
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesisitiza kuwa Tehran haitawahi kamwe kufanya mazungumzo yoyote kuhusu uwezo wake wa ulinzi na kuzuia uchokozi (deterrence), akibainisha kuwa ghala la makombora la nchi hii ndilo limeiweka Iran salama dhidi ya kukumbwa na hatima ya Gaza.
Ametoa kauli hiyo Jumanne akiwa ziarani nchini Pakistan, Rais Pezeshkian alikataa katakata wazo lolote la kujadili kupunguza uwezo wa kijeshi wa Iran, akisisitiza kuwa nguvu za ulinzi wa Iran ni muhimili wa kulinda mamlaka ya nchi dhidi ya vitisho vya nje.
Akizungumza kando ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Islamabad, Rais Pezeshkian amezikosoa nchi za Magharibi ambazo hujinadi kama watetezi wa haki za binadamu na kusema madai hayo hayaendani na vitendo vya nchi hizo.
Ziara hiyo ya siku moja ya Rais Pezeshkian ilihusisha mazungumzo ya kina na Waziri Mkuu Sharif, Rais Asif Ali Zardari, na Mkuu wa Majeshi ya Pakistan, Field Marshal Asim Munir.
Akimtanguliza Mungu na kuanza kwa beti za mshairi mashuhuri Muhammad Iqbal, Rais Pezeshkian amesema uhusiano wa Tehran na Islamabad umejengeka katika msingi wa heshima ya pande zote.
Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran inaamini kuwa amani, utulivu, na ustawi katika eneo la Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi vinaweza kupatikana tu kupitia mazungumzo ya dhati, ushirikiano wa kikanda, na mahusiano yanayozingatia heshima ya pande zote.
Ikumbukwe kuwa Pakistan ilichukua nafasi kubwa katika kuwezesha Mkataba wa Maelewano (MoU) kati ya Iran na Marekani. Mapatano hayo ya hivi karibuni yalifikiwa baada ya vita vya siku 40 vilivyoanzisha na Marekani na Israel dhidi ya Iran mnamo Februari 28.
Waziri Mkuu Sharif na Field Marshal Asim Munir walisaidia kama wapatanishi katika mazungumzo hayo, ambayo yaliandaa njia ya kusitishwa kwa vita vya kichokozi dhidi ya Iran na kufungua mlango wa majadiliano ya baadaye kuhusu kuondolewa kwa vikwazo na usalama wa kikanda.
Rais wa Iran ametoa wito wa ushirikiano wa karibu zaidi miongoni mwa nchi za Kiislamu, akisema Iran imenyoosha “mkono wa urafiki” kwa nchi za kanda hii katika harakati za kutafuta mfumo mpya wa usalama. Amezitaja Qatar, Saudi Arabia, Misri, na Uturuki kama nchi zinazoweza kuwa na mchango wenye matokeo katika kuunda mfumo huo.
Rais Pezeshkian pia ametoa shukrani kwa uongozi na wananchi wa Pakistan kwa uungaji mkono wao kwa Iran wakati wa vita vya hivi karibuni.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amesema mazungumzo yake na Rais wa Iran ni “yenye tija kubwa na yamefanyika katika mazingira ya kirafiki sana.
Sharif ameitaja ziara hiyo kama “tukio la kihistoria kati ya Pakistan na Iran” huku akiunga mkono hatua ya kumalizikka vita kati ya Iran na Marekani chini ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad. Waziri Mkuu huyo amepongeza jukumu la Pakistan kama “msuluhishi mwaminifu na mwenye nia njema” na amewashukuru viongozi wa Iran kwa kuamini juhudi za Islamabad.
Katika mikutano yake tofauti na Field Marshal Asim Munir na Rais Asif Ali Zardari, Rais Pezeshkian alijadili njia za kupanua ushirikiano wa kimkakati na kuimarisha uhusiano wa nchi mbili hizo.
Rais Zardari alisisitiza tena uungaji mkono wa Pakistan kwa amani, utulivu, mamlaka ya kitaifa, na ukamilifu wa ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Vilevile, Zardari alitoa salamu za rambirambi kwa ajili ya kufa shahidi kwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei. Amebainisha kuwa maafisa wa Pakistan watashiriki katika mazishi ya kiongozi huyo shahidi, yaliyopangwa kufanyika Julai 4–5.