Golikipa mkongwe wa Cape Verde, Vozinha bado anaendelea kutamba kwenye mtandao wa Instagram ambapo hadi sasa amefikisha idadi ya wafuasi milioni 15.8 katika mtandao huo akiingia kwenye orodha ya makipa watano wenye wafuasi wengi zaidi duniani.
Vozinha sasa anaungana na makipa wengine wanne kukamilisha idadi ya walinda milango watano wenye idadi kubwa ya wafuasi duniani katika mtandao wa Instagram.
Nafasi ya kwanza hadi ya tatu zinashikwa na makipa wa watatu ambao wameichezea Real Madrid kwa nyakati tofauti ambapo nafasi ya kwanza yupo kipa wa zamani wa timu hiyo, Iker Casillas mwenye wafuasi milioni 20.4, nafasi ya pili inashikiliwa na Keylor Navas ambaye sasa anacheza Klabu ya Pumas UNAM ya Mexico mwenye wafuasi milioni 19.1, huku nafasi ya tatu ikishikwa na kipa wa sasa wa Real Madrid, Thibaut Courtois mwenye idadi ya wafuasi milioni 17.9.
Nafasi ya nne yupo kipa wa Barcelona, Marc-André ter Stegen mwenye idadi ya wafuasi milioni 16.8 akifuatiwa na Vozinha ambaye anaendelea kufuatiliwa akifikisha idadi ya wafuasi milioni 15.8.
Kipa huyo ameingia kwenye chati hiyo baada ya kumpita kipa wa zamani wa Man United, David de Gea mwenye idadi ya wafuasi milioni 15.1.
Vozinha alianza kufuatiliwa na mashabiki wengi wa soka baada ya kuonyesha kiwango bora katika mechi dhidi ya Hispania ambayo ilikuwa ya kwanza katika kundi H la Kombe la Dunia 2026.
Kipa wa Cape Verde, Josimar José Évora Dias ‘Vozinha’ wakati alipokuwa akiokoa moja ya mchomo hatari kwenye mechi dhidi ya Hispania. Picha na Mtandao
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Atlanta huko Marekani, ulimalizika kwa suluhu baada ya kipa huyo kuonyesha makali yake akiokoa michomo hatari saba iliyopigwa kwenye lango lake.
Vozinha anayecheza Chaves inayoshiriki Ligi daraja la kwanza Ureno, umaarufu wake uliongezeka zaidi kutokana na kampeni kubwa ya mtandaoni iliyofanywa na wachambuzi wa soka kupitia kituo cha televisheni ya CazéTV kutoka Brazil baada ya kuvutiwa na kiwango chake ambapo waliwaomba watazamaji kumfuata kipa huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram ili kumpongeza kwa kile alichokifanya.
Hata hivyo, mafanikio hayo ya mtandaoni yameacha mjadala mkubwa kwa mashabiki wa soka baada ya Vozinha kuanza kuwapita kwa kasi baadhi ya mastaa wakubwa wanaocheza ligi za Ulaya.
Kipa wa Cape Verde, Josimar José Évora Dias ‘Vozinha’. Picha na Mtandao
Wachezaji kama Bukayo Saka wa Arsenal mwenye idadi ya wafuasi milioni 8.1, Declan Rice yeye anao milioni 6.5 wakati nahodha wao Martin Ødegaard akiwa na wafuasi milioni 7.2 wamejikuta wakipitwa kwa kasi na Vozinha.
Hali hiyo hiyo imewakuta nyota wa Manchester United na Chelsea, akiwemo Bruno Fernandes mwenye wafuasi milioni 11.3 wakati Cole Palmer akiwa nao milioni 8.5.
Cape Verde itashuka dimbani katika mechi ya mwisho ya kundi H ambapo itakabiliana na Saudi Arabia, Juni 27 mwaka huu katika Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea huko Marekani, Canada na Mexico.