Londoni. Siasa za Uingereza zimeingia katika kipindi kipya cha sintofahamu na mabadiliko makubwa baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Keir Starmer, huku Andy Burnham akijitokeza kama mrithi anayetarajiwa kuiongoza nchi bila kupitia uchaguzi mkuu mpya.

Katika hali inayozua mjadala wa kisiasa, Burnham anaweza kuingia rasmi katika makazi ya Waziri Mkuu ya namba 10 Downing Street ndani ya wiki chache zijazo ikiwa hatapata mpinzani katika kinyang’anyiro cha uongozi wa Chama cha Labour.

Kujiuzulu kwa Starmer kunahitimisha safari ya kisiasa iliyokuwa imeanza kwa matumaini makubwa baada ya ushindi wa kihistoria wa Labour katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.

Lakini ndani ya kipindi kisichofikia miaka miwili, umaarufu wa Serikali yake ulianza kuporomoka kutokana na changamoto za kiuchumi, migawanyiko ya ndani ya chama na matokeo mabaya ya uchaguzi wa serikali za mitaa.

Akizungumza wakati wa kutangaza kuondoka kwake, Starmer alisema amesikiliza sauti za wabunge wa chama chake waliokuwa wakijiuliza nani angefaa kuiongoza Labour kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

“Nimesikia hoja ya chama changu na wabunge kuhusu swali hilo, na nalikubali kwa moyo mkunjufu,” alisema.

Lakini nyuma ya pazia, taarifa kutoka ndani ya Labour zinaonyesha kuwa hali haikuwa tulivu kama ilivyoonekana hadharani.

Vyanzo vya kisiasa vinasema Starmer alikuwa amekasirishwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama waliomtaka kuweka wazi ratiba ya kuondoka kwake, huku baadhi ya washauri wake wakihofia kuwa mzozo huo ungeweza kuigawa Serikali.

Burnham apokelewa kishujaa Westminster

Wakati Starmer akiondoka katika mazingira ya huzuni, Burnham aliwasili Westminster katika mazingira tofauti kabisa.

Mbunge huyo mpya wa Makerfield na aliyekuwa Meya wa Greater Manchester alipokelewa kwa shangwe kubwa kutoka kwa wabunge wa Labour walioonekana kumuona kama tumaini jipya la chama hicho.

Katika korido za Bunge la Uingereza, wabunge walijazana kumlaki, kumpa mkono na kupiga picha naye huku wengine wakianza kutabiri nafasi watakazoweza kupata katika serikali mpya.

Lakini katikati ya shamrashamra hizo, mbunge mmoja wa Conservative alisikika akiwakejeli wabunge wa Labour kwa kusema: “Yeye si Masihi.”

Kauli hiyo ilionyesha namna ambavyo wapinzani wa Burnham wanavyopinga taswira ya kiongozi huyo kuonekana kama mwokozi wa kisiasa wa Labour.

Swali kubwa: Burnham ana mamlaka gani?

Mjadala mkubwa unaotikisa siasa za Uingereza kwa sasa ni iwapo Burnham anapaswa kupewa nafasi ya kuwa Waziri Mkuu bila kuitisha uchaguzi mkuu mpya.

Wakosoaji wake wanaeleza kuwa Burnham hakuwahi kuwa sehemu ya kampeni ya Labour iliyoshinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2024 na kwamba wapigakura hawakumpigia kura moja kwa moja kuwa Waziri Mkuu.

Hoja hiyo imepewa nguvu zaidi na ukweli kwamba Burnham alirejea bungeni hivi karibuni baada ya kushinda uchaguzi mdogo katika jimbo la Makerfield.

Kwa msingi huo, viongozi wa upinzani wanahoji kama ni sahihi kwa mtu aliyeungwa mkono na wapiga kura katika jimbo moja kupewa mamlaka ya kuongoza taifa lenye mamilioni ya wananchi.

Farage, Conservatives wataka uchaguzi mkuu

Kiongozi wa Reform UK, Nigel Farage, ameongoza mashambulizi dhidi ya mpango wa Burnham kuingia madarakani bila uchaguzi mpya.

Farage alisema ni jambo lisilo na mantiki kwa Labour kudhani inaweza kubadilisha Waziri Mkuu bila kuwapa wananchi nafasi ya kutoa uamuzi wao.

Kwa upande wake, kiongozi wa Conservative, Kemi Badenoch, ameonya kuwa kubadilisha kiongozi pekee hakutatosha kuondoa matatizo yanayoikabili Serikali.

Alisema Uingereza inakabiliwa na changamoto kubwa za usalama wa taifa, uchumi na uhamiaji na kwamba wananchi wanastahili kupata nafasi ya kuamua ni nani anapaswa kuongoza nchi.

Wes Streeting aondoa ushindani

Njia ya Burnham kuelekea uongozi imeonekana kuwa nyepesi zaidi baada ya aliyekuwa Waziri wa Afya, Wes Streeting, kuamua kumuunga mkono badala ya kuingia katika ushindani.

Hatua hiyo imepunguza uwezekano wa kuwapo kwa uchaguzi mkali ndani ya Labour na imeongeza nafasi ya Burnham kutwaa uongozi bila kupingwa.

Streeting alisema chama hicho hakipaswi kutumia miezi kadhaa katika mapambano ya ndani wakati nchi inahitaji mwelekeo mpya wa kisiasa.

Kwa kufanya hivyo, Burnham sasa anaonekana kuwa mgombea mwenye nguvu zaidi wa kuiongoza Labour na Serikali.

Changamoto kubwa

Licha ya mapokezi makubwa anayopata sasa, kazi inayomsubiri Burnham si ndogo.

Atalazimika kurejesha imani ya wapigakura waliokata tamaa baada ya kuondoka kwa Starmer.

Pia, atalazimika kukabiliana na ukuaji wa haraka wa chama kipya cha Reform UK ambao walijiengua kutoka Labour, chama ambacho kimevutia wapigakura wengi kwa hoja za uhamiaji, usalama wa mipaka na gharama za maisha.

Ndani ya Labour yenyewe, Burnham atahitaji kuunganisha makundi tofauti yaliyokuwa yakivutana wakati wa utawala wa Starmer.

Aidha, atalazimika kuonyesha kuwa ana timu ya viongozi wenye uwezo wa kuendesha Serikali pamoja na mpango wa wazi wa kukabiliana na changamoto za uchumi, afya na huduma za umma.

Wasifu wa Andy Burnham

Andy Burnham ni mwanasiasa wa Uingereza ambaye ni Mbunge wa jimbo la Makerfield.

Baada ya kuhudumu kwa mafanikio kama Meya wa Greater Manchester kuanzia mwaka 2017 hadi 2026, alirejea katika siasa za kitaifa na kujitokeza kama mmoja wa wagombea wakuu wa kuwania uongozi wa Chama cha Labour kufuatia kujiuzulu kwa Keir Starmer.

Maisha na Elimu

Burnham alizaliwa Januari 7, 1970 katika eneo la Aintree, Liverpool, na kukulia Culcheth, Cheshire nchini Uingereza. Anatoka katika familia ya kawaida ya wafanyakazi, jambo ambalo limekuwa sehemu muhimu ya utambulisho wake wa kisiasa.

Akiwa kijana, alivutiwa na masuala ya kijamii na kisiasa baada ya kutazama tamthilia maarufu ya BBC, Boys from the Blackstuff, iliyozungumzia maisha na changamoto za tabaka la wafanyakazi nchini Uingereza. Ushawishi huo ulimfanya ajiunge na Chama cha Labour akiwa na umri wa miaka 14.

Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi na sekondari, Burnham alijiunga na Chuo cha Fitzwilliam katika Chuo Kikuu cha Cambridge, ambako alisomea lugha na fasihi ya Kiingereza.

Safari ya siasa

Kabla ya kuingia rasmi katika siasa, Burnham alifanya kazi kwa muda mfupi kama mwandishi wa habari na mtafiti wa kisiasa.

Mwaka 2001 alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Leigh, hatua iliyomfungulia milango ya kupanda ngazi za uongozi ndani ya Chama cha Labour.

Katika serikali za mawaziri wakuu Tony Blair na Gordon Brown, Burnham alipewa majukumu mbalimbali muhimu serikalini, yakiwemo:

Mkuu wa Hazina Msaidizi kuanzia mwaka 2007 hadi 2008.

Waziri wa Utamaduni, Vyombo vya Habari na Michezo kuanzia mwaka 2008 hadi 2009. Waziri wa Afya kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.

Umahiri wake katika nafasi hizo ulimfanya kuwa mmoja wa wanasiasa vijana waliokuwa wakitajwa kuwa viongozi wa baadaye wa Labour.

Imeandikwa na Noor Shija, kwa msaada wa mtandao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *