Kwa mujibu wa UNECE hii ni hatua mpya katika historia ya usafiri wa barabarani. Uamuzi huo ulifikiwa na Jukwaa la Dunia la Kuratibu Kanuni za Magari (WP.29), ambalo limeweka viwango vya pamoja vya usalama vitakavyowezesha magari yenye mifumo ya kujiendesha yenyewe, maarufu kama Automated Driving Systems (ADS), kuanza kufanya kazi chini ya mfumo mmoja wa kimataifa.

“Hatua hii ni mafanikio makubwa katika historia ya udhibiti wa usafiri duniani. Kwa mara ya kwanza, dunia ina mfumo wa pamoja wa kuhakikisha magari yanayojiendesha kikamilifu bila dereva yanakuwa salama, yanawajibika na yanaaminika,” imesema UNECE katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi.

Usalama kwanza kabla ya ubunifu

Kanuni hizo mpya zinahitaji watengenezaji wa magari kuthibitisha kuwa mifumo yao ya kujiendesha inaweza kufanya kazi kwa kiwango kinacholingana au kuzidi uwezo wa dereva mwenye ujuzi.

Makampuni yatahitajika kuwasilisha ushahidi wa kina wa usalama kupitia mfumo unaoitwa “Safety Case”, kufanya majaribio ya kuaminika katika mazingira halisi na ya kidijitali, na kufuatilia utendaji wa magari hayo mara yatakapoanza kutumika barabarani.

“Teknolojia ya kujiendesha haiwezi kutegemea ahadi pekee. Lazima ithibitishwe kwa ushahidi kwamba hailengi kuweka maisha ya watu katika hatari zisizo za lazima,” imesisitiza UNECE.

Kanuni hizo pia zinataka magari yote yenye ADS kuwa na mfumo wa kuhifadhi taarifa muhimu za usalama ili kusaidia uchunguzi na ufuatiliaji wa matukio yatakayotokea.

Mataifa makubwa yaunga mkono mfumo huo

Mfumo huo mpya umeungwa mkono na baadhi ya masoko makubwa zaidi ya magari duniani, yakiwemo Marekani, China, Muungano wa Ulaya, Japan, Canada na Uingereza.

Kwa mujibu wa UNECE, hatua hiyo itasaidia kuepusha hali ambapo kila nchi ingeweka sheria zake tofauti, jambo ambalo lingeweza kuchelewesha maendeleo ya teknolojia na kuongeza gharama kwa watengenezaji.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa “Kanuni zilizoratibiwa kimataifa zinatoa uwazi kwa wazalishaji, zinajenga imani kwa watumiaji na zinafungua njia ya kupanua wigo wa ubunifu kwa usalama katika masoko mbalimbali dunianiā€.

Mbali na kupitisha kanuni mpya za ADS, WP.29 pia imefanyia marekebisho takribani kanuni 90 za Umoja wa Mataifa kuhusu magari ili kuhakikisha mfumo uliopo unaendana na enzi mpya ya magari yanayojiendesha yenyewe, ikiwemo yale yasiyokuwa na usukani wala vidhibiti vya kawaida vya dereva.

Kanuni hizo mpya zinatarajiwa kuanza kutumika rasmi ndani ya mwezi mmoja, zikifungua ukurasa mpya katika safari ya kuelekea usafiri wa zama zijazo unaotegemea akili mnemba na mifumo ya kiotomatiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *