Nchini Indonesia, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakishirikiana na Serikali kujenga mfumo wa nishati unaotegemewa zaidi na wenye mnepo mkubwa, huku pia yakisaidia jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kuboresha mtandao wa umeme

Mtandao wa umeme unaotegemewa ni msingi wa uhakika wa nishati. Ili kujiandaa kwa ongezeko la mahitaji ya umeme na kuunganisha nishati zaidi mbadala katika mfumo wa taifa,

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Miradi na Huduma (UNOPS) inashirikiana na kampuni ya umeme inayomilikiwa na serikali, PLN, kutambua zaidi ya gigawati mbili za uwezo wa nishati ya jua zinazoweza kuunganishwa kwenye gridi ya taifa.

Nishati ya jua pamoja na kituo kipya cha udhibiti vitaimarisha uthabiti wa mtandao wa umeme, kupunguza hitilafu za umeme na kupunguza utegemezi wa nishati ya mafuta ya kisukuku.

UN Indonesia Indonesia inaanzisha teknolojia ya kuboresha nguvu za umeme.

Kutumia nishati kwa ufanisi zaidi

Moja ya njia rahisi za kuimarisha uhakika wa nishati ni kupunguza upotevu wa umeme katika mtandao wa usambazaji.

Kwa kushirikiana na washirika wa serikali, UNOPS imeunga mkono ukaguzi wa matumizi ya nishati na mageuzi ya sera za kuongeza ufanisi wa matumizi ya umeme.

Juhudi hizi zinasaidia kaya, biashara na viwanda kutumia umeme kwa ufanisi zaidi, jambo ambalo hupunguza mahitaji ya jumla katika gridi ya taifa na kuhakikisha upatikanaji wa umeme ulio imara na wa gharama nafuu.

Kupunguza matumizi ya nishati viwandani

Sekta ya viwanda nchini Indonesia ni miongoni mwa watumiaji wakubwa zaidi wa nishati, hivyo kuongeza ufanisi katika sekta hii ni jambo muhimu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) linasaidia baadhi ya viwanda vinavyotumia nishati nyingi kupunguza matumizi ya nishati huku vikiongeza uzalishaji.

Katika sekta ya mbolea, hatua za uzalishaji safi na matumizi bora ya rasilimali zinazoungwa mkono na UNIDO zimesaidia kampuni zinazoshiriki kuepuka uzalishaji wa takribani tani 328,000 za hewa ukaa kila mwaka, huku zikipunguza gharama za uendeshaji.

UNIDO pia inashirikiana na Wizara ya Viwanda kuanzisha maeneo ya viwanda rafiki kwa mazingira kwa kuhimiza matumizi bora ya nishati, nishati mbadala, urejelezaji wa maji taka na usimamizi bora wa taka.

Kufungua fursa za ufadhili kwa mpito wa nishati

Indonesia ina malengo makubwa ya nishati, ikiwa ni pamoja na kuongeza karibu gigawati 43 za uwezo wa nishati mbadala ifikapo mwaka 2034.

Kufanikisha lengo hilo kutahitaji uwekezaji wa hadi dola bilioni 188 za Marekani.

© UNDP Vijana wanashiriki katika mafunzo ya wataalamu wa paneli za nishati ya jua huko East Nusa Tenggara, jimbo la kusini kabisa mwa Indonesia.

Ili kuvutia mitaji kwa miradi ya nishati mbadala, Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) linashirikiana na Serikali kuandaa mifumo bunifu ya ufadhili, ikiwemo mbinu za ufadhili mseto zinazounganisha uwekezaji wa umma na wa sekta binafsi.

Kuwasaidia wafanyakazi katika kipindi cha mpito

Kujenga mustakabali salama wa nishati si suala la teknolojia na miundombinu pekee, bali pia linawahusu watu.

Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa ILO linasaidia maeneo mbalimbali nchini Indonesia kujiandaa kwa athari za kijamii na kiuchumi za mpito wa nishati.

Hii inahusisha kutambua fursa mpya za ajira, kuimarisha ujuzi wa wafanyakazi na kulinda wale ambao maisha yao yanaweza kuathiriwa na mabadiliko katika sekta ya nishati.

Kupitia mipango hii, mpito huo unalenga kuimarisha jamii badala ya kuwaacha wafanyakazi nyuma.

Kupeleka nishati safi kwa jamii za pwani

Kwa jamii nyingi za wavuvi katika visiwa vya Indonesia, kupanda kwa gharama za mafuta kunaweza kuhatarisha maisha yao.

UNDP imesaidia zaidi ya wavuvi wadogo 2,400 kutumia teknolojia safi zaidi, ikiwemo injini za boti zinazotumia nishati ya jua, masanduku rafiki kwa mazingira ya kuhifadhia samaki na mifumo bora ya uhifadhi wa baridi.

© UNIC Jakarta Uvuvi ni chanzo kuu cha uchumi na lishe nchini Indonesia.

Ubunifu huu unapunguza matumizi ya mafuta, kupunguza gharama za uendeshaji na kufanya kipato cha wavuvi kisitegemee sana mabadiliko ya bei za nishati.

Wavuvi hao pia wamepewa mafunzo ya kutumia na kutunza vifaa hivyo ili kuhakikisha manufaa yake yanadumu kwa muda mrefu.

Kujenga jamii imara katika maeneo ya mbali

Katika baadhi ya maeneo ya Indonesia, jamii bado ziko mbali na gridi ya taifa ya umeme.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, UNDP imeunga mkono uwekaji wa megawati 1.1 za mifumo midogo ya umeme wa jua katika vijiji 22 vya mbali, na hivyo kutoa umeme wa uhakika kwa zaidi ya kaya 3,400 pamoja na huduma za umma.

Mifumo hiyo imepunguza gharama za nishati kwa hadi asilimia 40 na wakati huo huo kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa takribani tani 1,800 kila mwaka.

Waendeshaji wa mifumo hiyo, karibu nusu yao wakiwa wanawake, wamepewa mafunzo ya kusimamia na kutunza vifaa hivyo ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendelea kwa muda mrefu.

Wakati huo huo, UNOPS imeunga mkono mpango wa Vijiji vya Tabianchi wa Wizara ya Mazingira katika jimbo la South Sumatra, ambapo takribani wakazi 285,000 wamepata mafunzo kuhusu nishati mbadala, teknolojia za uzalishaji mdogo wa hewa chafu na mbinu za uchumi mzunguko.

Kuwainua wanawake kupitia nishati safi

Wanawake wana nafasi muhimu katika mabadiliko ya sekta ya nishati nchini Indonesia.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) yamesaidia zaidi ya wanawake wajasiriamali 400 kupata ufadhili wa kijani na kutumia teknolojia zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi.

© KUMPUL Washiriki wa mafunzo ya kujenga uwezo wakiwa mbele ya mfano wa mashine inayotumia nishati ya jua kukausha huko West Nusa Tenggara.

Teknolojia hizo zinajumuisha mifumo ya kukaushia mazao kwa nishati ya jua, suluhisho za kupikia kwa biogas na pampu za maji zinazotumia nishati ya jua, ambazo hupunguza gharama za nishati na kusaidia shughuli endelevu za kiuchumi.

Kwa kupanua fursa za kiuchumi na kuongeza upatikanaji wa teknolojia safi za nishati, programu hizi zinahakikisha manufaa ya mpito wa nishati yanawafikia watu wengi zaidi.

Kazi ya kipekee

“Kuanzia maboresho ya gridi ya umeme hadi kuongeza ufanisi viwandani, kuanzia kupata ufadhili hadi mifumo ya nishati ya jua inayomilikiwa na jamii, Umoja wa Mataifa unashirikiana na Serikali kuunga mkono kazi yake ya kipekee katika kuimarisha usalama wa nishati nchini,” amesema Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Indonesia, Gita Sabharwal.

Hatua hizi zinapunguza utegemezi wa masoko ya nishati ya kimataifa yenye mabadiliko makubwa ya bei, zinaimarisha uhakika wa upatikanaji wa nishati na kuhakikisha kuwa jamii zote, kuanzia vituo vikubwa vya viwanda hadi vijiji vya mbali, zinachangia kujenga mustakabali wenye ustahimilivu mkubwa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *