
Watu 164 wamethibitishwa kupoteza maisha nchini Venezuela baada ya kutokea kwa mitetemeko miwili ya ardhi siku ya Alhamisi, huku watu wengine ambao hawajaonekana wakitafutwa kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka huku idadi ya vifo ikitarajiwa kuongezeka.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Watalaam wa jiolojia wanasema mitetemeko hiyo miwili ilikuwa na ukubwa wa Ritcha 7.2 na 7.5, na ilitokea Magharibu mwa jiji kuu Caracas na kusababisha majengo marefu kuporomoka.
Rais wa mpito Delcy Rodriguez amesema watu wengine karibu Elfu moja wamejeruhiwa, huku maeneo ya La Guaira Kaskazini mwa Caracas, yakiathiriwa zaidi.
Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Simon Bolivar uliopo jijini Caracas umeharibiwa vibaya na kufungwa hatua ambayo imeathiri misaada ya kibinadamu kuwasili nchini humo kwa haraka.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio, amesema nchi yake inafanya kinachowezekana kutoa msaada wa haraka hasa kusaidia kuokoa watu waliokwama kwenye vifusi na kutoa misaada ya kibinadamu.
Naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema ametuma waokoaji 85 kwenda nchini Venezuela kusaidia kwenye shughuli ya uokoaji.
Mara ya mwisho kwa Venezuala kushuhudia tetemeko kama hili ilikuwa mwaka 1997 ambapo watu 73 walipoteza maisha jijini Caracas.
Hata hivyo, mwaka 1967, watu 236 walipoteza maisha baada ya kutokea kwa tetemeko lingine la ardhi.