
Katika hotuba yake aliyotoa leo wakati wa Wiki ya Hatua dhidi ya tabianchi mjini London, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza jinsi utegemezi wa mafuta kwa uchumi wa dunia unavyochochea janga la tabianchi na pia mgogoro wa uhuru wa nishati, ambao umehusishwa na usumbufu mkubwa wa usafirishaji wa baharini katika Mlango Bahari wa Hormuz na vita kati ya Israeli, Marekani na Iran.
“Migogoro hii inaweza kuonekana kuwa tofauti, lakini inashiriki nguvu ileile ya uharibifu, mafuta ya kisukuku. Inahitaji jibu lilelile, mpito wa haraka na wa haki kuelekea nishati safi pamoja na kuimarisha hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, mnepo na haki ya tabianchi kwa wale ambao tayari wanakumbwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi,” amesema Bwana. Guterres.
Ametoa wito wa uongozi wa kisiasa kusukuma mabadiliko ya kimataifa yanayofanana na yale yaliyohitajika kuondoa matumizi ya petroli yenye risasi na kupiga marufuku kemikali zilizosababisha tundu katika tabaka la ozoni.
Kigezo cha Paris
Miaka 10 imepita tangu viongozi wa dunia walipokubaliana mjini Paris kuweka kikomo cha ongezeko la joto duniani katika nyuzi joto 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, hatua iliyokuwa mfano wa mshikamano wa kimataifa ulioongozwa na Umoja wa Mataifa.
Leo, ingawa Mkataba huo bado upo na licha ya Marekani kujiondoa rasmi kwa mara ya pili mwezi Januari mwaka huu kwenye mkataba huo wanasayansi wanasisitiza kuwa wastani wa joto la kila mwaka duniani utavuka kiwango hicho katika miaka ijayo.
“Kila sehemu ya nyuzi joto ina umuhimu,” amesisitiza Katibu Mkuu, akionya “kuhusu uharibifu wa kudumu kwa miamba ya matumbawe ambayo haiwezi kuishi katika maji yenye joto kupita kiasi, kuyeyuka kwa tabaka kubwa la barafu kunakotishia kubadilisha mwonekano wa pwani na kuwafurusha mamilioni ya watu, pamoja na uwezekano halisi wa baadhi ya mataifa madogo ya visiwa kutoweka chini ya mawimbi ya bahari.”
Akikabiliwa na hali hiyo ya kutishia uwepo wa binadamu, Bwana. Guterres amesema kuwa “jukumu lililo mbele yetu ni kudhibiti kwa ukali kiwango cha kuvuka kikomo hicho, kupunguza muda wake, na kurejesha joto chini ya 1.5°C haraka iwezekanavyo.”
Ingawa amebainisha kwamba “makubaliano yoyote ya amani yanakaribishwa na yataleta afueni inayohitajika sana,” akirejelea kusitishwa kwa mapigano kwa siku 60 ili kuruhusu mazungumzo ya Iran na Marekani yanayoendelea nchini Switzerland, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema mgogoro wa Mashariki ya Kati umeanzisha “mshtuko mkubwa zaidi wa nishati kuwahi kutokea,” mkubwa kuliko usumbufu wa mafuta wa miaka ya 1970 na hata uvamizi kamili wa Ukraine na Russia kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, ingawa vita vya Mashariki ya Kati vimeathiri vibaya mataifa yaliyoendelea kiviwanda, nchi zinazoendelea zimeathirika zaidi, “Ni mshtuko wa madeni. Mshtuko wa chakula. Mshtuko wa maendeleo,” amesema, akiongeza kuwa athari zake “zina uwezekano mkubwa wa kudumu kwa muda mrefu.”
Mustakabali wa haki kupitia nishati jadidifu
“Habari njema ni kwamba tofauti na kila mgogoro wa nishati uliopita sasa tuna njia iliyowazi ya kutoka. Njia safi ya kutoka,” ameendelea kusema.
Amebainisha kuwa tangu mwaka 2010, gharama ya nishati ya jua imeshuka kwa karibu asilimia 90, nishati ya upepo wa nchi kavu kwa zaidi ya asilimia 70, na uhifadhi wa nishati kwenye betri kwa asilimia 95.
Kwa mujibu wa Bwana. Guterres, nishati jadidifu imezuia utoaji wa hewa ukaa unaozidi kiwango cha uzalishaji wa kila mwaka wa Marekani, Muungano wa Ulaya na Japan kwa pamoja.
Aidha, uwekezaji katika nishati safi sasa unavutia karibu mara mbili ya fedha zinazowekezwa katika mafuta ya kisukuku.
“Hakuna vikwazo vya biashara kwa mwanga wa jua, wala hakuna vizuizi kwa upepo,” aamesema.
Hatua saba muhimu
Kama sehemu ya mpango wa Katibu Mkuu wa “kuachana kabisa na mafuta ya kisukuku”, ameeleza hatua saba muhimu:
1. Kupunguza uzalishaji wa gesi chafu
Uzalishaji wa gesi chafu lazima ufikie kiwango cha juu mara moja na kisha ushuke kwa kasi katika muongo huu, huku dunia ikifikia kiwango cha kutozalisha kabisa hewa ukaa ifikapo mwaka 2050.
Kundi la nchi za G20, linalochangia takriban asilimia 80 ya uzalishaji wa gesi chafu duniani, lazima liongoze juhudi hizi. Hatua muhimu ni pamoja na kupunguza utoaji wa gesi ya methane, gesi ambayo ina nguvu mara 80 zaidi kuliko hewa ukaa lakini hudumu angani kwa muda mfupi zaidi.
2. Kuimarisha nishati safi
Miradi ya nishati safi inapaswa kupewa kipaumbele na ruzuku za umma kwa miradi mipya ya mafuta ya kisukuku ziondolewe.
“Kampuni nane kubwa zaidi za mafuta ya kisukuku zilipata faida ya ziada ya dola bilioni 6.5 katika robo ya kwanza ya mwaka huu pekee,” amesema Bwana. Guterres.
3. Kukabiliana na vituo vya data vya AI
Katibu Mkuu amebainisha kuwa vituo vya data vya akili Mnemba (AI) tayari vinatumia umeme mwingi kuliko mataifa mengi.
Amezitaka kampuni zote kubwa za AI kupima na kuweka wazi kwa umma athari kamili za kimazingira za matumizi yao ya hewa ukaa, maji na ardhi, na kujitolea kutumia nishati jadidifu pekee katika vituo vyao vya data ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wake, kufikia mwaka 2030, vituo vya takwimu vya AI vinaweza kutumia maji yanayotosha kukidhi mahitaji ya msingi ya wakazi bilioni 1.3 wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mwaka mzima.
4. Kuhakikisha mpito wa haki
Mpito kuelekea nishati safi lazima uwasaidie wafanyakazi, jamii na nchi zinazoendelea kote duniani, kwa msaada wa mkutano wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa, COP31, utakaofanyika nchini Uturuki.
“Mpito wenyewe hauko tena katika mjadala,” amesema. “Swali ni kama utasimamiwa vizuri au kwa vurugu, kwa haki au kwa ukosefu wa usawa, kama chanzo cha utulivu au mgawanyiko mkubwa zaidi.”
5. Kulinda walio hatarini zaidi
Wale walio katika hatari kubwa kutokana na athari za tabianchi wanapaswa kusaidiwa kuzoea hali mpya kwa sababu hatua hizi “zinaokoa maisha, kulinda makazi na jamii, kusaidia uchumi kustahimili mishtuko na kudumisha mshikamano wa kijamii.”
Amesema mifumo ya tahadhari na maandalizi lazima iwepo kabla mishtuko hiyo haijageuka kuwa majanga ya kibinadamu na kiuchumi.
Aidha, nchi zilizoendelea zinapaswa kutimiza ahadi yao ya kuongeza mara mbili fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, huku zikielekea kuziongeza mara tatu.
6. Fedha za haki kwa mpito unaojali mazingira
Nchi nyingi zinazoendelea hukabiliwa na gharama za kukopa fedha ambazo ni mara mbili hadi tatu zaidi ya zile za mataifa tajiri.
“Nchi zenye uwezo mkubwa wa nishati jadidifu zinaachwa nje ya mapinduzi ya nishati safi,” amesema, akitaja nchi za Afrika ambazo hupokea asilimia mbili tu ya uwekezaji wa dunia katika nishati safi licha ya bara hilo kuwa na asilimia 60 ya rasilimali bora zaidi za nishati ya jua duniani.
Amesisitiza kuwa uwezo wa ziada wa mikopo ya benki za maendeleo za kimataifa, kama Benki ya Dunia, unaokadiriwa kufikia dola bilioni 600 hadi 800, unapaswa kutumiwa kwa nguvu kufadhili miundombinu ya baadaye na hatua za kukabiliana na tabianchi.
Pia amesisitiza kuwa nchi zilizoendelea lazima zitimize ahadi zao, ikiwa ni pamoja na kusaidia Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu pamoja na Mfuko wa Kijani wa Tabianchi, na kuhakikisha dola bilioni 300 zilizoahidiwa kwa nchi zinazoendelea zinatolewa pamoja na hatua za kufanikisha dola trilioni 1.3 kwa mwaka kufikia 2035.
7. Kuamini sayansi na kupambana na taarifa za uongo
Katibu Mkuu ameonya kuwa upotoshaji wa taarifa unasambazwa kwa makusudi ili kuchelewesha hatua za kukabiliana na tabianchi, kulinda maslahi maalum na kudhoofisha imani ya umma.
Amehimiza watetezi wa haki za binadamu na wanahabari wanaoripoti kuhusu tabianchi na mazingira kulindwa, huku akisisitiza “umuhimu wa kuimarisha imani katika ushahidi na taasisi.”
Ametaja pia Mpango wa Kimataifa wa Uadilifu wa Taarifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, unaolenga kusaidia kufanikisha lengo hilo.