, Matha Selemani anasema baada ya msiba wa mume wake, ndugu wa marehemu walihamia nyumbani kwake wakidai wanasimamia mali na malezi ya watoto.
Anasema hali hiyo ilimfanya maisha yake kuwa magumu kutokana na msongamano wa watu na mgogoro wa mali uliodumu kwa muda.
Hata hivyo, anasema baada ya taratibu za mirathi kukamilika, alipata haki yake na watu waliokuwa wamehamia nyumbani kwake waliondoka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wajane (CCWT) Mkoa wa Morogoro, Dorothy Mwamsiku anasema baadhi ya wajane hukumbwa na mateso kutoka kwa ndugu wa waume zao, wakiwemo mawifi, mashemeji na wakwe, wanaowashutumu kwa uchawi na kuamini kuwa wamehusika na vifo vya waume zao.
Amesema hali hiyo husababisha migogoro ya mali na wakati mwingine wajane huamua kuachia haki zao ili kuepuka madhara na kuishi kwa amani.
“Wajane wananyanyasika na wakati mwingine wanashutumiwa kuwa wameroga waume zao. Hali hii husababisha migogoro ya mali na kuwafanya wajane wengi kuachia haki zao ili wawe salama,” amesema Mwamsiku.
Baadhi ya wajane wa manispaa ya Morogoro wakiwa kwenye kongamano la siku ya wajane ambayo kitaifa inafanyika Kibaha mkoani Pwani. Picha Hamida Shariff
Historia ya Siku ya Wajane
Siku ya Kimataifa ya Wajane ilianzishwa na taasisi ya The Loomba Foundation, ikiwa na lengo la kuangazia kile kinachoitwa “janga lisiloonekana” linalowakumba wajane duniani.
Kwa mujibu wa taasisi hiyo, wajane wengi hukumbwa na umasikini uliokithiri, kunyimwa haki za urithi, kubaguliwa kijamii na wakati mwingine kukosa msaada wa msingi baada ya kufiwa na waume zao.
Tarehe 23 Juni ina umuhimu maalumu kwa taasisi hiyo, kwani ni siku ambayo mwaka 1954, Shrimati Pushpa Wati Loomba, mama wa mwanzilishi wa taasisi hiyo, Lord Loomba, alifiwa na mume wake na kuwa mjane.
Tukio hilo lilihamasisha kuanzishwa kwa kampeni ya kimataifa ya kuwatetea wajane na hatimaye kuanzishwa kwa siku maalum ya kimataifa ya kuwaenzi na kuwasaidia.
Siku ya kwanza ya maadhimisho ya International Widows Day ilifanyika mwaka 2005, ikiongozwa na Lord Loomba pamoja na Cherie Blair, mke wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair.
Kwa mujibu wa kitabu cha mwaka 2010 kilichoitwa ‘Invisible, Forgotten Sufferers: The Plight of Widows Around the World’, inakadiriwa kuwa kuna takribani wajane milioni 245 duniani kote.
Kati ya hao, takribani milioni 115 wanaishi katika hali ya umasikini na wanakabiliwa na changamoto za kijamii na kiuchumi, ikiwemo ubaguzi na kunyimwa fursa kwa sababu ya kupoteza waume zao.
Ripoti hiyo iliwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo, Ban Ki-moon, Juni 22, 2010 kama sehemu ya juhudi za kuhamasisha hatua za kimataifa.