
KIGOMA: MANISPAA ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma inaelezwa kukumbwa na vitendo visivyo vya kimaadili hatua inayopelekea kuporomoka kwa maadili na utamduni wa mji huo.
Kutokana na hali hiyo, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Mussa Maulid amewataka wananchi wa mkoa huo ametaka kukemewa kwa nguvu zote vitendo vyovyote vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili.
Meya Maulid amesema hayo akifunga Tamasha la Utamaduni la Ujiji lililofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Kawawa Ujiji mjini Kigoma ambapo amesema kuwa watu wote wanapaswa kuwakemea na kuwafichua wale wanaoleta matamasha ya ushoga katika mji wa Ujiji.

Alisema kuwa mji huo bila kujali itikadi za kidini umekuwa na mila na desturi za malezi kwa vijana na maisha kwa jumla ambazo zilizingatia maadili, heshima na utu wa mtu, lakini kwa sasa mambo hayo yametiwa doa na tamaduni mbalimbali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi ya Taasisi ya Ujiji Heritage & Development Organization, Hassan Kabeke amesema kuwa anaungana na meya kukemea mmomonyoko wa maadili yanayotokea Kigoma Ujiji ikiwemo kuwepo kwa matamasha ya ushoga ambayo siyo mila na tamaduni za watu wa mji huo.

Shekhe Kabeke ambaye ni Shekhe wa Mkoa Mwanza amesema kuwa watu wa mji huo wasikubali tabia za watu wanaokuja na fedha na kuwataka kufanya mambo ambayo siyo mila na tamaduni zao kwa maana ya kusimamia maslahi yao hivyo wakatae fedha zinazoletwa zinazolenga kuharibu taswira ya mji huo wa kihistoria.