Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka 2025 kulithibitishwa ukiukwaji mkubwa wa matukio 38,558 dhidi ya watoto, ukiwaathiri watoto 24,174. 

Ukiukwaji huo ulijumuisha mauaji, majeraha mabaya, utekaji nyara, unyanyasaji wa kingono, kuandikishwa vitani na kunyimwa misaada ya kibinadamu.

Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 30 ya ufuatiliaji wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi wa serikali na vikosi vinavyoungwa mkono na serikali walihusika katika ukiukwaji mkubwa zaidi dhidi ya watoto kuliko makundi ya waasi au makundi mengine yasiyo ya kiserikali.

Kutochukua hatua ni uchaguzi wa kisiasa

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Silaha, Vanessa Frazier, akizungumza katika mkutano huo wa Baraza la Usalama amesema dunia haiwezi tena kudai kuwa haikujua mateso wanayopitia watoto katika maeneo ya vita.

“Baada ya miongo kadhaa ya ushahidi, maonyo na wito wa kuchukua hatua, jumuiya ya kimataifa haiwezi kudai kutofahamu kinachowatokea watoto katika migogoro ya silaha,” amesema.

Ameonya kuwa iwapo dunia bado haijashtushwa na mateso ya mamilioni ya watoto, basi inapaswa kukabiliana na ukweli mwingine wa kusikitisha zaidi.

“Kutochukua hatua hakusababishwi na kutofahamu. Ni uchaguzi wa kisiasa unaofanywa kwa makusudi,” amesema, akisisitiza kuwa gharama ya uchaguzi huo hupimwa kila siku katika maisha ya watoto.

Frazier amesema ripoti ya Katibu Mkuu inapaswa kutikisa dhamiri za wajumbe wa Baraza la Usalama, nchi wanachama na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.

“Hii ni hati ya mashtaka dhidi ya kutochukua hatua, na ni wito wa kutumia zana ambazo tayari tunazo ili kuwalinda watoto,” ameongeza.

Shule si viwanja vya vita: Catherine Russell

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Catherine Russell,amewaambia wajumbe wa Baraza hali halisi inayowakabili watoto katika maeneo ya migogoro ni ya kutisha.

“Shule, hospitali au chanzo cha maji havipaswi kuwa viwanja vya vita,” amesema.

Hata hivyo, amesema huo ndio uhalisia wa kila siku kwa mamilioni ya watoto wanaoishi katika maeneo yenye migogoro.

Russell amesema nyuma ya takwimu hizo kuna watoto waliouawa, kujeruhiwa, kutekwa nyara, kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha, kufanyiwa ukatili wa kingono, kunyimwa elimu, huduma za afya na misaada ya kibinadamu.

Ameeleza kuwa ukiukwaji mwingi zaidi haukuripotiwa kutokana na ukosefu wa usalama, hofu ya kulipiziwa kisasi na ugumu wa kurekodi matukio katika maeneo ya vita.

“Takwimu hizi zinaonesha kuwa ulinzi wa watoto unaotolewa chini ya sheria za kimataifa unakiukwa mara nyingi zaidi na kwa gharama kubwa zaidi,” amesema.

Amesema matokeo ya ripoti yanapaswa kuwatia wasiwasi wajumbe wote wa Baraza la Usalama, hasa ikizingatiwa kuwa vikosi vya serikali sasa vinatajwa kuhusika zaidi katika ukiukwaji huo kuliko makundi yasiyo ya kiserikali.

Watoto waachwe wakue kwa amani

Russell amezitaka nchi wanachama kutumia ushawishi wao kuhakikisha pande zote zinazohusika katika migogoro zinaheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.

“Hakuna mtu anayeweza kudai kutofahamu athari za vita kwa watoto,” amesema.

Amesisitiza kuwa watoto wanaohusishwa na vikosi vya kijeshi wanapaswa kutambuliwa kwanza kama waathirika badala ya wahalifu, huku akitaka uwajibikaji kwa wote wanaohusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.

Aidha, amelaani ongezeko la mashambulizi dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu na kuzuiwa kwa misaada kuwafikia wahitaji, akisema hali hiyo inahitaji hatua za haraka kutoka Baraza la Usalama.

“Watoto hawaanzishi vita, na hawana uwezo wa kuvisimamisha,” amesema Bi. Russell. “Tunawadai dunia ambayo vita ni jambo la wapiganaji, na watoto wanakuwa huru kukua, kujifunza na kuota ndoto zao kwa amani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *