Watafiti kutoka taasisi tano za kisayansi na kitiba nchini Iran wamefanikiwa kubuni chanjo ya aina yake ya mRNA kwa kutumia njia za hali ya juu za kompyuta.

Chanjo hii ambayo bado iko katika majaribi itakuwa na uwezo wa kuzuia ukuaji na kusambaa kwa uvimbe wa saratani ya matiti.

Saratani ya matiti inasalia kuwa moja ya changamoto kubwa zaidi za kiafya duniani. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 670,000 ulimwenguni mnamo mwaka 2022, na ndiyo saratani inayotambuliwa zaidi miongoni mwa wanawake katika nchi 157.

Ingawa matibabu ya kawaida kama vile kemikali (chemotherapy), mionzi, na upasuaji yameokoa maisha ya watu wengi, asili yake ya kutokubagua seli mara nyingi hudhuru seli zenye afya, husababisha madhara makubwa, na wakati mwingine husababisha mwili kupinga matibabu. Mapungufu haya yamechochea hamu kubwa ya tiba ya kinga (immunotherapy), mbinu inayoufanya mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kuangamiza seli za saratani huku ikipunguza madhara kwa tishu zenye afya zinazozunguka seli hizo.

Timu ya watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran, Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Semnan, Taasisi ya Utafiti wa Chanjo na Seramu ya Razi, Taasisi ya Pasteur ya Iran, na Taasisi ya Saratani ya Motamed, sasa imetengeneza chanjo ya mRNA iliyobuniwa kidijitali inayolenga saratani ya matiti.

Chanjo hiyo inalenga kwa wakati mmoja protini mbili ambazo zina dhima muhimu katika uhai na ukuaji wa uvimbe: VEGFR2 na c-MET. VEGFR2 huwezesha uvimbe kutengeneza mishipa mipya ya damu kupitia mchakato unaojulikana kama angiogenesis, hali inayoruhusu seli za saratani kupata virutubisho na kuendelea kukua. C-MET nayo huchochea ukuaji, uhai, na usambaaji wa saratani (metastasis)—yaani kusambaa kwa seli za saratani katika sehemu nyingine za mwili.

Tofauti na uundaji wa chanjo za jadi, ambao mara nyingi huhitaji majaribio mengi ya kimaabara kwenye sampuli za viumbe na wanyama katika hatua zake za awali, mbinu hii ya in silico (yaani ya kompyuta) inawaruhusu wanasayansi kutathmini wagombea wa chanjo kupitia uigaji wa hali ya juu wa kompyuta.

Licha ya matokeo ya kutia moyo, watafiti wamesisitiza kuwa matokeo hayo kwa sasa yameishia katika tafiti za kompyuta pekee. Kabla ya chanjo hiyo kufikiriwa kwa matumizi ya kitabibu, lazima ipitie uthibitisho wa maabara, majaribio kwa wanyama, na majaribio ya kliniki kwa binadamu ili kuthibitisha usalama na ufanisi wake.

Hata hivyo, utafiti huu unatoa ramani yenye matumaini kwa ajili ya maendeleo ya kizazi kipya cha chanjo za saratani na unaangazia jinsi ubunifu wa kidijitali unavyoweza kupunguza kwa kiasi kikubwa muda na gharama zinazohitajika kutengeneza tiba za kinga dhidi ya saratani zinazolenga shabaha mahususi. Iran hivi sasa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika utafiti wa tiba duniani pamoja na kuwa imewekewa vikwazo. Katika vita vya hivi karibuni vya Israel na Marekani dhidi ya Iran, tawala hizo mbili vamizi zilishambulia kwa mabomu idadi kubwa ya taasisi za kisayansi na vyuo vikuu ili kujaribu kuzuia kasi ya ustawi wa kisayansi nchini Iran lakini watafiti wa Iran wameonysha azma ya kuendeleza kazi zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *