
Dar es Salaam. Serikali imetangaza barabara nne za kimkakati inazotarajia kuzitekeleza kwa Ubia wa Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), huku wadau wakiitabiri hatua hiyo itakuwa muarobaini wa changamoto ya miundombinu nchini.
Kwa mujibu wa wadau hao, utekelezwaji wa miradi hiyo kwa PPP kutasaidia kuondokana na foleni inayosababisha magari yakiwemo mabasi na malori kukaa muda mrefu katika barabara mbalimbali nchini ikiwemo ya Morogoro
Miradi iliyotangzwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kutekelezwa kwa PPP ni barabara ya Morogoro hadi Dodoma yenye urefu wa kilomita 260 itakayojengwa kwa njia nne.
“Barabara hii ya Morogoro kwenda Dodoma, ni ya kimkakati kwa sababu ndiyo inaunganisha Mji Mkuu wa Kibiashara (Dar es Salaam) na Mji Mkuu wa Tanzania (Dodoma), ni njia yenye magari mengi,” amesema Ulega.
Waziri Ulega ameliambia Bunge kuwa barabara nyingine iliyowekwa kwenye mpango huo wa Serikali ni ile ya Chalinze – Segera – Tanga ambayo ni muhimu kwa kuunganisha ushoroba wa Kaskazini na bandari ya Tanga.
Mbali na hilo, Ulega amesema barabara nyingine ni ile ya haraka ‘expressway’ kutoka Bandari ya Dar hadi Kibaha kilomita 42 yenye lengo la kupunguza msongamano wa malori barabarani.
Waziri Ulega amesema zingine ni Handeni – Kiberashi – Chemba – Kwamtoro- Singida yenye urefu wa kilomita 384 itakayounganisha Bandari ya Tanga na mikoa isiyo na bandari ya Tanzania.
“Barabara nyingine ya kimkakati iliyo kwenye kundi hili ni ile ya mchepuko ya eneo la Mkina Kitonga mkoani Iringa. Itakuwa na urefu wa kilomita 27 ili kurahisisha usafiri na kupunguza ajali kwenye eneo hilo maarufu,”
“Wasafiri wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam watanufaika pia na ujenzi wa barabara ya haraka ya kilomita kuunganisha sehemu hizo.” amesema
Kwa mujibu wa Ulega, tayari Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), imeshatoa tangazo ikikaribisha wabia hao kupitia PPP.
“Naomba kuliambia Bunge lako tukufu kwamba mpango wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchi na kuona hakuna anayeachwa nyuma unaendelea,”
“Juni 19, 2026 tumetoa matangazo rasmi katika vyombo vya habari likiwemo Daily News kukaribisha wabia ili tuanze sasa kujenga barabara hizi,” amesema Ulega.
Wadau wanena…
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa) Issa John amesema ujenzi wa barabara hizo ukianza kutakuwa na foleni lakini ya muda, ingawa manufaa yake kutakuwa na suluhisho la kudumu la changamoto za miundombinu.
“Tutapata wakati mgumu utakaokuwa na manufaa mbeleni, kuliko hivi sasa tunakaa foleni hatujui kinachoendelea. Ujenzi wa barabara hizo utakuwa suluhu la kudumu ya foleni,” amesema John.
John amesema mojawapo ya barabara itakayokuwa na manufaa ni ile ya Kitonga akisema hivi sasa imekuwa kero isiyoelezeka hasa inapotokea lori au basi limepata hitilafu.
“Nyingine ni Uwanja wa Ndege hadi Katikati ya Jiji na kutoka Mjini hadi Kibaha. Hizi kero yake kubwa zaidi lakini zikijengwa zitaleta ahueni kuwa watumiaji,” amesema John.
John ametoa angalizo kuhusu tozo zitakazowekwa baada ya miradi hiyo kukamilika, akisema zisiwe za kuumiza wananchi na wamiliki wa vyombo vya moto.
“Hatuna budi kuzipokea tozo lakini angalizo, ziwekwe ziwe na mazingira rafiki si kutuumiza,” ameeleza.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John amesema hatua nzuri ya ujenzi wa barabara hizo zitakazopungua foleni katika maeneo mbalimbali.
“Kitu ambacho nina wasiwasi ni hawa watu binafsi kuhusu tozo zisiwe za tofauti na kusababisha barabara ziwe gharama kutumika. Barabara hizi zikijengwa zitafungua njia itakayookoa muda na gharama za uendeshaji,” amesema.
“Mafuta mengi yanatumika njiani kwa sababu ya ubovu wa miundombinu unaosababisha ajali nyingi pia.Kwa ujumla nchi itafunguka, mfano barabara ya Kiberashi-Singida hadi Kwa mtoro itarasisha usafiri,” amesema John.
Mbali na hilo, John amesema hata huo ukanda utakaojengwa barabara hiyo kuna shughuli nyingi za kiuchumi za kilimo ambazo zitainuka, akisisitiza kusiwe na gharama za ziada zitakazowaumiza watumiaji.
PPP wapongeza
Mkurugenzi Mtendaji wa PPP Centre, David Kafulila amepongeza hatua ya Tanroads kutangaza fursa hizo kwa uwazi ndani na nje ya nchi, akisema itawawezesha wawekezaji wakubwa kushiriki kwa ushindani wa haki.
Mbali hilo, Kafulila amesema hatua itasaidia Watanzania kupata nafasi ya kufuatilia maendeleo ya miradi hiyo muhimu.