- Familia ya Mbungu iko katika maombolezo kufuatia kifo cha binti yao na dada yao, Ann, aliyepoteza maisha kwa njia ya kusikitisha baada ya kuagiza teksi, huku maswali mengi yakisalia kuhusu mazingira ya kifo chake na kile kinachoonekana kuwa uzembe kutoka kwa mamlaka husika
- Kaka mwenye huzuni, Timothy, anatafuta haki kwa dada yake Ann, aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha, huku mwili wake ukipatikana ukiwa umetupwa kando ya barabara
- Maswali yameibuka kuhusu tofauti ya njia aliyopitia akiwa kwenye teksi na namna polisi walivyoshughulikia tukio hilo baada ya Ann kufariki katika ajali ya kugongwa na gari lililotoroka, huku maandalizi ya mazishi yake yakiendelea
Nairobi, Kenya: Familia moja imetumbukia katika majonzi kufuatia kifo cha binti yao, Annah, ambaye mara ya mwisho alionekana akiita teksi ili kurejea nyumbani kutoka kazini kabla ya kutoweka.

Akizungumza na TUKO.co.ke, kakake Timothy Mbungu alisema kuwa Ann aliagiza teksi iliyomchukua majira ya saa 3:20 usiku, lakini mwili wake ulikusanywa na polisi saa 3:36 usiku katika eneo lililokuwa mbali na alikokuwa anakwenda.
“Baadaye polisi walidai kuwa walipeleka mwili huo katika mochari ya City Mortuary saa 4:40 asubuhi. Ninakuomboleza dada yangu mdogo; kaka yako mkubwa hakuwepo kukulinda. Sikuwahi kujua ulikuwa na maadui wakubwa kiasi hicho. Dada yangu, niliona ulivyopitia maumivu makubwa… kosa lako pekee lilikuwa kuomba huduma kutoka kwa mtoa huduma uliyekuwa unamwamini, Bolt,” alisema.
“Uliomba teksi lakini hukuwahi kufika ulipokuwa unakusudia kwenda… kwa kampuni, wewe ni takwimu tu; walikuacha ukiwa huna uhai kando ya barabara na wakaendelea na shughuli zao kana kwamba hakuna kilichotokea. Kesho nitauliza maswali kwa ajili ya usalama wa wanafamilia wangu wengine; je, tuko salama?” alihoji.
Timothy Mbungu amekumbana na changamoto gani?
Timothy pia aliishutumu serikali kwa kuchelewa kuchukua hatua.
“Kwa baadhi ya watu yeye ni habari za kawaida tu; kwa wengine ni mwili unaopaswa kuondolewa haraka iwezekanavyo. Lakini kwangu alikuwa dada yangu.”
“Huenda mimi ni dhaifu mno kutafuta haki katika mfumo mgumu kama huu, lakini nitafanya kila niwezalo… lakini Ann, lazima nipate majibu. Bado nakupenda dada yangu mdogo… nakupenda sana kiasi kwamba siwezi kukuachia bila kujua ukweli,” alisema.
Hadi sasa, Timothy anataka kujua kwa nini teksi ilipitia njia tofauti na ile iliyotarajiwa, jinsi ilivyowezekana kwamba baada ya kusafiri kwenye teksi ndogo, dada yake alipatikana katikati ya barabara akiwa amegongwa na gari lililotoroka bila kuwa na mashahidi wa tukio hilo, ikiwemo dereva wa teksi.
Pia anataka kufahamu kwa nini polisi walipofika eneo la tukio hawakuchukua hatua za kutafuta taarifa ambazo zingeweza kusaidia kutatua kitendawili hicho.
“Iliripotiwa kuwa kufikia siku iliyofuata, dereva wa teksi husika alikuwa akiendelea na kazi yake kana kwamba hakuna kilichotokea. Ni baada ya kushinikizwa na watu wenye nia njema ndipo polisi walimwita dereva huyo katika Kituo cha Polisi cha Embakasi na gari lake kuzuiliwa. Maswali ni mengi lakini hakuna majibu,” alilalamika Timothy.
“Leo, Jumatano, ni siku ya mwisho ya mikutano yetu katika Hoteli ya Blue Springs. Tafadhali ungana nami tunapokamilisha maandalizi ya kumpa Ann safari ya mwisho inayomstahili Jumamosi hii. Blue Springs kuanzia saa 12 jioni… hapo ndipo mahali pa kuwa,” aliongeza.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke

