Ripoti mpya ya WHO, Kuimarisha uwezo wa uchunguzi, utambuzi na usimamizi wa kasoro za kuzaliwa kwa watoto wachanga, iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inaeleza kuwa uchunguzi wa watoto wachanga ni fursa muhimu ya kuharakisha maendeleo katika kuokoa maisha ya watoto.

Magonjwa na hali nyingi zinaweza kutibiwa kwa mafanikio ikiwa zitagunduliwa mapema baada ya kuzaliwa. Hali hizo ni pamoja na upungufu wa homoni ya tezi ya kuzaliwa), ugonjwa wa selimundu, matatizo ya kusikia (ukiziwi) na baadhi ya matatizo ya kimetaboli. Hata hivyo, mamilioni ya watoto bado hugunduliwa wakiwa wamechelewa au hawapati matibabu kabisa.

Duniani kote, takribani watoto milioni 8 huzaliwa kila mwaka wakiwa na kasoro za kuzaliwa, na hali hizi sasa zinachangia karibu asilimia 8 ya vifo vyote vya watoto walio chini ya miaka mitano, inaeleza WHO na kwamba inakadiriwa kuwa asilimia 90 ya watoto wanaozaliwa na kasoro kubwa za kuzaliwa wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambako huduma za uchunguzi, utambuzi na matibabu bado ni chache.

“Hakuna mtoto anayepaswa kukosa nafasi ya kuwa na maisha yenye afya kwa sababu hali ya kuzaliwa nayo haikugunduliwa mapema vya kutosha,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus. “Nchi mbalimbali duniani zinaonesha kwamba uchunguzi wa watoto wachanga kwa hali moja au zaidi unaweza kuokoa maisha, kuzuia ulemavu na kumpa mtoto mchanga nafasi bora ya kufikia uwezo wake.”

Tofauti kati ya nchi ni kubwa

Baadhi ya nchi huchunguza watoto wote wachanga kwa zaidi ya magonjwa au hali 50, huku nyingine zikiwa hazina uwezo wa kufanya uchunguzi wowote. WHO inahimiza kila nchi kuanza uchunguzi wa watoto wachanga kwa kuanzia hali ya kipaumbele kulingana na mazingira ya nchi husika, na baadaye kupanua huduma hizo kadri uwezo unavyoongezeka.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa kasoro za kuzaliwa zinachangia ongezeko la vifo vya watoto chini ya miaka mitano katika maeneo mengi duniani. Kati ya mwaka 2000 na 2023, kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinavyotokana na kasoro za kuzaliwa kiliongezeka kutoka asilimia 1 hadi 4 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, na kutoka asilimia 3 hadi 11 katika Asia Kusini. Mabadiliko haya kwa kiasi fulani yanaakisi mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya kuambukiza na sababu nyingine zinazoweza kuzuilika.

WHO inalenga kusaidia wizara za afya, hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, kuweka vipaumbele vya magonjwa au hali za kuchunguzwa kwa watoto wachanga kulingana na mazingira ya kila nchi.

Ripoti hiyo pia inaonesha mifano ya mafanikio kutoka nchi mbalimbali:

  • Argentina imeongeza kiwango cha uchunguzi wa watoto wachanga hadi kufikia karibu watoto wote.
  • Brazil imepanua uchunguzi wa kitaifa kwa magonjwa mengi yanayoweza kuhatarisha maisha.
  • Misri imeunganisha uchunguzi wa kusikia na upungufu wa homoni ya tezi kwa watoto wachanga katika huduma za afya ya msingi.
  • India imechunguza zaidi ya watoto milioni 28 katika kipindi cha miaka mitatu na kubaini takribani watoto 900,000 wenye kasoro za kuzaliwa, ambao wameunganishwa na huduma za utambuzi, matibabu na urekebishaji.
  • Ufilipino imepanua mpango wake kutoka hospitali 24 hadi vituo zaidi ya 7,000 vinavyochunguza hali 29 tofauti.
  • Sri Lanka imeunganisha uchunguzi wa watoto wachanga katika huduma za kawaida, ambapo karibu asilimia 80 ya watoto hupimwa hali ya upungufu wa homoni ya tezi.
  • Uganda ina mpango wa serikali wa kutambua mapema watoto wenye ugonjwa wa selimundu katika maeneo yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa huo na kuwapatia matibabu yanayookoa maisha pamoja na ufuatiliaji wa muda mrefu.

WHO sasa inazitaka serikali kuunganisha huduma za uchunguzi, utambuzi na matibabu ya watoto wachanga katika huduma za kawaida za afya na mipango ya huduma za afya kwa wote, kwa kuanza na hali zinazopewa kipaumbele katika kila nchi na ambazo zinaweza kugunduliwa na kutibiwa kwa ufanisi ndani ya mifumo yao ya afya.

Ripoti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mashauriano ya kimataifa yaliyoandaliwa na WHO, yaliyowaleta pamoja wawakilishi wa serikali, wataalamu wa kiufundi, madaktari, watafiti, vyama vya kitaaluma, mashirika ya kiraia na familia zilizoathiriwa na kasoro za kuzaliwa ili kubaini vipaumbele vya kuimarisha uchunguzi wa watoto wachanga, utambuzi na huduma za muda mrefu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *