Hata hivyo, maafisa wa afya wanasema kuna dalili za matumaini baada ya wagonjwa 100 kupona ugonjwa huo.

WHO inasema idadi hiyo inaonesha kuwa Ebola inaweza kudhibitiwa na kutibiwa iwapo wagonjwa watapata huduma za afya kwa wakati.

Juhudi za kukabiliana na mlipuko zaimarishwa

Katika mwezi uliopita, WHO, Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC), pamoja na washirika wengine, wameisaidia Wizara ya Afya ya DRC kuongeza idadi ya vituo vya matibabu ya Ebola, kuimarisha uwezo wa maabara na ufuatiliaji wa ugonjwa, na kutoa mafunzo kwa wahudumu zaidi wa afya kuhusu huduma za kliniki na hatua za kuzuia maambukizi.

Mashirika ya afya pia yameongeza juhudi za kuelimisha na kushirikisha jamii ili kuboresha uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya Ebola.

Maafisa wa WHO wanasema timu za kijamii zina mchango mkubwa katika kubaini wagonjwa mapema, kusaidia familia zilizoathirika na kuzuia kuenea kwa maambukizi.

© WFP/Arete/Seros Muyisa Mfanyakazi wa UN akiua vijidudu kwenye godoro la ndege katika Uwanja wa Ndege wa Bunia, kama sehemu ya kukabiliana na mlipuko wa Ebola katika Mkoa wa Ituri, DR Congo.

Bado mengi yanahitajika

Licha ya hatua zilizopigwa, WHO imeonya kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa rasilimali.

“Bado tunahitaji vituo zaidi vya matibabu, wahudumu zaidi wa afya, vipimo zaidi na timu zaidi kutoka ndani ya jamii kusaidia jamii zao,” shirika hilo limesema.

Maafisa wa afya wameongeza kuwa ufikiaji salama na endelevu wa maeneo yaliyoathirika ni muhimu ili kufikia watu wote wanaohitaji msaada.

WHO imetoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mlipuko huo.

Shirika hilo limesisitiza kuwa kumaliza mlipuko wa Ebola kutahitaji mshikamano wa kimataifa pamoja na mazingira ya amani.

“Tunahitaji mshikamano endelevu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ili kukomesha mlipuko huu. Na hatimaye, tunahitaji amani kwa watu wa DRC,” imesema WHO.

Maafisa wanaeleza kuwa amani ya kudumu itawawezesha wahudumu wa afya kuwafikia kwa usalama wananchi wote walioathirika na hivyo kusaidia kumaliza mlipuko huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *