DC Arusha: Bima ni kinga ya uchumi wa familia na taifaDC Arusha: Bima ni kinga ya uchumi wa familia na taifa

ARUSHA: Wadau wa sekta ya bima nchini wametakiwa kuongeza juhudi za kuwafikia wananchi, hususan waendesha bodaboda na mama lishe, ili kuongeza uelewa na matumizi ya huduma za bima kwa lengo la kuwakinga dhidi ya majanga yanayoweza kuathiri maisha yao na shughuli za kiuchumi.

Wito huo umetolewa jijini Arusha na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ambapo hotuba yake ilisomwa na Mkurugenzi wa Huduma za Bima ya Afya kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Samuel Mweu, wakati wa maadhimisho ya Bima Walk 2026 yaliyolenga kutoa elimu ya bima kwa wananchi na makundi mbalimbali, ikiwemo waendesha bodaboda na mama lishe.

Mkude alisema bima ni nguzo muhimu katika kulinda uchumi wa familia, biashara na taifa kwa ujumla, hivyo kila mwananchi anapaswa kuwa na bima ili kujihakikishia usalama wa maisha ya sasa na ya baadaye.

“Bima ni kinga ya uchumi wa familia, biashara na taifa kwa ujumla. Hivyo wananchi wanapaswa kuitumia ili kujilinda dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na majanga mbalimbali,” alisema Mkude.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Bima Walk 2026, Ismail Samah Hali Suleiman, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapa elimu kwamba bima ni huduma muhimu kwa kila mtu bila kujali kipato chake.

“Tunataka wananchi waelewe kwamba bima siyo ya matajiri pekee, bali ni kwa ajili ya kila mtu kwa sababu kila mmoja anaweza kukumbwa na janga wakati wowote,” alisema Suleiman.

Naye mwakilishi wa waendesha bodaboda mkoani Arusha, Mourice Bosaseli, alipongeza programu hiyo akisema imewasaidia kupata uelewa kuhusu umuhimu wa bima katika kulinda maisha, afya na shughuli zao za kila siku.

“Bima ni uhai, bima ni maisha na bima ni uhakika wa kesho yako. Sisi waendesha bodaboda tunahamasisha matumizi ya bima kwa sababu ndiyo kinga yetu dhidi ya changamoto zinazoweza kutokea wakati wa kazi,” alisema Bosaseli.

Wadau wengine waliohudhuria maadhimisho hayo wamesema elimu zaidi inahitajika ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, wakisisitiza kuwa bima haipaswi kuonekana kama huduma ya matajiri pekee bali ni ya kila mtu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *