BODI ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeanza rasmi utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa mfumo huo na kuhakikisha changamoto zinazojitokeza zinapatiwa ufumbuzi bila kurejea kwenye biashara holela ya mazao.
Akitoa taarifa baada ya kutembelea mikoa ya Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Morogoro na Iringa, Mkurugenzi Mtendaji wa WRRB, Asangye Bangu, amesema ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya bodi hiyo yaliyofanyika Mei 19, 2026 jijini Dodoma.
Bangu amesema katika ziara hiyo alikutana na viongozi wa mikoa, wilaya pamoja na Kamati za Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kujionea namna mfumo huo unavyotekelezwa katika zao la ufuta.
“Nimeridhishwa na namna serikali za mikoa zinavyoendelea kushirikiana na WRRB katika kuhakikisha mfumo unasimamiwa vizuri. Viongozi wote tuliokutana nao wameonesha utayari mkubwa wa kusimamia utekelezaji wa mfumo huu na kushughulikia changamoto zinazojitokeza,” amesema.

Amesema moja ya maelekezo makubwa yaliyotolewa na Waziri Mkuu ni kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika mfumo huo hazitumiki kama sababu ya kurejea katika biashara holela ya mazao, bali zitafutiwe ufumbuzi kwa wakati.
Kwa mujibu wa Bangu, baadhi ya changamoto zilizobainishwa zinahusisha miundombinu ikiwamo ujenzi wa maghala, matengenezo ya barabara na uboreshaji wa mazingira ya kurahisisha usafirishaji wa mazao yanayopitia katika mfumo huo.
Amesema WRRB imeweka mikakati mahsusi ya kuimarisha ubora wa mazao kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na wilaya ili kuhakikisha bidhaa zote zinazopelekwa maghalani zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

“Tumewaelekeza waendesha maghala kuzingatia kikamilifu miongozo iliyotolewa na taasisi husika. Kwa sasa zao lililo sokoni ni ufuta na tayari miongozo ya utekelezaji imetolewa na COPRA,” amesema.
Kuhusu upungufu wa maghala, Bangu amesema WRRB imeanza mazungumzo na halmashauri mbalimbali ili kutafuta namna ya kutumia fursa za uwekezaji katika miundombinu hiyo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa mfumo na kuwafikisha wakulima karibu zaidi na minada.
Aidha, amesema WRRB kwa kushirikiana na COPRA imeanza kuangalia uwezekano wa kuongeza mazao mengine katika mfumo huo ikiwamo karanga, njugu mawe na choroko ili kupanua wigo wa wanufaika.

Akizungumzia changamoto ya mdororo wa bei, Bangu amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakilinganisha bei za sasa na zile za miaka mitatu iliyopita bila kuzingatia mabadiliko ya soko la dunia, hivyo bodi hiyo imeendelea kutoa elimu kuhusu mwenendo wa bei katika masoko ya kimataifa.
Pia amesema baadhi ya maeneo yamekumbwa na upungufu wa uzalishaji kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa mbegu bora, huku WRRB ikianza mazungumzo na Jeshi la Magereza Tanzania ili kutumia mashamba yake kuongeza uzalishaji wa mbegu.
Bangu amewahakikishia wananchi kuwa mfumo wa stakabadhi za ghala unaendelea kuimarishwa na kwamba changamoto zote zinazojitokeza zitapatiwa ufumbuzi kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali.
“Tunapoendelea kushirikiana na wadau wote, tunaamini tutamkomboa mkulima wa Tanzania na kuhakikisha anapata thamani halisi ya mazao yake,” amesema.