Mlipuko huo uligunduliwa mwezi Mei 2024 baada ya virusi vya polio vinavyotokana na aina ya pili (cVDPV2) kubainika katika sampuli ya majitaka iliyochukuliwa mjini Mbale.

Ingawa hakukuwa na wagonjwa waliokuwa wameripotiwa, Wizara ya Afya ilitangaza mlipuko ndani ya siku tano na kuanzisha operesheni ya dharura.

Kukimbizana na muda

Kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la afya WHO, la Kuhudumia Watoto UNICEF, Shirika la Kimataifa la bahati naibuRotary International na Wakfu wa Bill na Melinda Gates, Uganda ilianzisha uchunguzi wa haraka na kutathmini hatari ya maambukizi katika maeneo yaliyoathirika.

Tathmini imebaini viwango vya chini vya chanjo kwa baadhi ya watoto, mapungufu katika ufuatiliaji wa ugonjwa na mazingira yaliyoongeza hatari ya kusambaa kwa virusi.

© UNICEF/Henry Bongyereirwe Chanjo zinasafirishwa nchini Uganda kwa kutumia boti, piki piki au kutembea.

Kampeni ya kitaifa ya chanjo

Mwezi Oktoba na Novemba 2024, Uganda ilitekeleza awamu mbili za kampeni za chanjo ya polio aina ya nOPV2 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Kampeni hizo zilifanikiwa kuwafikia zaidi ya watoto milioni 5.9, huku wahudumu wa afya wakitembea nyumba kwa nyumba kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Wakati wa kampeni hizo, wahudumu wa afya waligundua pia wagonjwa wa surua katika baadhi ya maeneo. Mamlaka zilijumuisha chanjo za surua katika hatua hizo ili kuimarisha ulinzi wa afya ya watoto.

Matokeo yaliyoonekana

Ndani ya miezi michache, hakuna ushahidi wa maambukizi endelevu ya polio uliobainika. Mfumo wa ufuatiliaji uliimarika, viwango vya chanjo viliongezeka na huduma za afya zikaboreshwa.

Mwezi Mei 2026, tathmini huru ilithibitisha kuwa Uganda ilikuwa imetimiza vigezo vyote vya WHO vya kutangaza mwisho wa mlipuko huo.

Mafanikio ya Uganda yanaonesha umuhimu wa mifumo ya ufuatiliaji wa mapema, kampeni za chanjo na ushirikiano wa wadau katika kuzuia milipuko ya magonjwa kabla haijasababisha madhara makubwa kwa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *